The House of Favourite Newspapers

Itilima: Waganga Wamiminika Kuchanjwa

0

WILAYA ya Itilima iliyopo mkoani Simiyu inatajwa kuongoza kwa idadi ya watu wanaojitokeza kupata chanjo dhidi ya ugonjwa wa uviko19 mkoani humo. Wilaya hiyo inatajwa kuwa miongoni mwa wilaya zenye waganga wengi wa tiba asilli na inakadiriwa kuwa zaidi ya waganga elfu saba.

 

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Faiza Salim, wakati akitoa taarifa juu ya hali halisi ya uchanjaji wa chanjo ya UVIKO19 inavyoendelea wilayani humo ambapo amesema jamii imehamasika vya kutosha huku Idadi kubwa ya wanaojitokeza wakiwa waganga wa tiba za asili na wateja wao na kwamba hadi kufikia Ock 2,2021 walikuwa wamemaliza chanjo zote.

 

“Tulianza hamasa Kata kwa Kata kwahiyo kutoka chanjo 60 ambazo tulikuwa tunachanja kwa siku tukafikia kuchanja chanjo 782 kwa siku… mafanikio yetu ni shirikishi…tulikutana na waganga wa tiba asili walikuwa 120 ambao ni viongozi.

 

Waliochanja siku hiyo walikuwa 82… awali tulipewa chanjo 3320 na zilivyoisha tuliongezewa nyingine 910 na kufikia chanjo 4230 ambapo mpaka Oct 3, 2021 tumechanja chanjo 3584 sawa na asilimia 108 na hivyo kubakiwa na chanjo 646.

 

Tunaamini siku hizi mbili au leo tunamaliza hizi zilizobaki, serikali imedhamilia kuongeza chanjo hivyo wananchi wazidi kujitokeza” amesema DC Faiza.

 

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Itilima Dkt. Anold Musiba amesema walipoanza walikuwa na vituo vitatu ambavyo watu walikuwa wakipata huduma ya chanjo na mwendo haukuwa mzuri na walipogundua hilo wakaongeza juhudi za kuongeza elimu kwenye jamii ambapo walifikia makundi tofauti tofauti ikiwemo waganga tiba asili kutokana na kundi hilo kuwa na watu wengi nyuma yao hivyo hatua iliyopelekea kufanikiwa kwa zoezi hilo kutokana na wengi wao kujitokeza kwa wingi wakiwa na wateja wao.

 

Naye mwenyekiti wa waganga wa Tiba Asili Wilaya ya Itilima, Shija Limbe, amesema waganga baada ya kupewa ukweli dhidi ya chanjo hiyo wamehamasika tofauti na awali walivyokuwa wakipotoshwa kuwa mtu akichanjwa damu inaganda, sehemu aliyochomwa chanjo hiyo ukiweka balbu inawaka kitu ambacho waligundua kuwa ni upotoshaji na hivyo wakaamua njia sahihi ya kuchanja.

 

Awali Mkuu wa Mkoa huo, David Kafulila, aliwapongeza wakuu wote wa wilaya zilizopo mkoani humo ambao wilaya zao zinaendelea kufanya vizuri kwenye zoezi hilo kwa jitahada kubwa wanazozifanya kuwahamasisha wananchi kupata chanjo dhidi ya UVIKO- 19 huku akiwataka wananchi ambao bado hawajachanjwa kuendelea kujitokeza kupata chanjo hiyo ambayo ni muhimu kiafya.

Na Anita Balingilaki

Leave A Reply