The House of Favourite Newspapers

Jiji Mauti -11

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Kwa mara ya kwanza nikamuona mama yangu akianza kulia, sikujua kilichomliza ila mara kwa mara alikuwa akimtaja bibi kwamba ilikuwa ni lazima amkomeshe. Sikujua alimaanisha nini na sikujua kwa nini alimsema sana bibi, tena kwa mabaya.
ENDELEA NAYO…

Mama hakutaka kuzungumza kitu kingine, alichokifanya ni kulala huku akiangua kilio kilichojaa kwikwi. Asubuhi ilipofika, hakutaka niende shule bali aliniambia nijiandae kwani kulikuwa na sehemu alitaka twende, hakukuwa na tatizo, nikajiandaa.

Baadaye akanichukua na kwenda sehemu moja hivi, sikumbuki ilikuwa eneo gani ila kulikuwa na kijipori kidogo, kimlima kidogo huku kwa mbali nikiona nyumba moja ya nyasi. Tukaanza kuisogelea nyumba ile, tulipoifikia, mama akapiga hodi, nikasikia sauti ya mzee f’lani ikitukaribisha.

Tulipoingia ndani ndipo nikagundua kwamba hapo kulikuwa kwa mganga wa kienyeji, aliponiona, alishtuka mno lakini hakutaka kuonesha hali yoyote ile, akatuambia tukae na kumsikiliza mama alikuwa akisema nini.
“Babu nimekuja, kuna tatizo,” alisema mama.
“Tatizo gani?”
“Huyu mtoto wangu, usiku alichukuliwa na wachawi,” alisema mama.
“Mmmh!” aliguna mganga.

“Kuna nini tena?”
“Ooppss…” alishusha pumzi nzito.
“Niambie kuna nini!”
“Mtoto wako amekabidhiwa uchawi, tena mkubwa wa wachawi kanda yote ya Pwani,” alisema mganga.
“Unasemaje?”

“Siwezi kufanya lolote, chochote akikitaka juu yangu, kitatokea, ninaogopa, naomba muondoke,” alisema mganga yule huku akionekana kuogopa.
“Ninahitaji msaada wako babu.”

“Naomba muondoke,” alisema mganga yule kwa sauti iliyojaa ukali, alionekana kuogopa.
Sikupenda kumuona mama yangu akikaripiwa au kulalamikiwa na yeyote yule kama alivyofanya mganga yule. Japokuwa sikumjua, nikamwangalia kwa macho makali yaliyobadilisha hali ya hewa mule ndani, ghafla, huku nikimwangalia, nikamuona mganga akianguka chini na kuanza kurusha miguu na mikono huku na kule, mapovu yakaanza kumtoka mdomoni.

Tukaogopa, kumuona mganga yule akigaragara chini huku mapovu yakimtoka, hakikuwa kitu cha kawaida hata kidogo. Tulichokifanya ni kuondoka mahali hapo, tena kwa mwendo wa harakaharaka.
Mama hakufahamu kama mimi ndiye niliyekuwa chanzo lakini wakati tukiwa njiani, alianza kuwa na wasiwasi mno juu yangu kwa kuona kwamba inawezekana nilimfanyia jambo lile mganga yule.
“Davina…” aliniita.
“Abeee.”

“Umefanya nini?”
“Nimefanya nini mama?” nilimuuliza, hata mimi sikuwa nikifahamu chochote.
“Umemfanya nini yule mganga?” aliniuliza.
“Sijui! Sikumfanya kitu.”

Huo ndiyo ukweli nilioufahamu, kipindi hicho, hasa muda huo wa kuwa mchawi kwa mara ya kwanza sikuwa nikifahamu kitu chochote kile, sikufahamu kama zile nguvu nilizokuwa nazo ndizo zilizomfanya mganga yule kuwa kwenye hali ile.

Naweza kusema kwamba sikujitambua. Tuliondoka na mama mpaka nyumbani, bado aliendelea kuwa na wasiwasi mno. Aliniambia wazi kwamba bibi alinikabidhi uchawi, alitaka niwe mchawi baada ya yeye kukataa.
Japokuwa nilikuwa na umri mdogo lakini nilifahamu kidogo masuala ya uchawi, hivyo nikaogopa sana. Mama alikuwa mtu wa kulia, alionesha dhahiri kwamba hakupendezwa na uchawi ambao nilikabidhiwa ila hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya.

Usiku ulipoingia, tulipomaliza kula na kulala, ghafla nikaanza kusikia sauti za watu waliokuwa wakicheka, sauti hizo zilitokea chumbani, niliangalia huku na kule, sikuona mtu lakini sauti zile ziliendelea kusikika.
Nikamuamsha mama lakini hakuamka, nikaanza kuwa na hofu kubwa. Nikasimama na kuifuata swichi ili niwashe taa, umeme haukukatika lakini cha ajabu, taa haikuwaka.

Sikujua nini kiliendelea. Wakati najiuliza, ghafla wakatokea watu watatu katika pembe moja ya chumba kile, walisimama imara huku wakiwa watupu kabisa, mara nikajiona kuwa na kitu mkononi, nilipojiangalia, nilikuwa na ule mkoba wa kichawi alionipa bibi.

Nikaanza kuwafuata wachwi wale ambapo baada ya kuwafikia, wakanishika mkono na hapohapo tukapotea, tulipoibukia, kulikuwa kwenye ule uwanja mkubwa uliokuwa na wachawi wengi waliokuwa uchi wa mnyama.
Bibi akanipokea kwa furaha na kuniambia kwamba siku hiyo ilikuwa ni siku ya kujifunza kuroga na kufanya mambo mengine.

Ndugu yangu, haya ninayokuandikia hapa yalinitokea, uchawi upo, uchawi unaua na katika miaka mingi ya kufanya uchawi, sikuona faida yake zaidi ya kupewa Jini Mauti ambalo liliyagharimu sana maisha yangu.

Leave A Reply