The House of Favourite Newspapers

Ndugu Zangu Walinichukua Msukule-8

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Nilipoangalia, ajabu nikaona nyasi zikining’inia kuelekea niliko mimi, nikazishika na kuzitumia kutokea mle ndani ya pango.ENDELEA MWENYEWE…

Nilivyofanikiwa kutoka kwenye lile shimo tu, ghafla nikawaona wale ndege wakiwa wamenizunguka. Ndipo nikaanza kutembea tena kwa mwendo wa kasi huku wale ndege wakiwa juu, tukienda sambamba kwa hatua kufuata hatua zangu.

Safari ikaendelea mpaka tukafika mahali nikahisi kuchoka na kuishiwa nguvu kabisa. Nilitamani nikae chini lakini ikashindikana kwa sababu wale ndege walinizonga. Lakini pia  nilikuwa nina hofu ya kupata adhabu nyingine kama ile ya kwanza.

Ilifika mahali wakati nimefika kwenye pori moja kubwa sana nikahisi kuishiwa nguvu na kutojimudu tena, nikaanguka chini na kupoteza fahamu moja kwa moja.

Pale sikuwa na kumbukumbu tena mpaka ndugu zangu walipokuja na kunikuta nikiwa nimelala na kuwekewa jiwe kubwa sana kifuani jambo lililowashangaza sana.

Cha ajabu sasa, hilo jiwe lilikuwa likitolewa tu pale kifuani mimi mapigo ya moyo yalisimama na kuwa mfu palepale. Yaani nafariki dunia. Lakini jiwe liliporudishwa mapigo ya moyo wangu yakaenda  kama kawaida na kuwa hai tena.

Ila sikuwa na uwezo wa kuzungumza lolote mbele ya ndugu zangu zaidi ya kuwaangalia tu ndugu zangu ambao walionesha kunishangaa sana.

Hali ilizidi kuwachanganya ndugu zangu na yule mtaalamu mpaka ikabidi waanze kutengeneza machela kwa kutumia miti kwa ajili ya kunibeba ili lile jiwe lisidondoke pale kifuani kwangu na kupoteza maisha moja kwa moja.

Baada ya machela kukamilishwa na ndugu zangu, nilibebwa mpaka sehemu ya karibu na barabarani  ambapo ndugu zangu walikaa kwa muda mrefu kusubiri usafiri wa kunifikisha nyumbani.

Mara, lilitokea gari dogo moja ndipo yule mwenyekiti alilikimbilia na kwenda kuongea na dereva kumwambia kwamba kuna mgonjwa anatakiwa kupelekwa katika kijiji chetu kwa ajili ya kutibiwa na ana hali mbaya sana, yaani mimi.

Dereva alikubaliana na mwenyekiti wa kijiji chetu na safari ya kuelekea nyumbani ikaanza palepale bila kupoteza muda.

Hatimaye tulifika nyumbani na kukuta watu wengi sana. Inaonekana habari zilienea kwamba, mimi nimepatikana nikiwa hai na napelekwa.

Pale nyumbani, niliingizwa ndani kabisa na ndugu zangu japokuwa watu walionesha dalili za kila mmoja kutaka kuniona nilivyo kwa wakati ule baada ya kufariki dunia muda mrefu uliopita.

Mtaalam akaanza kunishughulikia kwa tiba zake ili kwanza nirejewe na fahamu. Kweli kiasi fulani fahamu zilinirejea tena, mtaalamu akaamuru watu, haswa wanaume wa kijiji chetu waende wakafukue mara moja kaburi nililozikwa.

Vijana wa kijijini kwa kushirikiana na wazee wakaenda kulifukua lile kaburi langu. Mimi wakati huo nilikuwa ndani. Wakati wa kulifukua kaburi kila mtu alipenyeza macho kwa lengo la kutaka kuona nini kitakutwa ndani mwake kwani walivyojua wao, mwili wangu ndiyo ulizikwa.

Cha ajabu ndani ya kaburi walikuta kinu ambacho huwa kinatumika kwa ajili ya kutwangia. Lakini hakikuwa kinu cha pale nyumbani kwetu na nilisikia watu wakisema baadhi ya ndugu zangu ndiyo walionichukua msukule kwa lengo la matumizi yao binafsi.

Kila mtu alishangaa kwani hakuna aliyefikiria kama kinaweza kutolewa kitu kama kinu. Mtaalam akakipasua kile kinu ukakokwa moto na mimi nikaambiwa niote ule moto ili moshi wake uliokuwa ukitoka pale uingie mwilini mwangu ili fahamu zinirejee kama zamani na kuwa kawaida.

Nilifanya vile mpaka pale mtaalam aliporidhika kwamba nipo sawasawa akanitoa. Kisha nikaondolewa pale kwenye moto nikapelekwa sehemu nyingine kwa ajili ya kufanyiwa dawa nyingine.

Wakati huo tayari nyumbani kwetu kulikuwa bado kumefurika watu, yaani kijiji chote ni kama kilihamia pale. Lengo kubwa lilikuwa ni kuniona jinsi nilivyo.

Niliendelea kupata matibabu kutoka kwa mtaalam kwa siku kadhaa na haukupita muda mrefu nikawa mzima kabisa, akili zangu timamu na natambua watu na kuongea nao vizuri.

Ndugu zangu pamoja na mwenyekiti wa kijiji walifurahi sana waliponiona nimerejea katika hali yangu ya kawaida. Ikaandaliwa sherehe kubwa sana nyumbani, watu wakala, wakanywa na kusaza. Mtaalam naye baada ya kumaliza kazi akawashauri ndugu zangu kwa kuwaambia kwamba, natakiwa niende Zaire kwa ajili ya tiba zaidi na kwa muda ambao nilikuwa nimefariki dunia mpaka kuja kupatikana nikiwa hai tayari nilikuwa nimeshatimiza miaka mitatu na nusu.

Nilifanya hivyo, nilikwenda Zaire kwa ajili ya tiba zaidi na nilipomaliza nilirudi kijijini na kuendelea na maisha yangu kama zamani. Nilikaa kijijini kwa muda kisha nikaamua kuhamia hapa Dar es Salaam kwa ajili ya kutafuta maisha zaidi ambako mpaka sasa nafanya kibarua mahali.

Namshukuru sana Mungu kwa kuniokoa. Hayo ndiyo yaliyonikuta mwenzenu.

JIUNGE NA GLOBAL BRAKING NEWS

GLOBALBREAKINGNEWS100.jpg

Leave A Reply