The House of Favourite Newspapers

INAUMA SANA… MKE AUAWA KWA SHOKA

Waombolezaji wakilia msibani.

GRACE Mwakipesile, mkazi wa UbungoKibangu jijini Dar, anadaiwa kuuawa kwa shoka, Amani lina mkasa kamili. Kwa mujibu wa chanzo makini kutoka eneo la tukio, mauaji hayo yalitokea usiku wa Jumamosi iliyopita ambapo Grace alikuwa nyumbani na mumewe hadi baadaye ilipobainika kuwa Grace amefariki dunia kwa kupigwa na shoka shingoni na mgongoni.

“Nilishangaa sana baada ya kusikia kuwa Grace ameuawa kwa kupigwa shoka licha ya kwamba mara kadhaa tuliwahi kusikia malumbano kati ya Grace na mumewe, lakini siku hiyo sijui nini kilitokea,” kilidai chanzo.

Kikizidi kuelezea tukio hilo, chanzo hicho kilidai kuwa, siku ya tukio, ilipofika saa 1:00 usiku, mzee Kamugisha (mume wa marehemu) alionekana akichoma nguo zake moto bila kusema sababu ya kufanya hivyo.

CHANZO CHAFUNGUKA

“Siku za nyuma Grace na mumewe walikuwa na migogoro ya hapa na pale, lakini siku hiyo sijui hata nini kilitokea maana hatukusikia ugomvi wowote hadi pale tulipoambiwa ameuawa,” kilidai chanzo hicho.

Siku ya mazishi.

KUHUSU MIGOGORO

Kikiielezea familia hiyo, chanzo hicho kilidai kuwa, mara kadhaa Grace na mumewe waliwahi kufikishana katika Ofisi za Serikali ya Mtaa kwa kuwa na tofauti mbalimbali. “Yaani walikuwa na migogoro ya mara kwa mara na iliwafanya wafikishane Ofisi ya Serikali za Mtaa kushitakiana na kupata suluhu.

MTOTO AGUNDUA KUUAWA KWA MAMA

“Siku ya tukio, sijui ilikuwaje maana kila mtu alikuwa
akiendelea na mambo yake, lakini ilipofika saa 4:00 usiku, mmoja wa watoto wa marehemu alikwenda kugonga kwenye mlango wa mama yake ndipo akabaini kuwa ameuawa na alipomtafuta baba yake, hakuwepo nyumbani,” kilidai chanzo hicho.

POLISI WAUCHUKUA MWILI

Mara baada ya majirani kupewa taarifa na kukusanyika, walitoa taarifa polisi ambao walifika mara moja na kuuchukua mwili kisha baadaye kumtia mbaroni mumewe.

UJUMBE WAKUTWA

Hata hivyo, chanzo hicho kilieleza kuwa, wakati wa kuutoa mwili, polisi walikuta ujumbe ambao ulionekana kuachwa baada ya tukio hilo. “Wakati polisi wakiendelea kupekua mle ndani, walibaini kuna ujumbe wa karatasi uliosomeka: “Nimeteseka kwa miaka 38 na kuona bora nife.” Gazeti la Amani, lilifika eneo la tukio, lakini familia hiyo haikuwa tayari kutoa ushirikiano na hata alipotafutwa mmoja wa watoto kuzungumzia tukio hilo, alisema kuwa, yeye si msemaji wa familia.

MWENYEKITI ATHIBITISHA

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Desdeu Ishengoma alithibitisha kutokea kwa tukio hilo mtaani kwake. “Ni kweli marehemu na mumewe ni wananchi wa mtaani kwangu na ni kweli tukio hilo limetokea, huyo mwanamke amekutwa akiwa ameuawa kwa shoka,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu kuwepo kwa mgogoro kati ya wanandoa hao, mwenyekiti huyo alikiri kuwepo kwa mgogoro baina ya wanandoa hao. Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, ACP
Salum Hamduni alipotafutwa kuhusiana na tukio hilo, alikiri kutokea na kueleza kuwa wanamshikilia mume wa marehemu kwa ajili ya uchunguzi.

“Taarifa za tukio hilo ninazo na huyo mume wa marehemu tumemkamata, shitaka lake lipo Kinondoni linafanyiwa upelelezi.” wili wmarehemu Grace ulisafirishwa Jumanne iliyopita kuelekea jijini Mbeya kwa mazishi.

STORI: WAANDISHI WETU| AMANI

Breaking News: Chadema Wafunguka Lissu Aachiwe, Ngeleja Akamatwe!

Comments are closed.