The House of Favourite Newspapers

Jamani Kaka Cheni …Ndiyo Nini Sasa?!

0

Mama alikaa uani akiosha vyombo. Aliponiangalia nikitoka chumbani kwangu aliacha kuosha, akaonesha dalili za kuzubaa huku akinikazia macho na kuniuliza…
“We Tina una nini… mbona umekuna sana uso?”
“Sina kitu mama…”
“Huna kitu wakati sura yako inaonesha una kitu? Umechukia nini?”
“Usingizi tu mama, haujaisha sawasawa…”
“Sasa kama usingizi haujaisha sawasawa nani kakulazimisha kuamka?”
Badala ya kumjibu mama, niliangalia nyuma yangu ambapo kuna mlango wa kuingia chumbani kwangu na mlango wa kuingia chumbani kwa kaka ‘angu, anaitwa Cheni. Nilizoea kumwita kaka Cheni.
Kaka Cheni na mimi tuliachiana ziwa kunyonya. Tumesoma wote shule ya msingi, darasa moja licha ya yeye kuwa ni mkubwa kwangu kwa tofauti ya miaka miwili. Nadhani pengine umbo linachangia, maana mimi nina umbo kubwa.
Urefu tuko sawa, lakini nimemzidi wowowo, rangi nyeupe na mng’aro wa ngozi yangu. Watu wanasema tumefanana lakini mwanamke ni mwanamke tu bwana! Mimi nina macho mazuri ya golori yeye yake ya kiume, makavu kama mjusi kabanwa na mlango.
Katika maisha yetu ya undugu, nimekuwa nikimshuhudia kaka Cheni akikua mpaka kubadilika sauti, hasa baada ya kumaliza darasa la saba. Sauti ilianza kuwa nzito kiasi kwamba alipokuwa akiongea yeye, nje watu walijua ni baba.
Wakati anaanza kutamani wasichana, alikuwa akigombana sana na baba na mama wakimwambia akiharibu watoto wa watu mzigo ataubeba mwenyewe. Lakini kaka Cheni hakuwahi kujirekebisha kuhusu hilo.
Wasichana wengi mtaani kwetu, mfano Mage, Joy, Asha, Mwajuma, Kidawa, Halima, Moureen, Asumta, Doto, Aisha, walikuwa wakinitania mimi kwa kuniita wifi Tina kwa sababu ya kaka Cheni kuwatokea.
Wazazi walipoona sasa kijana wao amekuwa hashikiki, waliamua kumwamishia kwenye chumba cha nje ambacho kimepakana na changu.
Sasa ili uingie chumbani kwa kwangu au kwa kaka Cheni ilikuwa lazima utoke ndani kuja nje au uani. Kwa hiyo mimi na kaka Cheni ndiyo pekee tulikuwa tunaishi vyumba vya nje. Ndani nyumba kubwa waliishi wazazi wetu lakini pia aliishi bibi mzaa mama. Kaka yetu mkubwa alikuwa akiishi Arusha kikazi na alishaoa siku nyingi.
Nyumba za uswahilini zinajulikana jamani! Chumba na chumba vilitenganishwa na ukuta tu lakini juu hakukuwa na kitu, yaani kama mimi nililala nikazima taa halafu kaka Cheni akawa hajalala akawasha taa, mwanga wake ulifika mpaka chumbani kwangu.
***
“Sasa unapoangalia mlangoni una maana huo usingizi ndiyo upo pale? Halafu mbona nakusikiaga usiku mkitupiana maneno na kaka yako, kwani kunakuwaga na nini? Kwa nini hamuheshimiani lakini?” mama aliuliza.
Ni kweli, siku tatu nyuma nilijibizana na kaka Cheni. Mimi nina jamaa yangu, akinihitaji namfuata gesti au baa kukaa. Yeye kaka Cheni akiwa na wasichana wake anawaleta chumbani nyumbani, ndipo kelele zangu kwake ni hizo…
“Hakuna kitu mama,” nilimjibu mama kisha naye akaendelea na kuosha vyombo.
Mara, kaka Cheni akatokea akiwa anafikicha macho kuashiria kwamba naye alikuwa akiteswa na usingizi kama mimi…
“Haaa! Haa! We Cheni, ina maana ulikuwa bado umelala?” mama alimuuliza kaka Cheni ambaye alikubali kwa kutingisha kichwa…
“Yaani mtoto wa kiume unalala mpaka jua linatoka, husikii aibu? Vijana wenzako wote mtaani wameshatoka…Mgunda amepita nje sasa hivi…Mashaka nimemwona na baba yake wanakwenda mjini…wewe bado umelala.”
Kaka Cheni akaonekana kuchukia, akarudi chumbani. Baada ya muda akafungulia redio kwa sauti ya juu huku akifuatisha wimbo uliokuwa ukipigwa.
Nilisimama nikaenda kuoga, nilipotoka nilijiandaa na kwenda zangu chuo.
Siku hiyo nilishinda darasani nikijiuliza kama maisha ya kaka Cheni pale nyumbani ni sahihi. Si kwa maana ya kuishi bali kwa maana ya vitendo vyake. Kwanza hana kazi maalum lakini anapiga pamba ile mbaya.
Nilijiuliza hata videmu vyake anavipa nini mpaka kumpenda kiasi kile. Maama mimi mtaani umaarufu wangu ulitokana na kaka Cheni.
“Nitamshauri kaka Cheni ahame. Atafute chumba akapange kokote kwingine, pale nyumbani si sahihi tena kwake,” niliwaza moyoni.
***
Ilikuwa saa mbili na nusu usiku, tulikuwa sebuleni tunakula, mimi nakula na mama na bibi, kaka Cheni anakula na baba kwenye meza yao. Kwa mbali mimi nilisikia mlio wa mlango wa chumba cha kaka Cheni ukifunguliwa, nilimtupia jicho baba akaonekana hajasikia, nikamwangalia mama, pia akaonesha hajui kinachoendelea, nikamwangalia kaka Cheni mwenyewe, akanifinya jicho.
Ina maana yeye alijua kuna mtu kaingia chumbani kwake. Mimi kwa haraka tu nikajua ni mmoja kati ya mademu zake maana sijawahi kumwona mwanaume kaingia chumbani kwake zaidi ya kuishia nje.
Palepale kaka Cheni akanawa, akasimama ili aondoke…
“Cheni,” aliita baba…
“Naam…”
“Kaa hapo,” baba alisema kwa sauti yenye mamlaka. Kaka Cheni akakaa…
“Mimi nani?”
“Baba…”

Je, unajua nini kiliendelea huko? Usikose kusoma kwenye gazeti hilihili, wiki ijayo.

JIUNGE NA GLOBAL BRAKING NEWS

GLOBALBREAKINGNEWS100.jpg

Leave A Reply