The House of Favourite Newspapers

Unending Love – 71

0

Penzi zito linachanua kati ya vijana wawili wadogo, Jafet na Anna, wote wakiwa ni wanafunzi wa sekondari mbili tofauti jijini Mwanza. Kutokana na Jafet alivyokuwa akimpenda msichana huyo, anaamua kukataa kusomea upadri kwa lengo la kutaka kuja kuoana na Anna, binti kutoka familia ya kitajiri.

Siku zinazidi kusonga mbele, Anna na Jafet wanazidi kukua na kupendana, wanaahidiana mambo mengi mazuri. Kwa bahati mbaya, Anna anapatwa na matatizo ya figo zake moja kushindwa kufanya kazi.

Kutokana na mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, anatoa figo yake moja na kumpa Anna. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa Anna, wazazi wa msichana huyo wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi.

Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani. Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William. Mapenzi yao yanaendelea na baadaye Anna ananasa ujauzito lakini William anamruka futi mia moja.

Anna anaamua kutoroka kurejea nyumbani kwao, Mwanza ambako wazazi wake wanamtoa ujauzito kihalali na huo unakuwa mwanzo wa kulipuka upya ugonjwa wake wa figo. Anasafirishwa mpaka jijini Dar es Salaam anakoenda kulazwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili lakini hali inazidi kuwa mbaya, anapelekwa nchini India.

Jafet anafuatwa na baba yake Anna na kupelekwa India kutokana na shinikizo la msichana huyo. Cha ajabu, japokuwa Anna alikuwa na hali mbaya, Jafet anapowasili nchini India, hali yake inaanza kuimarika kwa kasi na kumshangaza kila mmoja. Kwa pamoja wanakubaliana kwenda kutoa shukrani kwa Mungu wao.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Jumapili ya wiki hiyo, kama walivyokubaliana, wazazi wa Anna walimuombea ruhusa mgonjwa wao kwa ajili ya kwenda kushiriki ibada ya Jumapili katika kanisa lililokuwa jirani na hospitalini hapo. Kwa kuwa hali ya kiafya ya Anna ilikuwa imeimarika sana, waliruhusiwa kirahisi.

Anna na Jafet wakavaa nguo nzuri kisha wakaongozana na wazazi wa Anna mpaka kwenye Kanisa la India Evangelical Lutheran Church lililokuwa kwenye Mtaa wa Karnataka, Mumbai nchini India kwa ajili ya kumshukuru Mungu wao kwa miujiza mikubwa aliyowatendea.

Walipofika kanisani hapo, walipokelewa vizuri na wahudumu wachangamfu na kuelekezwa kuingia ndani, wakaenda kujumuika na mamia ya waumini wengine wa mataifa mbalimbali katika misa ya Jumapili.

Baada ya kumalizika kwa misa hiyo, baba yake Jafet aliinuka na kwenda kuzungumza na mchungaji ambapo alimueleza kwamba anahitaji kufanya maombi maalum ya kumshukuru Mungu kutokana na miujiza aliyoitenda kwa binti yake.

Mchungaji huyo alifurahi kusikia hivyo, akamwelekeza kwenda kuwachukua wenzake na kumfuata kwenye ofisi yake ambako angeenda kuwaongoza katika sala hiyo maalum ya shukrani. Muda mfupi baadaye, baba yake Anna alienda mpaka pale alipoiacha familia yake na kuwaeleza alichoambiwa na mchungaji.

Wakainuka na kuelekea ofisini kwa mchungaji huyo ambaye aliwapokea kwa uchangamfu na kuanza kusikiliza upya maelezo kutoka kwa baba yake Anna pamoja na Anna mwenyewe. Ushuhuda mzito walioutoa, ulimfanya hata mchungaji mwenyewe asisimke sana.

Kwa kuwa bado waumini walikuwa wakiendelea na ratiba nyingine kanisani hapo, alituma ujumbe kwa msaidizi wake kwamba watu wote wasiondoke kwa sababu kuna waumini walikuwa wakitaka kutoa ushuhuda mzito utakaomsisimua kila mmoja.
Mchungaji huyo, Bishop Taraj Williams aliyekuwa na mchanganyiko wa Mzungu na Mhindi aliwaongoza katika sala maalum ya kumshukuru Mungu na walipomaliza, walirudi walipokuwa wamekaa awali.

Mchungaji akapanda juu ya madhabahu na kuwasalimu tena waumini wake kisha baada ya hapo, akaanza kueleza kuhusu habari ya Anna na jinsi Mungu alivyomtendea muujiza. Kila mmoja alisisimka sana kusikia habari hiyo, ikabidi mchungaji awasimamishe Anna, baba yake, mama yake na Jafet na kuwakaribisha madhabahuni kwani kila mmoja alikuwa na shauku kubwa ya kuwaona.

Waliposimama, waumini wote walinyamaza kimya kabisa, hakuna kelele zilizosikika zaidi ya hatua walizokuwa wanapiga kuelekea mbele kabisa. Walipofika madhabahuni, mchungaji alivunja ukimya na kuanza kuwatambulisha kisha baada ya hapo, alimpa kipaza sauti baba yake Anna na kumtaka awasalimu waumini wote kwa niaba ya familia yake.

