The House of Favourite Newspapers

Jafo Afungukia Suala La Kugombea Urais -Video

0


MBUNGE wa Jimbo la Kisarawe ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Selemani Jafo amefungukia suala la kugombea urais endapo ataombwa kufanya hivyo.

Jafo amefungukia jambo hilo mapema leo kwenye kipindi cha Front Page kinachorushwa na +255GlobalRadio mara baada ya kuulizwa kama atakuwa tayari kugombea urais miaka ijayo na ndipo aliposema suala hilo sio kipaumbele chake.

“Kiti cha urais bwana mh! Mara nyingi hilo huwa nasema ni mipango ya Mungu. Mimi sasa hivi nawatumikia wananchi wa kawaida, haya mimi nayaona ndio ya msingi kuliko hayo makubwa. Hayo tumuachie mheshimiwa rais anatuongoza vizuri,” alisema Jafo.

Kwenye mahojiano hayo, Jafo alizungumzia pia mafanikio mbalimbali ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imeyapata.

“Binafsi nipende kushukuru Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dr John Pombe Magufuli, imekuja na staili ya tofauti sana hasa katika kuwekeza kwenye miradi mikubwa.

“Tunayo miradi ya Standard Gauge, kuna Stiegler’s Gorge ambayo kuna vijana wengi sana wa Kitanzania wapo pale, kuna ujenzi wa vituo vya afya zaidi ya mia nne na tano na kila kituo cha afya kinachukua mafundi zaidi ya ishirini,” alisema Jafo.
Waziri Jafo alisema katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali, wameafanikiwa kwa kiasi kikubwa katika mapambano ya rushwa na sasa nchi ipo kwenye nafasi nzuri kiuchumi.

“Kwanza ajenda ya rushwa sio ya mchezo ndio maana unaona kuna watu wengi misingi yao ya biashara imeporomoka kwa sababu walikuwa wanatumia rushwa,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu baadhi ya mitazamo ya watu ambao wanakosoa kuhusu miradi mikubwa inayoendelea kwamba pengine ni mzigo kwa Taifa, Jafo alitofautiana na mitazamo hiyo.

“Nchi isipofanya kazi watu wanasema hivi, nikichukua hansadi za nyuma watu walikuwa wanasema nchi gani hii haina ndege hata moja, leo hii ndege zipo, shule, vituo vya afya vinajengwa watu tena wanaanza kulalamika lakini hii ni kwa sababu kuna watu walikuwa wanapata fedha kutoka kwa watu ambao wanaingiza fedha kwa njia za ujanja ujanja,” alisema.

Waziri Jafo alisema, kwa kiasi kikubwa kupitia wizara ya TAMISEMI, wamefanikiwa kuongeza mapato kwa sababu ya kuweka mfumo wa kisasa wa ukusanyaji mapato na halmashauri nyingi zimekuwa zikivuka malengo ya ukusanyaji.

Kusikiliza vipindi vingine vya +255GlobalRadio, pakua App ya Global Publishers katika simu janja.

Stori: Erick Evarist

Leave A Reply