The House of Favourite Newspapers

Jini mweusi -62

0

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.

Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.

Nyuma ya kila kitu, kuna mwanaume mmoja mwenye sura mbaya, tena akiwa ni Kamanda Mkuu wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, (DCP) Dickson ndiye ambaye anafanya mauaji hayo pasipo kugundulika. Kazi yake ni kununua machangudoa na yeyote atakayemgundua, humuua kikatili na kuondoka zake. Polisi wanachanganyikiwa, wanamtafuta muuaji, wanamkosa kwani anaonekana kuwa makini hasa kwenye kufuta alama za vidole vyake.

Hali ya hofu inaendelea kutanda jijini Dar es Salaam.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Amani ikatoweka moyoni mwake, muda mwingi Pamela alionekana kuwa na majonzi mengi, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea kwamba marafiki zake, wafanyakazi wenzake wa uchangudoa walikuwa wakifa katika mazingira ya kutatanisha.

Moyo wake ulijawa hofu lakini hakutaka kujali sana, aliingia jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutafuta fedha tu na hakutaka kurudi tena Arusha pasipo kuwa na fedha. Alifanya kazi yake huku akiwa na hofu kubwa lakini hilo, alilipuuzia kwa kuamini kwamba kama siku yako ya kufa imefika, hata ufanye nini utakufa tu.

Siku hii alikuwa amejipumzisha chumbani kwake, ilikuwa majira ya saa kumi jioni. Alijisikia kuchoka, alihitaji muda mwingi wa kupumzika kabla ya usiku kuelekea katika shughuli zake kama kawaida.

Wakati akiwa hapo, akasikia simu yake ikiita, alipoangalia namba ya mpigaji, alikuwa Stella, changudoa mwenzake maeneo ya Kinondoni Makaburini. Hakujua alitaka nini, mara nyingi halikuwa jambo la kawaida kupigiwa simu muda huo kwani machangudoa wengi hupenda kulala kwa ajili ya kazi kubwa ya usiku. Alichokifanya, akaipokea.

“Shoga, unasikia kinachozungumziwa kwenye TV?” aliuliza Stella hata kabla ya salamu.

“Kituo gani?”

“Global TV.”

Haraka akachukua rimoti na kuwasha televisheni yake na kuweka kituo hicho alichoambiwa. Macho yake yakatua kwa mtu ambaye alimfahamu kabisa, alikuwa akizungumza kama Kamanda Mkuu wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Kamanda Dickson.

Kwanza hakuamini kile alichokiona, akaisogelea televisheni na kumwangalia yule mtu aliyekuwa akizungumza kwa kuhisi labda alimfananisha, alipomwangalia, alikuwa mwenyewe.

“Kumbe ni mkuu wa polisi!” alisema Pamela kwa mshtuko, hofu ikaanza kumuingia, kijasho chembamba kikaanza kumtoka.

“Halo Pamela unamsikia huyo polisi anavyoongea?” alisikika Stella akiuliza.

“Abee..” aliitikia Pamela huku akionekana kuwa kwenye lindi la mawazo.

“Umemsikia?”

“Ndiyo!” alipojibu hivyo tu, hapohapo akakata simu.

Pamela akakosa nguvu, hakuamini kile alichokiona kwenye televisheni. Akasimama na kuanza kuzungukazunguka ndani ya chumba chake huku akiongea peke yake kama chizi. Kichwa chake kilijaa mawazo mengi, alichojiuliza ni juu ya Kamanda Dickson ambaye bado alikuwa akizungumza kwenye televisheni.

Hapo ndipo akajaribu kuvuta kumbukumbu za nyuma, siku alipokutana na Kamanda Dickson kwa mara ya kwanza. Aliikumbuka siku hiyo, alikumbuka sana kwamba alimuita ndani ya gari kulipokuwa na mwanga hafifu na kisha kumchukua tena huku kichwani akiwa na kofia.

Hapo ndipo alipopata jibu juu ya kofia ile, hakuishia hapo, alikumbuka mpaka siku walipokwenda chumbani, alipotoka kuoga na kuuona uso wake kisha kuulizwa kama alishtuka na yeye kujibu hapana.

Pia alikumbuka siku ambayo yeye na machangudoa wengine walikamatwa na polisi kisha kutupwa sero, cha kushangaza kabisa ambacho kilimwachia maswali mengi, yeye aliachwa huru pasipo kujua sababu ya polisi kufanya hivyo.

Kila kitu kikaanza kutiririka kichwani mwake, akapata majibu ya kila swali lililokuja kichwani mwake. Mbali na kufikiria hivyo, pia akaanza kukumbuka maneno ya watu wengine ambao walimuona muuaji wa machangudoa wote kwamba alikuwa mwanaume fulani aliyekuwa na kofia ya Marlboro kichwani.

Hapo pia akapata jibu kwamba inawezekana yule muuaji aliyekuwa akiwaua machangudoa alikuwa mwanaume huyohuyo, swali muhimu lililokuja kwake ni sababu za mtu huyo kuwaua watu hao zilikuwa nini? Na kama kweli yeye ndiye alikuwa muuaji, kwa nini hakumuua siku ya kwanza alipoingia naye chumbani? Kila alichojiuliza, akakosa jibu kabisa.

“Lakini inawezekana yeye ndiye huyu muuaji?” alijiuliza.

“Mmh! Hapana! Mbona mimi hakuniua? Kwa nini? Ila inawezekana kweli akawa ndiye muuaji? Siwezi kukubali hilo, hebu ngoja kwanza nimpigie simu,” alisema Pamela kisha kuchukua simu yake.

Haikuwa kazi kubwa kuipata namba ya Kamanda Dickson, aliisevu kwa jina la ‘Buzi’, alipoiona, moja kwa moja akampigia simu kwa lengo la kuzungumza naye. Simu ikaanza kuita.

Macho yake yalikuwa yakimwangalia Kamanda Dickson kwenye televisheni, aliendelea kuipiga, bado haikupokelewa na mara baada ya dakika kadhaa, Kamanda Dickson alipomaliza kuzungumza, simu haikuwa ikipatikana.

*   *   *   *

Mara baada ya kufika kwenye nyumba ya wageni, moja kwa moja Dickson na Happy wakaingia ndani. Muda wote, Happy alikuwa kimya, moyo wake ukahisi kwamba inawezekana huyo mwanaume ndiye aliyekuwa muuaji kwani muda wote aliing’ang’ania kofia yake kuwa kichwani mwake, hakutaka kuivua.

“Usiwashe taa mpenzi…” alisema Kamanda Dickson.

“Kwa nini?”

“Napenda giza, giza ndiyo mzuka wenyewe…”

Happy akazidi kuwa na wasiwasi, mbali na kofia, pia tukio hilo likampa uhakika kwamba mwanaume huyo ndiye aliyekuwa muuaji kwani hakuona sababu ya mtu kusema kwamba hakutaka mwanga kwa kuwa alipenda giza, yaani ufanye mapenzi na mtu pasipo kumuona uso wake, lilikuwa jambo lisilowezekana.

“Ndiye yeye…” alisema Happy, akaomba ruhusa kwenda chooni kwanza, kitu kilichomshangaza Kamanda Dickson, msichana huyo alikwenda na kipochi chake huko chooni, kitu hicho kikampa maswali mengi.

“Mmh!” alijikuta akiguna, tayari machale yakamcheza, naye akajiweka sawa pasipo kujua msichana huyo alikuwa mtu hatari.

Je, nini kitafuatia? Usikose riwaya hii ya kusisimua Alhamisi ijayo kwenye gazeti hilihili.

Leave A Reply