The House of Favourite Newspapers

Jerry Tegete aishtaki Yanga

0

tegete Jerry Tegete Mwadui FC.

Hans Mloli, Dar es Salaam
WAKATI Yanga ikiendelea na kampeni nzito za kutwaa ubingwa msimu huu, upande wa pili kumeibuka shutuma za kuburuzwa kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili ya kulipa mamilioni ya fedha wanayodaiwa.

Madai hayo ni kutoka kwa wachezaji wa zamani wa timu hiyo wakiongozwa na Jerry Tegete ambaye sasa anaichezea Mwadui FC ya Shinyanga.

Tegete ameungana na Hamis Thabit na Omega Seme ambao kwa pamoja wamewasilisha madai yao kwa Chama cha Wacheza Soka Tanzania (Sputanza) kutaka kumaliziwa fedha zao za usajili wakati wanajiunga na timu hiyo.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinaeleza kuwa uongozi wa klabu hiyo uliitwa na Kamati ya Nidhamu na Maadili ya TFF ukitakiwa kumalizana na wachezaji hao lakini Yanga walikuwa kimya, hata walipokumbushwa kwa barua hali ikawa hivyohivyo, ndipo sasa wameitwa kuhukumiwa rasmi kupitia kamati hiyo.

Katibu Mkuu wa Sputanza, Abeid Kasabalala, amesema: “Muda wowote tutakaa kwenye kikao cha kamati ya maadili kwa sababu tayari Yanga wameshapewa barua ya wito na kimsingi haitakuwa maelewano bali ni hukumu ya wapi zikatwe hizo fedha ili wapewe hao wachezaji.”

Alipotafutwa Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro, alisema: “Kama tumeandikiwa barua ya kufika huko, tutakwenda. Wanasema wanatudai lakini tunajua hatudaiwi kwa hiyo kila mtu ataweka ushahidi wake, tutajua inakuwaje.”

Leave A Reply