The House of Favourite Newspapers

Vyakula tiba kwa wagonjwa wa vidonda vya tumbo

1

WIKI iliyopita tulichambua kwa kirefu makundi ya vidonda vya tumbo.
Leo tutaangazia vyakula tiba kwa wagonjwa wa vidonda vya tumbo.

Katika makala ya leo, tutaangalia aina ya vyakula anavyopaswa kula au kuviepuka mgonjwa  wa vidonda vya tumbo (Ulcers)ili kupata nafuu na kuishi bila kusumbuliwa nao. Ili kupunguza makali au kujiepusha kabisa na ugonjwa huo unapaswa kujiepusha kula vyakula vyenye mafuta na sukari nyingi.

Epuka ulaji wa vyakula vilivyopikwa na kuungwa viungo vingi vya aina mbalimbali, kama vile pilipili kali za aina zote na viungo vingine vyenye ladha ya ukali ambavyo hutiwa ndani ya mboga ama chakula ili kuongeza ladha.

Pombe na kahawa au vinywaji vingine vyenye caffeine, vinaweza kuleta matatizo kwa mtu mwenye vidonda vya tumbo na kwa mtu asiye navyo anaweza kupatwa na tatizo, hivyo ni vyema kuepuka au kutumia kwa kiasi kidogo vinywaji hivyo kwani huongeza asidi tumboni na hivyo vinaweza kusababisha vidonda au kuzidisha maumivu kwa anayeumwa.

Kuna uhusiano kati ya ulaji chumvi na vidonda vya tumbo. Mgonjwa anashauriwa kuepuka ulaji wa vyakula vyenye chumvi nyingi, hususan vyakula vya kusindika ambavyo huwekwa chumvi nyingi ili visiharibike haraka. Pia jiepushe na kuongeza chumvi kwenye sahani wakati wa kula.

Wagonjwa wa vidonda vya tumbo wanashauriwa kula mafuta yatokanayo na samaki (Omega-3 fats) ambayo yameonekana kutoa ahueni kwa wagonjwa. Na kwa mtu ambaye si mgonjwa atakuwa anajiwekea kinga dhidi ya vidonda vya tumbo na magonjwa mengine ya tumbo.

Ulaji wa vyakula vyenye madini na vitamini kwa wingi husaidia pia kuleta ahueni kwa mgonjwa wa vidonda vya tumbo na kutoa kinga kwa wale ambao hawajaathirika.

Wenye vidonda vya tumbo wanashauriwa kupenda kula matunda na mboga za majani kama vile karoti, juisi ya kabeji, ndizi mbivu na matunda mengine yenye vitamin C, halikadhalika maziwa ya mbuzi, jibini na cream za maziwa kwani huleta ahueni kwa wagonjwa.

Sigara ni mbaya kwani huongeza hatari ya mtu kupatwa na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na wasiwasi. Kuepukana na maradhi hayo, watu wazingatie ulaji sahihi na kuishi maisha ya furaha.

1 Comment
  1. catherine simon says

    Your Comments ahsanten xana kwa maelezo mazuri ya vyakula juu ya ulcers. Nina swali maziwa fresh ya ng’ombe je yanafaa ili kutuliza maumivu ?

Leave A Reply