The House of Favourite Newspapers

Jeraha Lililojeruhiwa – 05

0

ILIPOISHIA:

“Pambano lilifanyika katika ukumbi maarufu wa Las Vegas Marekani, uwanja ulijaza kila mtu alikuwa na hamu ya kuona majigambo ya mpinzani wangu aliyejitapa kuniulia ulingoni. Kwa maandalizi niliyokuwa nayo mwanzoni niliapa kummaliza mapema ili kumkata ngebe.

 SASA ENDELEA…

“Lakini tatizo lililojitokeza lilipoteza kila kitu na kujikuta nikipanda ulingoni kwa lazima lakini sikuwa mimi ninayejijua. Kama kawaida niliingia ulingoni na wapambe wangu kila mmoja akiwa na matumaini ya kushinda japokuwa kesi yangu iliwachanganya sana.

“Kutokana na uwezo wangu bado mashabiki wangu walikuwa na matumaini ya mimi kushinda pambano hilo. Akili yangu yote haikuwaza pambano zaidi ya kumfikiria mke wangu ambaye ni mama yako. Kila dakika nilijiuliza kitu gani kimempata kufikia uamuzi mzito kama ule!

“Niliamini kabisa hakukuwa na kosa la kudai talaka kutokana na muda niliokaa naye na maisha tulivyoishi ya mapenzi ya dhati. Bado nilikuwa njia panda juu ya uamuzi wa mama yako. Nilijiuliza bila kupata jibu juu ya uamuzi wake wa kikatili kama ule wa kuniacha ghafla.

“Ilikuwa sawa na kuzima chuma cha moto na maji baridi ilikuwa lazima chuma kipinde au kitie ufa. Ulikuwa ukatili wa hali ya juu mtu niliyemkabidhi moyo wangu naye alijua kabisa nampenda kulivunja penzi ghafla, ulikuwa unyama wa hali ya juu.

“Nilikuwa tayari anipe adhabu yoyote  japokuwa sikuwa na kosa lakini si kuniacha. Tangu nijuane na mama yako hatukuwahi kugombana kufikia hatua ya kutishiana kuachana, pamoja na kuwa mimi nilikuwa mbabe wa dunia nilijishusha kwake hata kufikia hatua ya kumuomba radhi nilipomkosea.

“Nilikuwa jogoo nje lakini ndani nilikuwa mume mwema mwenye mapenzi ya dhati kwa mke wangu. Sikuwahi kuwaza hata siku moja kama kuna siku nitatengana na mama yako, mapenzi yake ya dhati yalinitia upofu  na kunifanya nisione mwanamke mwingine yeyote zaidi ya mama yako japo nilipendwa na wanawake wengi wengine wazuri kuliko mama yako lakini moyo wangu niliufunga baada ya mama yako kuingia ndani ya moyo wangu na ufunguo kuutupa baharini.

“Tuliapizana atakayemsaliti mwenzake basi mabaya yampate, pamoja na kuapizana bado niliamini hakuna atakayemsaliti mwenzake na kusahau kila aliae hushika kichwa chake na si cha mwenzake. Pia hakuna aliyemkamilifu zaidi ya Muumba peke yake ndiye hana upungufu.

“Kuhusu kugawana mali nilikuwa nipo radhi kupoteza kila kitu changu lakini si kumpoteza  mama yako. Asikuambie mtu kuachwa na umpendaye ni sawa na kupasuliwa moyo kwa kisu butu tena bila ganzi. Maumivu niliyoyapata baada ya mahakama kuvunja ndoa yangu na mama yako Mungu pekee anajua.

“Narudia kukuambia mali tulizogawana kwangu hazikuwa  kitu kama upendo wa mama yako. Nilisimama kwa vile nilikuwa mwanaume lakini nilipigwa pigo zito maishani mwangu. Niliamini maumivu niliyokuwa nikisikia kama ungetolewa moyo nje ungekuwa unavuja damu kila kona.

“Nilikuwa sina jinsi ilinibidi kukubali kupigana, nilipanda ulingoni kama mgonjwa kila nilipojitahidi kuchangamka akili na mwili vilikataa. Baada ya muda mpinzani wangu aliingia na wapambe wake wakiwa wamebeba jeneza kuonesha siku ile ndiyo kifo changu.

