The House of Favourite Newspapers

Kilichonitokea Baada ya Kubakwa na Kaka Yangu-26

0

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale mama yake mdogo wa Dorcas alipomfahamisha kwamba siku iliyofuata angeondoka pale kijijini na kurudi mjini kauli iliyomhuzunisha sana msichana huyo aliyejiuliza angeishije katika mazingira yale mageni ya kijijini! Je, kilifuatia nini? Songa mbele na kisa hiki cha kuhuzunisha…

Nikiwa nawaza hivyo, bibi alirudi akiwa na karanga zilizokaangwa akanikaribisha ndipo mama mdogo akamuomba bibi wakaongee jambo f’lani, wakatoka nje.

Walipotoka nilijua mama mdogo alitaka kumweleza bibi masaibu yangu na lengo la mimi kwenda kule kijijini, baada ya dakika kama arobaini waliingia.

Bibi alinipa pole kwa yote yaliyotokea na kuniambia nisiwe na kinyongo na Evance kwani alifanya hivyo kwa sababu ya ujana na kwamba niwe na amani moyoni.

Kauli ya bibi iliniumiza sana kwani nilijua alisema vile kwa sababu aliyenibaka alikuwa mjukuu wake ambapo nilijiuliza kama angefanyiwa binti yao Emmy wangethubutu kusema aliyemfanyia hivyo alifanya kwa bahati mbaya.

Kutokana na uchungu nilioupata, kwanza wa kushindwa kuendelea kusoma, kubakwa na kupewa mimba nilijikuta nikitiririkwa na machozi.

Bibi aliyegundua niliumizwa sana na jambo hilo alianza kunibembeleza ninyamaze na nivumilie na kwamba atanipa uangalizi mzuri mpaka nitakapojifungua kisha nirudi shuleni.

Kwa kuwa sikuwa na la kufanya, nililazimika kuwa mpole na kuendelea kumkumbuka marehemu mama na kujisemea kama angekuwa hai yote yaliyonitokea yasingetokea.
“Dorcas, nakuomba usiwaze sana jambo lililotokea, kwa kuwa upo na bibi naamini hautapungiwa na kitu na msamehe Evance hayo ni mambo ya vijana, naamini ipo siku atakusaidia kwani hata yeye anajutia kosa lake,” Dorcas anasema mama mdogo alimwambia.

Tukiwa tunaongea huku nikiwa sina furaha zaidi ya kusumbuliwa na msongo wa mawazo, alikuja mama mmoja ambaye nilitambulishwa kwamba alikuwa na undugu na mama.

Tuliposalimiana, bibi alimtambulisha kwamba nimetokea mjini nitakuwepo pale kijijini kwa muda mrefu, yule mama akamwuliza nitakuwa nasoma kule?

Kufuatia kuulizwa hivyo, bibi alimwambia hapana nilikwishahitimu darasa la saba hivyo nitakuwepo kule kijijini kwa muda mrefu bila kumwambia kama nilikuwa mjamzito.

Kwa kuwa tangu tulipofika tulikuwa tunapiga stori, yule mama alinikaribisha kule kijijini kisha akaaga na kwenda kwake ndipo bibi alimwambia mama mdogo aandae mboga ya majani, usiku tulipokula ugali nikaoneshwa sehemu ya kulala.

Kutokana na mazingira yale kuwa mapya na jinsi nyumba ilivyokuwa, sikuweza kupata usingizi mapema, lakini baadaye nilipitiwa na usingizi.

Kulipokucha mama mdogo aliondoka nikaanza rasmi kuishi na bibi ambaye awali tulikuwa tukienda naye shambani lakini kadiri siku zilivyosonga mbele nikashindwa na kuwa mtu wa kushinda nyumbani.

Jambo la kumshukuru Mungu ni kwamba ujauzito wangu haukuniletea matatizo ya kuumwa kama inavyowatokea wanawake wengine, isipokuwa nilikuwa sipendi kula.
Kilichonishangaza zaidi ni kitendo cha mama aliyeahidi kunisaidia kwa kila jambo kukata mawasiliano nami, wala hakuja kunijulia hali na nilipomuuliza bibi aliniambia kwamba huenda alibanwa na biashara zake.

Hata mama mdogo aliyeniacha kule kijijini naye alikata mawasiliano kabisa, kwa ujumla kitendo cha mama kutokuja kuniona kilinihuzunisha sana.

Mbaya zaidi sikuwa na fedha za akiba ambazo ningezitumia kama nauli ya kwenda mjini, kufuatia hali hiyo nikawa sina namna ya kufanya.

Maisha ya kule kijijini yaliniweka katika wakati mgumu sana kwani nilimkumbuka marehemu mama na mama mkubwa wa Mbeya ambao walinilea kwa upendo.

Nilikuwa najiuliza kwa nini mimi pekee nilikuwa naandamwa na mikosi, wa kwanza kutomfahamu baba yangu, kusumbuliwa na wachawi nilipokuwa Mbeya, kifo cha mama, kubakwa na kupewa ujauzito, kukatishwa masomo kisha kwenda kutelekezwa kijijini!
Mambo hayo yaliniumiza sana, kuna wakati bibi akiwa hayupo nyumbani nilijikuta nalia peke yangu na kuiona dunia haikuwa rafiki yangu hata kidogo.

Wakati nikiwa kule kijijini nilikuwa nakwenda katika zahanati moja ambapo zilitolewa huduma za kliniki, kila nilipopimwa niliambiwa mtoto alikuwa akiendelea vizuri na kupewa maelekezo mengine yaliyohusiana na masuala ya uzazi.
Je, kilifuatia nini? Usikose wiki ijayo. Maoni, nicheki kupitia namba hiyo hapo juu.

Leave A Reply