The House of Favourite Newspapers

Mume Wangu Anaishi Mara ya Pili – 5

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Nilianza kusali sala zote ninazozijua mimi huku nikiendelea kuangalia nje kwa ujasiri wa hali ya juu.

“Hujambo mama Kisu?” nilisalimiwa na mtu kutoka kushoto kwangu kwenye siti niliyokaa. Nikashtuka sana.

ENDELEA MWENYEWE SASA…

Niligeuka kumwangalia, nikamwona mwanaume mmoja, sura yake si ngeni hata kidogo lakini sikukumbuka nilimwonea wapi!

“Sijambo, mzima wewe?” nilimjibu.

“Mimi mzima, sijui wewe?”

“Hata mimi pia sijambo. Unatoka wapi, unakwenda wapi?” nilimuuliza.

“Natoka kijijini kwa mama, narudi mjini. Pole kwa msiba,” aliniambia.

Aliposema ‘pole kwa msiba’ akili zikafunguka zaidi. Kwamba yule ni nani, alisikia wapi? Je, uhusiano wake na mimi au na marehemu mume wangu ukoje?

“Nimeshapoa. Za siku nyingi lakini?” nilimwambia huku nikimtazama kwa umakini ili nione kama nitamkumbuka. Lakini wapi!

“Za siku nyingi njema sana. Ndiyo unarudi kutoka msibani?”

“Ndiyo tunarudi bwana. Lakini samahani sana, nikumbushe kidogo. Tulionana wapi vile?” nilimuuliza nikimwangalia tena.

“He! Mama Kisu, umenisahau mara hii? Mimi naitwa Tiaki!”

“Tiaki! Samahani sana! Tiaki wa wapi?”

“Tiaki wa kampuni ya Mabati. Niliwahi kuja nyumbani kwako na marehemu mumeo. Hunikumbuki kabisa?”

“Mh! Kwa kweli sikukumbuki kabisa. Huenda nakukumbuka lakini akili nazo zimehama kwa ajili ya huu msiba. Si unajua tena!”

“Ni kweli. Pole sana lakini! Mimi nilipopata habari hizi nilishtuka sana lakini nilikuwa na safari ya kwenda Nairobi, nimerudi juzi ndiyo nikaja kijijini. Pole sana shemeji yangu.”

“Nashukuru sana shemeji,” nilimjibu kwa sauti yenye utulivu wa hali ya juu.

Safari iliendelea lakini ghafla nikakumbuka kitu. Kwamba, wakati nakaa kwenye siti yangu, hapakuwa na mtu mwingine pembeni na nilimkumbatia mtoto miguuni pangu. Pia basi hilo halijasimama popote. Je, Tiaki alipandia wapi?

Basi lilitembea, kila abiria alikuwa kimya ndani. Watoto tu ndiyo walisikika wakilia kwa kero ya joto.

Tulifika mahali, basi likatoa mlio wa pa! Pa! Pa! Pa! Yaani liliharibika, likasimama.

Wahusika walishuka kutengeneza, baadhi ya abiria nao walishuka ili kupata upepo wa nje au kujisaidia kwa mahitaji mbalimbali. Eneo hilo lilikuwa na msitu, hakukuwa na dalili ya kuwepo kwa nyumba ya wenyeji jirani. Abiria wengine hawakushuka, nikiwemo mimi. Lakini jirani yangu Tiaki, yeye alishuka. Nikiwa nimebaki mimi, mtoto wangu na ndugu zangu waliokuwa wamekaa kwenye siti nyingine, meseji ya wifi iliingia.

“Wifi simu yangu ilikuwa haina hela, imebidi niweke. Unajua kama Daniel amepanda kwenye basi hilohilo ulilopanda wewe?”

Nilishtuka sana. nikatulia kwanza, kisha nikageuka kuangalia kushoto, kulia, nikainuka na kuangalia siti za nyuma lakini sikumwoma Daniel. Kusema ukweli, ilibidi nimpigie simu wifi, akapokea haraka sana.

“Wifi umeona meseji?” aliniuliza.

“Nimeona wifi. Ni Daniel yupi wifi? Maana kuna yule uliyenionesha wewe na yule niliyekuonesha mimi.”

“Mimi huyo wako simjui wifi. Niliyekuonesha mimi.”

“Si alikuja mpaka tulipokuwa ndiyo basi likasimama?”

“Si akaondoka. Nikamwona kule kwenye kibanda cha mkaa amesimama wakati wewe unapanda basi. Lakini alikuwa amekasirika sana. Basi lilipoondoka na yeye nikamwona anakimbilia na kupanda. Sema simu yangu ikawa haina salio na sikuwa na pesa mpaka nimerudi nyumbani kuchukua pesa. Ina maana wewe ndani ya basi hujamwona wifi?”

“Sijamwona wifi, ila kama machale yananicheza wifi,” nilimwambia.

“Kivipi tena wifi?”

“Kuna mtu amekaa siti moja na mimi, kaniita jina la mama Kisu, akanipa pole na msiba, akasema aliwahi kuja nyumbani na marehemu. Lakini simjui. Anasema anaitwa Tiaki.”

“Sasa hapo machale yanayokucheza ni yapi wifi, kwani  ni Daniel?”

“Hawezi kuwa yeye amejigeuza?”

“Mh! Kaka Daniel usimjue wifi? Halafu atakupaje pole wakati mlishakaa mkaongea.”

“Kwani we wifi hujapata picha kwamba, kuna Daniel wawili?”

“Ha! Kivipi wifi?”

“Wewe muda ule ulinionesha Daniel wa kwenye mkokoteni, mimi nilikuwa namwona Daniel wa kwenye kibanda cha mkaa. Huoni kama ni wawili hao?”

Wifi alicheka akaniambia niachane na dhana ya ushirikina. Hakuna Daniel wawili.

“Na kama unasema hivyo kwa sababu ya Daniel kuja nyumbani usiku jana na yule aliyesema amekurithi. Yule ni mmoja tu ila alitaka kutuchezea akiamini sisi hatuna akili.”

Mara, Tiaki alitokea, nikamuaga wifi kwamba tuchati kwa meseji.

“Vipi mama Kisu, naona ulikuwa unaongea na wifi yako.”

Je, nini kiliendelea? Usikose kusoma wiki ijayo mkasa huu unaoitwa Mume Wangu Anaishi Mara ya Pili.

Leave A Reply