The House of Favourite Newspapers

INASIKITISHA! MTOTO ATEKWA, ACHINJWA

BUKOBA: Wakati watoto wawili, Idrisa Ally (13) na Gabriela Kilimba (3) wa jijini Dar wakiwa hawajulikani walipo baada ya hivi karibuni kutekwa na watu wasiojulikana, tukio lingine baya limetokea la mtoto Clavery Lucas (7) kukutwa amechinjwa, Risasi lina habari hii ya kusikitisha.  

 

Mtoto huyo asiye na hatia ambaye ni mwanafunzi wa chekechea inadaiwa usiku wa Oktoba 2, 2018 alitekwa kisha kuuawa kikatili na watu wasiojulikana ambao baada ya kutekeleza unyama huo, walimtelekeza shambani jirani na nyumbani kwao, Kijiji cha Nyakigando, Kata ya Kaibanja Wilayani Bukoba.

 

Akizungumza na gazeti hili, baba wa mtoto huyo, Lucas Clavery alisema kuwa, Oktoba 1, mwaka huu mama mzazi wa mtoto huyo aliyefahamika kwa jina la Jenipha Joseph aliondoka nyumbani na kwenda Kijiji cha Kilimilile kulikokuwa na msiba huku akimuacha Clevery.

 

“Kule Kilimilile kulikuwa na msiba wa shangazi yake na mke wangu, yeye akaondoka na kuniacha na Clavery ila na mimi nilikuwa na safari ya kwenda huko msibani. “Kwa hiyo kesho yake (Oktoba 2) nikamwambia Clavery aende kwa bibi yake aitwaye Rhoda (umbali wa kilomita 1). Mimi na rafiki yangu tukaondoka kwenda kule msibani kwa usafiri wa baiskeli,” alisema baba huyo.

 

Ikaelezwa kuwa, baada ya mzazi huyo na mwenziye kuwaona wafiwa, walianza safari ya kurejea nyumbani ambapo saa nne usiku walipofika kwa bibi Rhoda kwa lengo la kumchukua Clavery, wakakutana na taarifa za kwamba mtoto huyo licha ya kushinda nyumbani hapo lakini aliondoka jioni na haijulikani alipo. “Mpaka saa nne usiku Clavery alikuwa hajulikani alipo na sisi tulipofika pale na kupewa taarifa hizo ilibidi turudi nyumbani haraka tukidhani huenda alienda huko.

 

“Inauma sana kwani tulipofika karibu na nyumbani, kwenye shamba lililopo jirani tulikutana na mwili wa mwanangu ukiwa umetapakaa damu, inaonesha alichinjwa. Tulishitushwa sana na tukio hilo, hatuamini tulichokuwa tunakiona mbele yetu,” alisema Lucas kwa masikitiko.

 

Inazidi kuelezwa kuwa, kufuatia hali hiyo mzazi huyo alipiga kelele na ndipo walipofika wanakijiji na kushuhudia mtoto huyo akiwa amelala chini, damu ikiwa imetapakaa. Mmoja wa majirani aliyejitambulisha kwa jina moja la Sued alisema kuwa, mauaji hayo yamewasikitisha hasa ikichukuliwa kwamba, mtoto huyo hana hatia yoyote.

 

“Kwa kweli hili tukio limetuumiza sana, unajiuliza kuwa, mtoto wa watu kawakosea nini hadi wamuue kinyama hivi? Mimi naliomba jeshi la polisi liwatafute waliohusika na mauaji haya na hatua stahiki zichukuliwe,” alisema Sued. Naye jirani mwingine aitwaye John alisema kuwa, yawezekana mtoto huyo ameuawa na watu ambao walikuwa na uhasama na wazazi wake hivyo ni vyema upelelezi ukafanyika haraka.

 

Hata hivyo, baba wa marehemu alipoongea na gazeti hili alisema kuwa, hana uhasama wowote na mtu hivyo anashindwa kuelewa ni kwa nini mwanaye ameuawa kikatili hivyo. Diwani wa Kata Kaibanja, Jasson Lwankomezi alielezea kusikitishwa na mauaji hayo na kusema kuwa kwa kushirikiana na polisi watahakikisha wauaji wanapatikana na kupelekwa kwenye vyombo vya sheria.

 

Mpaka sasa inadaiwa watu watatu wanashikiliwa kwa kuhusishwa na tukio hilo. Jitihada za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, SACP Augustine Ollomi kuzungumzia tukio hilo hazikuzaa matunda kufuatia simu yake ya mkononi kutokuwa hewani. Gazeti hili linalaani vikali mauaji hayo, linawapa pole wafiwa na linaomba vyombo vya dola vihakikishe waliohusika na tukio hilo wanapatikana na hatua kali zinachukuliwa ili kukomesha vitendo hivyo vya kinyama.

STORI: Abdullatif Baisy, Risasi Jumamosi

INASIKITISHA! Afungiwa Bandani Zaidi ya Mwaka, Maisha yake ni Hatari!

Comments are closed.