“Maneno yale niliyapuuza kwa vile kwangu hayakuwa ya kwanza wapo waliojitapa lakini hawakufika raundi ya pili. Baada ya kila mmoja kuwa ulingoni tuliitwa katikati kwa mawaidha mafupi kabla ya pambano. Baada ya nasaha fupi  wapambe wetu kutolewa nje ya ulingo na kubaki wanaume wawili wa shoka.

“Kutokana na kutokuwa vizuri kiakili na mwili nilianza pambano kwa kujilinda sana kuliko kushambulia tofauti na kawaida yangu kuanza pambano kwa kasi kubwa.

“Ilikuwa ajabu ya mwaka raundi ya kwanza sikutupa hata ngumi moja zaidi ya kuzuia na kumkumbatia adui yangu kitu kilichomfanya kocha wangu apige kelele muda wote kutokana na adui yangu kunitupia ngumi nyingi ili animalize mapema baada ya kujua nini kinanisumbua.

“Raheem ondoa mawazo ya nje ya ulingo pigania nafsi yako ukifanya mchezo unaweza kufia ulingoni,” Kocha wangu alipiga kelele baada ya kuniona kabisa sikuwepo katika pambano lile.

“Wakati wa mapumziko aliendelea kunisisitiza: “Raheem najua upo katika wakati gani huu ni muda wa kuonesha uanaume wako usikubali kupoteza pambano usimpe sifa bwege huyu hakuwezi.” Nilimkubalia kwa kichwa lakini nilikuwepo ulingoni kimwili akili yangu na mawazo hayakuwepo pale kabisa.

“Raundi ya pili ilipoanza kwa staili ileile ya kukumbatia lakini safari ile nilirusha ngumi za kumzuia adui yangu asinishambulie muda wote. Mchezo wangu uliwaboa watu na kuanza kupaza sauti kuwa lile pambano limepangwa kwa mimi kununuliwa ili nilipoteze.

“Wapambe wangu na watu waliocheza kamari upande wangu walipaza sauti kama nikipigwa kizembe hawakubali wataniua kwa risasi baada ya kuangushwa na kuchanwa juu ya jicho na kufanya damu nyingi zinitoke.

“Kauli zile zilinifanya nibadilike raundi ya tatu kuanza kwa kushambulia na kuweza kumdondosha chini mpinzani wangu na kuufanya ukumbi ulipuke kwa mayowe huku mtangazaji akisema kazi ndo kwanza imeanza.

“Raundi ya nne niliendelea kucheza vizuri kwa kumshambulia adui yangu ambaye naye baada ya kupokea makonde ya nguvu alianza kunikumbatia. Pamoja ya kucheza vizuri bado nilihisi mikono yangu haina nguvu kutokana kutokuwa vizuri kiakili na kimwili.

“Raundi ya sita nilishtushwa na mabango ya kashfa juu yangu yaliyoniita mimi shoga, kwa kweli maneno yaliyokuwa kwenye mabango yalikuwa ya udhalilishaji mkubwa yaliniumiza sana. Ili kuikimbilia ile kashfa nilitaka nilimalize pambano lile mapema kuliko kuendelea kudhalilishwa.

“Niliingia raundi ya saba kama mbogo na kumshambulia adui yangu mfululizo bila kumpa nafasi, katika raundi hiyo nilimchana naye jicho na kumuangusha mara mbili. Kengele ya mapumziko ndiyo iliyomuokoa raundi ile kumpiga KO, kutokana na kupandwa na hasira niliapa hatamaliza raundi inayofuata.

“Ajabu raundi ya nane ilichelewa kwa kisingizio glovu imeharibika wanasubiri nyingine kumbe ile ilikuwa njama ya kumpumzika baada ya kumpa kipigo kizito ambacho ningemmaliza mapema katika raundi iliyofuata.

Kumbe wapinzani wangu walijipanga kwa kila hali kuhakikisha napoteza pambano lile kwa njia yoyote.  Aliingia akiwa na glovu maalum yenye chuma kwa ndani ambayo walipanga kutumia pindi nitakapomzidi nguvu.

Itaendelea wiki ijayo.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

Leave A Reply