The House of Favourite Newspapers

Jenista atoa siku 14 kukagua mikataba ya ajira

0

jenistaWaziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama.

Dar es Salaam.

Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama ametoa siku 14 kwa maofisa kazi wote nchini, kukagua mikataba ya ajira kama inaendana na kanuni na sheria za ajira nchini.

Mhagama alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam, alipotembelea kiwanda cha kutengeneza nguo cha Tooku Tanzania Germent kilichopo Mabibo External, ambacho wafanyakazi wake waligoma Jumatatu ya wiki hii wakiomba kuongezwa mishahara .

Akiwa ameongozana na Naibu wake, Antony Mavunde, na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage aliwataka maofisa kazi kumpa mrejesho baada ya siku 14, huku akitaka uongozi wa kiwanda hicho kumpa majibu ya malalamiko ya wafanyakazi hao ndani ya saa nane.

“Jambo hili halikubaliki wakati kuna maofisa kazi wameajiriwa kwa ajili ya kazi hii. “Naomba mnipe maelezo ya kutosha baada ya siku hizo 14 na uongozi wa kiwanda hiki, nawapa saa nane hadi kufika saa 10:00 jioni(jana) muwe mmenipa majibu sahihi kama mtawaongezea mishahara au mnafunga kiwanda,” alisema.

Awali, Mhagama alikutana na wafanyakazi wa kiwanda hicho na kuwataka kuendelea na shughuli zao wakati wakitafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo.

“Waziri ametuomba tuendelee na kazi suala letu litatatuliwa, tumekubali kuendelea na kazi tukisubiri majibu ya waziri na uongozi ili tujue mwisho wetu nini,” alisema Faith Ruben mmoja wa wafanyakazi kiwandani hapo.

Leave A Reply