The House of Favourite Newspapers

Jini mweusi -59

0

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.

Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.

Nyuma ya kila kitu, kuna mwanaume mmoja mwenye sura mbaya, tena akiwa ni Kamanda Mkuu wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, (DCP) Dickson ndiye ambaye anafanya mauaji hayo pasipo kugundulika.

Kazi yake ni kununua machangudoa na yeyote atakayemgundua, humuua kikatili na kuondoka zake.

Polisi wanachanganyikiwa, wanamtafuta muuaji, wanamkosa kwani anaonekana makini hasa kwenye kufuta alama za vidole vyake.
Hali ya hofu inaendelea kutanda jijini Dar es Salaam.

Je, nini kitafuatia?

SONGA NAYO…

Kule chooni alikoingia, Happy alifungua kipochi chake na kutoa bastola ndogo tayari kwa kumuweka chini ya ulinzi Kamanda Dickson pasipo kujua kwamba mtu huyo alikuwa hatari zaidi yake.

Hakutaka kuchelewa kule, akatoka huku akijiamini kwani alikuwa na uhakika kwamba mwanaume huyo hakuwa akijua yeye alikuwa nani na chooni alikwenda kufanya nini. Akaufungua mlango kwa ajili ya kuingia chumbani, kitu kilichomshtua, ngumi moja nzito ikatua usoni mwake, akabaki akipepesuka, hapohapo akaanguka chini.

Kamanda Dickson hakutaka kuchelewa, tena alipoiona bastola ile akagundua kwamba mtu huyo alikuwa hatari na kama angemuacha basi ilikuwa lazima afe, hivyo kitu cha haraka kilichomjia kichwani, iwe isiwe ilikuwa ni lazima kumuua.

Akamsogelea pale chini kwa lengo la kukamilisha alichokitaka, kwa ustadi mkubwa kama mtu aliyepitia mafunzo ya karate, Happy akainyanyua miguu yake na kuikamata shingo ya Kamanda Dickson na kumwangusha chini.

“Kamanda…” alijikuta akiita Happy huku akionekana kuwa na mshtuko, hakuamini kile alichokiona, mkuu wake wa kazi ndiye aliyekuwa naye chumbani, tena akipambana naye kwa ajili ya kuuokoa uhai wake.

“Koh koh koh…” Kamanda Dickson alijikuta akikohoa huku akijitahidi kuiondoa miguu ya Happy ambayo iliikaba shingo yake vilivyo.

Dickson hakutaka kukubali, hakuwa tayari kuona akikamatwa kirahisi namna hiyo hivyo alichokifanya ni kujinyanyua pale chini alipokuwa, akamnyanyua Happy huku miguu ya msichana yule ikiendelea kuing’ang’ania shingo yake.

Alimbeba juujuu na kumbamiza chini kwa kuanguka naye. Sauti kubwa ya maumivu ikasikika kutoka kwa msichana huyo, hata kabla hajajua nini cha kufanya, Dickson akajisogeza pembeni, akaishika shingo yake iliyokuwa na maumivu na kuanza kukohoa mfululizo.

“Who the hell are you?” (Wewe ni nani?) aliuliza Dickson huku akimwangalia mwanamke huyo kwa macho ya mshangao, hakuamini kama kungekuwa na changudoa aliyekuwa na mbinu za kujihami namna ile.

“I don’t know, I am here to kill you,” (Sijui, nipo hapa kwa ajili ya kukuua)
Wote walisimama na kuanza kuangaliana, Happy alimwangalia kamanda wake ni kweli alimfahamu vilivyo, wakati mwingine alipokea amri kutoka kwa mkuu wake huyo na kuambiwa nini cha kufanya lakini kwa hali ilivyokuwa chumbani humo, hakukuwa na muda wa kupeana heshima tena, ulikuwa ni wakati wa hatari, wakati wa kuiokoa nafsi yake.

“Kama unataka kuniua, niue kama utaweza! Ukishindwa, nakuua wewe,” alisema Dickson huku akikunja ngumi. Hakukuwa na kingine kilichofuata zaidi ya kupigana. Kila mmoja alipitia mafunzo makali lakini kwa Dickson alionekana kuwa hodari katika kurusha ngumi mfululizo, mateke na hata ukwepaji wake ulionesha kabisa kwamba alikuwa mzuri katika kupambana tofauti na Happy.