Akaanza kwa kuwasabahi kisha baada ya hapo, akaelezea kwa kifupi historia ya maradhi yaliyokuwa yanamsumbua mwanaye jinsi yalivyoanza. Waumini wote walikuwa kimya kabisa, wakisikiliza kwa makini maelezo hayo.

Baada ya kumaliza kuelezea, baba yake Anna alimkaribisha binti yake naye aeleze ilivyokuwa. Maelezo aliyoyatoa ya jinsi alivyokuwa akiteseka na maradhi hayo, yaliwafanya waumini wengi washindwe kuzificha hisia zao, wakawa wanatokwa na machozi ya uchungu.

Kwa umri wake mdogo, kila mmoja aliona kama Anna hastahili kupitia mateso makali kiasi hicho. Aliendelea kueleza jinsi Jafet alivyojitolea figo yake ili kuokoa maisha yake na yote yaliyoendelea baada ya hapo.

Kadiri alivyokuwa anazidi kuelezea jinsi alivyoteseka mpaka muda huo, ndivyo watu walivyokuwa wanazidi kutokwa na machozi kutokana na simulizi hiyo iliyozigusa nyoyo za watu wengi.

Alipofikia sehemu ya kuhitimisha na kueleza jinsi ujio mpya wa Jafet katika maisha yake ulivyomsaidia kupona maradhi yaliyokuwa yakikaribia kuyakatisha maisha yake, kanisa zima lililipuka kwa shangwe, nderemo na vifijo. Ulikuwa ni ushuhuda ambao ama kwa hakika ulizigusa mno hisia za waumini wote.

Ili kuthibitisha alichokuwa anakisema, Anna alimuomba mama yake atoe vyeti vya hospitali vilivyokuwa vinaonesha maendeleo ya afya yake mpaka wakati huo, kila mmoja akawa haamini kwamba kweli kitu hicho kinawezekana.

“Huu ni ushuhuda kwamba hakuna kinachoshindikana kwa Mungu, binti huyu mdogo amewekwa kama ufunuo kwetu sisi wanadamu ili tuamini kwamba Mungu yupo na anatenda,” alisema Mchungaji Taraj, waumini wakashangilia tena na kuusifu utukufu wa Mungu.

Baadaye, mchungaji alihitimisha kipengele hicho cha ushuhuda kwa kuwashauri wazazi wa Anna na Anna mwenyewe kuhakikisha anaendelea kumuabudu na kumtukuza Mungu wake kutokana na miujiza mikubwa aliyomtendea. Ibada ilifikia mwisho na waumini wote wakatawanyika.

Nje ya kanisa, shughuli ilikuwa pevu kwa sababu watu wengi walikuwa wakitamani kuzungumza na Anna, kupeana naye mikono na kupiga naye picha kutokana na miujiza mikubwa aliyotendewa na Mungu wake. Waandishi wa habari nao hawakuwa nyuma, waliitumia fursa hiyo kumpiga picha Anna na kumuuliza maswali machache, mengine akawa anayajibu na mengine hakuwa akiyajibu.

Baadaye waliondoka na kurejea hospitalini kila mmoja akiwa amechoka, Anna akaachwa apumzike kidogo kwani japokuwa alikuwa na nafuu kubwa, bado mwili wake haukutakiwa kufanyishwa shughuli nyingi kama ilivyokuwa siku hiyo.

Jioni ya siku hiyo, taarifa za habari kwenye redio na runinga zilitawaliwa na habari ya Anna kupona maradhi sugu ya figo katika mazingira ambayo ilikuwa ni vigumu kuyaelezea. Tofauti na habari nyingine zilizorushwa siku kadhaa zilizopita, siku hiyo kulikuwa na sauti ya Anna mwenyewe akitoa ushuhuda kanisani akieleza jinsi alivyopona maradhi hayo yaliyokuwa yakikaribia kuukatisha uhai wake.

Kila aliyezisikia taarifa hizo, alisisimka mno kwa sababu halikuwa jambo la kawaida kwa mgonjwa kama yeye aliyefikia hatua mbaya kiasi kile kupona kirahisi, jina lake likazidi kuwa gumzo kila kona.

Kesho yake asubuhi, magazeti mengi ya nchi hiyo yalipambwa na picha za binti huyo mrembo iliyokuwa kurasa za mbele kabisa, yakiwa na vichwa vya habari vilivyoelezea jinsi alivyoweza kuyashinda maradhi ya figo kimiujiza.

“Jafet!”
“Naam!”
“Nakushukuru sana mpenzi wangu, haya yote yasingewezekana kama na wewe ungeamua kunilipa mabaya. Hata sijui namna ya kukushukuru,” alisema Anna na kumkumbatia Jafet kwa nguvu kifuani kwake.

“Usijali Anna, niliahidi kuwa na wewe katika shida na raha. Uzima wako ndiyo kitu chenye thamani kubwa kuliko vyote kwa sasa,” alisema Jafet, kauli iliyomfanya msichana huyo aendelee kumganda kama ruba huku machozi yakimtoka kwa wingi na kumlowanisha Jafet.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano ijayo kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

Leave A Reply