The House of Favourite Newspapers

Jeraha Lililojeruhiwa – 3

0

ILIPOISHIA:

“Mmh! Sawa, kama nitakuwa hai hiyo miaka mitano nitakuuliza swali japo sina uhakika kama nitakuwa bado nafanya kazi hii.”
“Nitakuachia mawasiliano yangu ili tuwe tunawasiliana kama nikiondoka.”
“Itakuwa vizuri sana,” Mikias alimwambia Johnson.

SASA ENDELEA…

Johnson na mkewe walikuwa wakimiliki chuo cha urembo cha Moureen Fashion Institute of Technology kilichokuwa jijini New York. Baada ya kufika Zinash alipokelewa na kufanyiwa vipimo vyote ambavyo vilionesha yupo vizuri sana. Baada ya kupumzika wiki moja alianza kujifunza lugha na mazoezi ya kuutunza na kuutengeneza mwili akiwa chini ya Dk. Moureen.

JIJINI CALFORNIA MAREKANI
Raheem Junior alikuwa amekaa pembeni ya baba yake aliyekuwa akisoma kitabu, pamoja na kuwa pembeni ya baba yake mawazo yake yalikuwa mbali sana. Kila muda baba yake alipomtupia jicho alimuona mwanaye yupo mbali kimawazo kitu kilichomfanya aache kusoma kitabu cha James Hard Chase You’re Dead Without Money (Utakufa bila fedha) na kumwita.

“Raheem..Raheem..Reheem ,” pamoja na kumwita mara tatu bado alikuwa mbali kimawazo mpaka alipomshtua kwa kumtikisa.
“E…e…ee,” aliitikia kama yupo kwenye njozi.

“Vipi mwanangu mbona siku hizi umekuwa mwingi wa mawazo?”
“Ni kweli baba, ukimya wako umekuwa unanipa wakati mgumu sana maishani mwangu kila nikikuuliza unaniambia nisubiri muda, mpaka lini kila kukicha afadhali ya jana, kila tukiamka kiza ndicho kinazidi mara dufu mbele ya macho yangu, kwa nini usinipe nuru ya akili yangu japo kwa sekunde moja ili niondoke kwenye kiza totoro kilichoziba akili yangu isijue kesho,” Raheem Jr alisema kwa uchungu mkubwa.

“Mwanangu pamoja na umaskini nilionao najisikia vibaya kukueleza sababu ya mimi kuwa katika hali hii japokuwa miaka kumi na tano iliyopita niliishika dunia mkononi mwangu lakini kuna kitu sikutaka ukijue ambacho kitakutengenezea chuki nzito moyoni mwako.”

“Baba sasa hivi nina miaka kumi na nane ni mtu mzima natakiwa niwe msaada kwako, sitaki nirudie kosa lako itakuwa sawa na kulijeruhi jeraha lililoanza kupona.”
“Una maana gani?”

“Kwa hatua uliyofikia kwa kuikamata dunia mkononi mwako na hali uliyonayo kwa sasa ni vitu viwili tofauti. Inawezekana kuna kosa ulifanya kwa bahati mbaya au makusudi ambalo halitakiwi kurudiwa na mimi mwanao.”

“Ni historia ndefu ambayo huwa sipendi kuizungumza kwani kila nikilikumbuka kovu lililo moyoni mwangu huchubuka upya na maumivu yake huchukua muda mrefu kupoa, hasa nikiutazama umaskini nilionao na utajiri uliopotea. Mwanangu hukuwa wa kuishi maisha ya kuungaunga kama kamba mbovu.”

“Nina imani huu ni muda muafaka wa kulichubua jeraha hilo nikiwa mtu wa mwanzo na mwisho kusababisha maumivu moyoni mwako. Najua ulisema chanzo ni mama na hutamsamehe mpaka unakufa. Japokuwa namchukia mama na nimekubali kuishi na wewe maisha haya ya umaskini lakini mwisho wake nini?

“Nataka leo nijue mimi kumchukia mama yangu ni haki au si haki japokuwa nimekuwa mfuasi wako kwa vile nakupenda sana baba yangu. Japo kuna taarifa nilizisikia zamani juu ya kitendo alichokufanyia mama ambacho kwangu bado sikubaliani nacho mpaka nipate ukweli toka mdomoni mwako na si kusikia kwa watu.

“ Siamini bingwa wa dunia wa ngumi za uzito wa juu kuwa maskini wa kutupa. Ungekuwa mtu wa starehe ningesema sifa zilikulewesha lakini hukuwa hivyo, naomba uniambie ukweli mama kachangia vipi kuharibu maisha yetu?”

“Raheem mwanangu, kila kinachosemwa kipo wazi, kama ulivyosikia na kusoma sehemu mbalimbali juu yangu bingwa asiyepigika niliyefilisiwa na mwanamke.”
“Nimesoma bado siamini kwani nikikuuliza unaniambia nisubiri, nimevumilia lakini sasa ni wakati muafaka.”

“Mama yako ndiye chanzo cha yote hayo, alinunuliwa kwa pesa nyingi ili kuharibu rekodi yangu baada ya wapinzani wangu kushindwa kwa kila mbinu. Niliamini katika maisha yangu sitapigwa na bondia yeyote chini ya ardhi labda atoke moja kwa moja kwa Mungu.

Nimepigana mapambano 62 nimepigwa moja kwa hila jambo lililonifanya niache ngumi.

“Katika mapambano yote niliyocheza 60 nilishinda kwa KO na moja kwa pointi nyingi. Wacheza kamali waliokuwa wapo upande wa pili walipoteza mamilioni ya fedha kutokana na uwezo wangu mkubwa wa kushinda kila pambano lililokuja mbele yangu.
“Walihangaika kila kona kutafuta bondia atakayenipiga nao kuweka fedha nyingi lakini waliishia kupoteza fedha zao. Baada ya kuona hakuna njia nyingine waliamua kumfuata mama yako waliyempa fedha zaidi ambazo ningelipwa kwa pigano langu la mwisho.

“Walifanya mpango wa siri mimi bila kujua tena wakati huo nilikuwa najiandaa kupigana na bondia niliyepigana naye mara mbili. Mara ya kwanza nilimpiga kwa KO raundi ya tatu. Hakukubali alikwenda kujiuliza na kujitapa kuwa nilimbahatisha na kuomba pambano la marudiano.

Kweli pambano lilikuwa gumu kwangu kwa vile jamaa alikuwa amejipanga hasa baada ya kuusoma mchezo wangu. Lakini pamoja na ugumu wa pambano bado nilimpiga raundi ya mwisho baada ya kumpasua chini na juu ya jicho huku jicho lake moja likiwa limevimba na kufumba alikuwa nunda lakini kipigo alikipata cha shetani motoni, lilikuwa pambano la kwanza kukutana na upinzani mkubwa.

“Baada ya pambano lile bado hakukubali aliapa kuomba pambano la mwisho kama nitampiga basi angekubali kuwa mimi ni mbabe wake.
Alijitapa kuwa alikuwa amenijulia na pambano litakalofuata lazima anizamishe. Baada ya pambano lile nilipigana mapambano manne kabla ya kurudiana na Shock na kushinda yote kwa KO za mapema.

“Wakati huo, Shock naye alipigana mapambano matatu na kushinda kwa KO za mapema kama mimi na kujipa moyo wa kunipiga. Pambano hilo lilisubiriwa kwa hamu kutokana na majigambo ya Shock kuwa ataniua ulingoni.
Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wake wiki ijayo.

Leave A Reply