Dakika kumi na tano zilikatika huku wakiendelea kuoneshana kazi, tena kimyakimya pasipo kuwasumbua wateja wengine waliokuwa kwenye vyumba vingine. Happy akaishiwa nguvu, akashtukia akipigwa ngumi mfululizo zilizomchanganya na kujikuta akiangukia kitandani huku uso wake ukiwa umevimba vilivyo na damu zikimtoka. Akabaki akipiga kelele tu. Akawahiwa kwa kuzibwa mdomo.

“Nyamazaaa…” alisema Kamanda Dickson kwa ukali huku akimziba mdomo.
Wakati akiwa amemtuliza pale kitandani, mara akasikia mlango ukigongwa, akajua fika kwamba mgongaji alikuwa mhudumu wa gesti ile hivyo akaufuata mlango na kuufungua, hata kuvaa kofia yake alisahau kuivaa.
“Nikusaidie nini?”

“Nimesikia kelele kaka…”
“Ndiyo! Ni kelele za mahaba… na wewe unataka?”
“Hapana! Samahani, nilifikiri mnahitaji msaada,” alisema msichana yule huku akitetemeka.

Dickson hakutaka kuzungumza sana, akaufunga mlango na kumfuata Happy kitandani pale, kilichofuatia ni kuendelea kumpiga ngumi za uso mfululizo na mwisho kabisa akainyonga shingo yake kwa kumkaba.

“Kwisha kazi…” alijisemea Dickson huku akikaa pembeni.
Alikaa kwa dakika kama kumi hivi ndipo alipokumbuka jambo moja la muhimu sana. Wakati ameufungua mlango na kuzungumza na dada wa mapokezi, hakuwa na kofia ya kuuficha uso wake na ndiyo maana dada yule alikuwa akizungumza naye huku akitetemeka, hasa baada ya kugundua alikuwa akizungumza na nani.

“Kanigundua…kanigundua…ni lazima nimuue,” alisema Dickson huku akionekana kuchanganyikiwa.

Harakaharaka akainuka kutoka pale kitandani, akaufuata mlango na kutoka. Breki ya kwanza ilikuwa mapokezi, alipofika hapo, dada huyo hakuwepo, alichanganyikiwa zaidi, akaanza kuita kwa kuhisi labda msichana huyo alikuwa sehemu, hakuisikia sauti iliyoitikia.

Huku akiangalia huku na kule, ghafla akasikia sauti za watu nje wakija, maneno aliyoyasikia ni koplo, kamanda na mkuu, mbali na maneno hayo, akasikia sauti ya msichana, akajua kwamba dada huyo wa mapokezi alikwenda kuwaita polisi, alichokifanya, akaufunga mlango wa kuingilia ndani ya gesti ile, polisi wale wakaanza kugonga kwa nguvu.

“Fungua mlango… fungua mlango kabla hatujauvunja,” alimsikia polisi mmoja ambaye alizungumza huku akiikoki bunduki yake, Dickson akabaki akiwa amesimama, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya, alichanganyikiwa, hakujua kama alitakiwa kuufungua mlango au la.

Kilichomchanganya zaidi, aligundulika kama alikuwa yeye, maiti ya kule ndani ilimtia hofu kubwa, hakujua afanye nini, kwanza akasimama na kuanza kujifikiria, polisi waliendelea kugonga mlango wakitaka wafunguliwe.

“Siwezi kukamatwa kijinga…” alijisemea Dickson, kweli, kwa jinsi hali ilivyokuwa, lingekuwa jambo gumu kwa mtu kama yeye kukamatwa kizembe namna ile. Ghafla, polisi wale wakaanza kupiga teke mlango kwa lengo la kuuvunja huku yeye akiwa amesimama, tena amepigwa butwaa.
Je, nini kitafuatia? Usikose riwaya hii ya kusisimua Alhamisi ijayo kwenye gazeti hilihili.

Leave A Reply