The House of Favourite Newspapers

Jini Mweusi – 70

5

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.

Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.

Aliyekuwa akiwaua wanawake hao ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Dickson. Aliwaua kwa siri lakini baada ya kipindi fulani kupita, akagundulika na hivyo kuanza kutafutwa.

Kwa sasa yupo Mlandizi, baada ya kuona msako umekuwa mkubwa barabarani anaamua kwenda Mwanza kwa miguu kupitia Mlandizi. Anapofika porini, anaamua kujipumzisha huku polisi wenye mbwa wakiendelea kusogea kule alipokuwa.Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Usingizi ulikuwa ukimnyemelea, alichokitaka kwa wakati huo ni kulala tu kwani muda ulikwenda sana na hakujisikia kuendelea na safari yake. Sauti za mbwa ziliendelea kusikika masikioni mwake, hakutaka kujali sana kwani bado akili yake ilimwambia kuwa mbwa waliokuwa wakija hawakuwa na madhara yoyote kwake kwani watakuwa ni mbwa wa wawinda kenge ambao mara kwa mara walikwenda porini na hata pembezoni mwa mito kuwinda wadudu hao.

Wakati akiwa amekwishajiachia huku akiuvuta usingizi, akahisi mwili wake ukianza kusisimka mno. Haikuwa kawaida yake hata kidogo, alihisi labda kulikuwa na tatizo, akayafumbua macho yake na kuangalia huku na kule kuona kama kulikuwa na hatari ya kiumbe chochote mbele yake, hakukuwa na kitu chochote.

Usingizi haukuja tena, alijitahidi kuuvuta lakini mwili wake haukukubali hata kidogo. Alipitia mafunzo, aliujua mwili wa binadamu ulivyo, hakutaka kubishana nao, alihisi kwamba kulikuwa na tatizo na kama asingefanya lolote liwezekanalo basi angeweza kukutwa na hatari.

Alichokifanya ni kusimama, akaanza kuyapeleka macho yake huku na kule. Kwa mbali, aliweza kusikia sauti kadhaa za watu wakija kule walipokuwa, maneno aliyoyasikia, hayakuwa ya kawaida, yalikuwa ni koplo, kamanda na mengine, japokuwa aliyasikia kwa mbali, alihisi kwamba hao walikuwa polisi.

Kutoka hapo aliposimama mpaka sehemu ambapo polisi wale walifika, ilikuwa ni kama hatua mia moja, na sauti zile alizisikia vizuri ingawa ilikuwa na umbali mkubwa kutokana na ukimya uliokuwepo usiku, hakukuwa na haja ya kusubiria mahali hapo, alichokifanya ni kukimbia zake.

Hakutaka kusimama sehemu yoyote ile, aliendelea kusonga mbele, milio ya mbwa wakibweka haikuacha kusikika masikioni mwake, iliendelea kusikika zaidi hivyo kuongeza kasi kuelekea mbele zaidi.

Kulikuwa na giza, hakuanguka, kulikuwa na miba lakini hakujichoma, wakati mwingine alipita mpaka sehemu zilizokuwa na upupu, cha kushangaza hakuweza hata kuwashwa.

“Ni lazima nijiokoe, siwezi kukamatwa kizembe hivi,” alijisemea.

Alikimbia hadi alipofika sehemu ambapo kulikuwa na uwazi mkubwa, haikumpa tabu kugundua kwamba sehemu ile ilikuwa shambani. Hakukuwa na mtu yeyote mahali hapo, alijaribu kuangalia vizuri, shamba hilo lilikuwa ni la mpunga.

Hakutaka kusubiri, hakutaka kujiuliza, alichokifanya ni kuingia shambani humo huku akiendelea kukimbia. Shamba hilo lilikuwa kubwa, aliharibu mpunga lakini hakutaka kusimama, alisonga mbele zaidi huku akihema kama mbwa.

“Yule kule, kamata huyo mwiziiiii….kamata mwizi huyooooo….” alisikia sauti nyuma yake, alipogeuka, akawaona watu watano wakiwa wanamkimbiza kwa kasi kubwa.

