The House of Favourite Newspapers

Jini Mauti-31

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA
Hiyo ilikuwa siku ya kwanza, wengine walikuja kuniuliza, majibu yangu yalikuwa mawili tu, sikumuona kwa kipindi chote na sikujua alikuwa wapi. Endelea…

Sikuwa na furaha hata kidogo, kichwa changu kilikuwa na mawazo tele juu ya John, nilichanganyikiwa mno, sikujua alikuwa wapi na kama kupotea alipotelea wapi. Kitendo kile alichokifanya, kile cha kupotea kilionesha dhahiri kwamba inawezekana alikuwa mchawi, lakini ilikuwaje siku ile tulipokwenda kwake hakukuwa na dalili zozote za kuonesha kwamba alikuwa mchawi? Je, kama hakuwa mchawi wala jini, alikuwa nani? Kila nilichojiuliza, sikupata jibu.

Mwezi wa kwanza ukapita, John hakuonekana, mwezi wa pili nao ukaingia, hakuonekana na mpaka tunamaliza kidato cha tano na kuingia cha sita, bado John hakuonekana. Katika kipindi chote hicho nilikuwa na mawazo tele, kutokuwepo kwa John kulinisikitisha mno, sikuamini kama hakuwa nami tena.

Baada ya kufunga shule kwa likizo ndefu, sikutaka kukaa Dar es Salaam, nikamwambia mama kwamba ninataka kwenda kumtembelea bibi mkoani Tanga, hakuwa na kipingamizi, akaniruhusu hivyo kwenda huko.
“Ila utapafahamu?” aliniuliza.

“Hakuna tatizo, nitafika tu, si umesema Lushoto? Wala usijali, nitafika tu,” nilimwambia mama.

Sikuwahi kufika kijijini kabla, sikuwahi kumuona bibi yangu katika hali ya kawaida zaidi ya ile hali ya kichawi ambayo kila siku ilitufanya kuonana. Niliondoka nyumbani siku iliyofuata na kuanza safari ya kuelekea Lushoto.
Ndani ya basi nilikuwa na uhakika wa kufika huko, nilikuwa na nguvu ya kichawi ambayo ilikuwa na kazi ya kuniongoza kila sehemu na ndiyo maana lisingekuwa jambo rahisi kupotea huko.

Ndani ya basi nililokuwemo nilikaa kitini na mvulana mmoja, kiukweli alikuwa mweupe mno, alikuwa na mchanganyiko wa rangi iliyoonesha mmoja wa wazazi wake alikuwa Mwarabu.

Kijana yule alikuwa mchangamfu mno, kila wakati aliyatawala mazungumzo, sikuwa muongeaji sana lakini kutokana na uchangamfu wake, naye akanifanya niwe muongeaji mkubwa.
“Lushoto kwa nani?”
“Bibi yangu!”
“Waoo! Kumbe tupo safari moja.”
“Na wewe unakwenda Lushoto?”
“Ndiyo!”
“Ni kwa nani?”
“Babu yangu!”
“Sawa! Nashukuru kuwa nawe safari moja.”
“Usijali! Inawezekana tukawa ndugu bila kujua,” aliniambia na wote kuanza kucheka.
“Inawezekana.”
“Yeah! Hivi unaitwa nani?”
“Davina. Na wewe?”
“Naitwa Karim.”
Safari ikaendelea huku tukiendelea kupiga stori za hapa na pale. Tulipofika Mombo, tukateremka kisha kuchukua mabasi madogo yaliyokuwa yakienda Lushoto. Tukaanza safari nyingine tukiwa pamoja, cha kushangaza, mpaka nilipokuwa nikiteremka, naye alikuwa akiteremka hapohapo.

“Eeh! Kumbe bado tupo pamoja!”
“Ndiyo maana nilikwambia isije kuwa babu yako ndiye babu yangu!” aliniambia Karim huku akitabasamu.
Alipokuwa akielekea Karim ilikuwa jirani na alipokuwa akiishi bibi. Nyumba ya bibi ilikuwa hapa na nyumba ya babu yake ni kama ya tatu kutoka tulipokuwa tukiishi. Bibi alifurahi kuniona, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kunipongeza kwa kazi kubwa niliyokuwa nikiifanya ambayo wachawi wengine waliona kuwa juu sana.

Kwa kawaida inapofika usiku, hasa kwa sehemu kama Lushoto ambapo kunakuwa na baridi kali, huwa watu wanatoka nje usiku na kuwasha kuni kisha kuanza kuota moto. Siku hiyo na mimi nilikuwa miongoni mwa watu waliokuwa nje kwa ajili ya kuota moto.

Tulikusanyika watu wote kutoka katika nyumba ya bibi, tulikuwa kama kumi na moja kisha kuwasha moto. Bibi alikuwa na kazi kubwa ya kutuhadithia mambo ya zamani huku wakati mwingine akituhusia kumcha Mungu kana kwamba yeye alifanya alichotuambia.

Wakati tukiendelea kuota moto, kwa mbali nikamuona Karim akiwa amesimama, sikutaka kukaa hapo, nilichokifanya ni kusimama na kuanza kumfuata. Aliponiona, aliachia tabasamu pana. Akanivuta pembeni.
“Vipi?” nilimuuliza.
“Poa! Nataka twende sehemu tukazungumze kidogo.”
“Wapi?”
“Hapo mbele.”
“Usiku wote huu!”
“Kwani unaogopa nini? Upo na mimi komandoo,” aliniambia Karim huku akionekana kujiamini.
Sikuhofia kitu chochote, aliponiambia kwamba twende pembeni kidogo, nikakubaliana naye. Tukaelekea huko, kulikuwa na giza totoro.

Nilijua kile ambacho kingekwenda kutokea, nilijua fika kwamba Karim alitaka kufanya mapenzi na mimi, sikutaka kukataa, mimi mwenyewe nilishampenda hivyo kusingekuwa na tatizo lolote.
Sura yake nzuri, uchotara wake ulinichanganya mno, sikuona kama kungekuwa na sababu ya kumkatalia mwanaume kama Karim, tena alikuwa amekuja yeye mwenyewe.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane wiki ijayo.

Leave A Reply