The House of Favourite Newspapers

Jini Mauti-13

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Ghafla nikajihisi kuwa na amani moyoni mwangu pasipo kujua kwamba kumbe wakati huo ndiyo niliingiziwa Jini Mauti pasipo kujijua, kwangu, niliona nipo vilevile tu.
ENDELEA NAYO…

“Thomas…”
“Naam!”
“Nikwambie kitu?”
“Kitu gani?”
“Kinachonisumbua moyoni.”
“Sawa! Niambie.”

“Ninakupenda! Ninakupenda mno.”
“Mimi?”
“Ndiyo! Naomba uwe wangu.”
“Davina! Upo timamu kweli?”

“Ndiyo! Kama nimechanganyikiwa, basi kwa mapenzi yako.”
“Mmmh! Ninyi wanawake mtaniua, mtu wa kumi wewe, yaani mapenzi…mapenzi, kila kona mapenzi.”

“Naomba uwe wangu.”
“Haiwezekani. Siwezi. Kwa heri.”
Sikutaka kuendelea kuteseka, niliamua kumwambia Thomas ukweli kwamba nilichanganyikiwa kwa mapenzi yake, sikutaka kubaki kimya, moyo wangu ulichanganyikiwa na sikuwa na jinsi zaidi ya kumwambia ukweli.

Kama kuogopa, ningeogopa hadi lini? Ningekaa kimya mpaka siku gani? Sikutakiwa kuwa hivyo, mimi kama msichana mwenye uhuru na maisha yake, niliamua kumwambia ukweli juu ya kile kilichokuwa kikiendelea moyoni mwangu.

Thomas hakunielewa, hakujua ni kwa jinsi gani niliumia moyoni mwangu kwa ajili yake, kwake, kila kitu kilichoendelea moyoni mwangu alikichukulia kawaida sana, kumbe wakati nilipomwambia kuhusu mapenzi, nilimaanisha.

Mbali na mimi, kulikuwa na rundo la wasichana waliokuwa wakimpenda Thomas, nilichukia lakini sikuwa na jinsi, na miongoni mwa wasichana waliokuwa wakimpenda sana Thomas alikuwa ni Agape.

Agape alimpenda sana Thomas, alikuwa radhi kumwambia kila mtu juu ya mapenzi aliyokuwa nayo juu ya mvulana huyo. Kiukweli nilikasirika sana, sikupenda kumuona mtu yeyote akimpenda Thomas zaidi yangu kwani nilijiona kustahili kuwa na mvulana huyo kuliko mtu yeyote.

Niliumia moyoni ila sikujiweka wazi, nikatokea kumchukia sana Agape, kila siku nilitamani kumfanyia jambo kama kumkomoa lakini kila nilipotaka kufanya hivyo, nilimuonea huruma kwa kuwa niliona hakuwa na kosa.

“Hakuna msichana anayefaa kuwa na Thomas zaidi yangu,” alisema Agape, msichana mzuri na hakika alijivunia uzuri wake.
“Hahaha!” walisikika wasichana wengine wakitoa vicheko.

Nilizidi kumchukia Agape, alikuwa msichana mzuri na niliona kwamba ni lazima angemchukua Thomas ambaye kila siku sikulala kwa ajili yake. Siku zikaendelea kukatika, kila nilipomuona Thomas, nilimfuata na kuanza kuzungumza naye lakini hali ilikuwa vilevile, hakutaka kuwa nami.

“Davina…” aliniita.
“Abeee…” niliitikia kiheshima.
“Unanipenda?”
“Ndiyo! Tena sana.”
“Umenipendea nini?”

“Thomas! Swali lako gumu, ila jua kwamba ninakupenda sana. Naomba uwe wangu,” nilimwambia bila kuogopa chochote.
“Nisikilize Davina…”
“Sawa!”

“Sikupendi, nashindwa kulielezea hili, yaani sikupendi tu, sina sababu,” aliniambia Thomas huku akiwa amenikazia macho.
Sikuamini kile nilichokisikia, nilimwangalia Thomas huku nikitaka kusikia zaidi kile alichoniambia, macho yake tu yalionesha ni jinsi gani alimaanisha.

Moyo ukanyong’onyea, ukaanza kudunda kwa nguvu huku kijasho chembamba kikianza kunitoka, nikaanza kutetemeka, nikashindwa kubaki hapo, nikaondoka.

Nilikwenda darasani na kuanza kulia huku nikiwa nimeegemea meza. Niliumia mno, sikutegemea kwamba mwanaume niliyempenda kwa mapenzi ya dhati, Thomas aliamua kuniambia ukweli kwamba hakuwa akinipenda.

“Kwa nini mimi? Kwa nini Thomas amenikataa? Haiwezekani, ni lazima nimroge, ni lazima awe wangu kwa lazima…” nilijisemea huku nikilia darasani, hakukuwa na mtu aliyegundua hilo kwani niliegemea meza.

Je, nini kitaendelea? Tukutane wiki ijayo.

Comments are closed.