Akili yake ikamwambia kwamba watu hao walikuwa polisi, akazidi kukimbia, tayari alijiona kukamatwa kama tu asingefanya juhudi za kukimbia na kuwaacha. Ila pamoja na hayo yote, kilichomtatiza ni juu ya mbwa.

Katika kipindi alichokuwa kule chini ya mti, alisikia watu wakija huku wakiwa na mbwa, alijua kabisa kwamba watu hao walikuwa polisi kutokana na majina waliyokuwa wakiita. Sasa hawa waliokuwa wakimkimbiza, ambao alihisi kwamba walikuwa polisi, hawakuwa na mbwa, walikuwa wao kama wao.

“Simama, tutakupiga mishale,” alisema mwanaume mmoja, naye alikuwa kasi kama wenzake.

“Aisee Iddi! Mfyatulie mmoja kwanza, piga wa mgongoni,” alisikika jamaa mwingine akimwambia mwenzake.

Iddi, mwanaume aliyejulikana kuwa na shabaha akaanza kumrushia mishale. Dickson alijua kilichokuwa kinaendelea hivyo naye kitu alichokifanya ni kukimbia kwa staili ya zigizaga, yaani kushoto kulia, kulia kushoto, yote ikiwa ni harakati za kukwepa mishale ile.

Wakati akiwa amebakiza kama hatua ishirini kumaliza shamba lile na kutoka nje, akashtukia akipigwa na mshale katika mguu wake, maumivu aliyoyasikia yalikuwa makubwa mno, akadondoka chini lakini hakutaka kutulia, akasimama na kuendelea kuukimbia huku akichechemea, damu zilimtoka mguuni lakini hakujali.

“Simama….tunasema simama utatuletea kesi ya mauaji…” alisema mwanaume mmoja kwa sauti ya juu.

Dickson hakuwa radhi kusimama, alijua kitendo cha kufanya hivyo matokeo yake ni kifo. Alipambana, alizidi kusogea mbele zaidi huku akichechemea, alipolimaliza lile shamba tu, hakuweza kupiga hatua, akajikuta akianguka chini, watu hao wakamfikia.

“Wewe ni nani?” aliuliza mwanaume mmoja kwa sauti ya juu huku akiwa amemuelekezea mshale mwingine usoni.

“Nao..mba mn..isa..meh..e..” alisema Dickson huku akihema kwa nguvu.

“Wewe ni nani?”

“Mbona unamuuliza maswali mengi Iddi, kama vipi mtawanye ubongo wake tu! Halafu nashangaa siku hizi una huruma sana aisee…” alisema jamaa mwingine huku akimwangalia swahiba wake ambaye alimuelekezea mshale Dickson.

“Haina noma, ngoja tuue fastafasta halafu tukamtupe porini,” alisema Iddi kisha kujiandaa kuachia mshale usoni mwa Dickson.

*   *   *   *

Polisi waliendelea kusogea mbele, kadiri walivyozidi kusogea ndivyo ambavyo mbwa walivyozidi kubweka kuon  esha kwamba mtu waliyekuwa wakimtafuta hakuwa mbali kutoka hapo walipokuwa.

Baada ya sekunde kadhaa wakafika katika ule mti alipokuwa amepumzika Dickson, mbwa wakausogelea, wakanusanusa sehemu ile na kusonga mbele zaidi.

Polisi walikuwa na uhakika kwamba hatimaye wangeweza kumpata Dickson, hawakukata tamaa, walizidi kusonga mbele na baada ya dakika kadhaa, wakafika katika eneo moja kubwa, lilikuwa shamba, hakuna walichojiuliza, walichokifanya ni kuingia shambani na kusonga mbele, kama kawaida mbwa waliendelea kubweka.

Je, nini kitaendelea? Usikose wiki ijayo.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

 

5 Comments
  1. MONIE says

    dick umekwisha

  2. MONIE says

    dick umekwiii sha

  3. breckii says

    kwisha habari yako kamanda dickson

  4. Hussein kassimu says

    Dick umekwisha

  5. Hussein kassimu says

    Mbona hamjaweka sehemu ya 71?

Leave A Reply