The House of Favourite Newspapers

Jini Mweusi-74

0

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.

Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.
Aliyekuwa akiwaua wanawake hao ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Dickson. Aliwaua kwa siri lakini baada ya kipindi fulani kupita, akagundulika na hivyo kuanza kutafutwa.
Aliamua kukimbia kupitia Mlandizi, huko, akapitia misukosuko mingi na mwisho wa siku akajikuta kwenye kijiji kimoja ambapo baada ya wanakijiji kumuona, wakaanza kujificha. Huku akijiuliza nini kinaendelea, akatokea kijana aliyekuwa na picha yake mkononi, Dickson akashtuka.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Kazi iliyokuwa mbele yake ilikuwa kubwa lakini hakutaka kuliona hilo. Alikuwa amefanya kazi ya upelelezi katika nchi nyingi, tena kwa watu waliokuwa na mtandao mkubwa, wauza madawa ya kulevya lakini kote huko alifanikiwa kwa asilimia zote.
Hiyo kazi iliyokuwa mbele yake, Fredrick aliiona kuwa ndogo sana, haikuwa kubwa, kumkamata mtu kama Dickson ambaye hakuwa akilindwa, hakuwa na mtandao wowote ilionekana kuwa kazi nyepesi, kama kumsukuma mlevi kwenye mteremko wa mlima.
Mara baada ya kuiona picha ya Dickson, akaondoka. Hakutaka kufanya kazi ya kwenda sehemu nyingine yoyote ile zaidi ya Mlandizi ambapo huko, kitu cha kwanza kabisa akaonana na polisi waliokuwa wamemfuatilia Dickson na mbwa wao lakini hawakufanikiwa.
“Tulimfuatilia lakini tulimkosa,” alisema mkuu wa kituo.
“Mlihisi anakwenda wapi?” aliuliza Fredrick.

“Hatujui kwa kweli, ila ni pori kwa pori, nahisi kuna sehemu anakwenda,” alijibu huku akimwangalia Fredrick usoni, alionekana kutokuwa mtu wa masihara hata mara moja.
Alichokitaka ni kupelekwa katika njia ile aliyoingia Dickson, hilo halikuwa tatizo, akachukuliwa na kupelekwa huko kisha kuachwa, sasa kazi ikawa kwake, kufuatilia hatua kwa hatua mpaka kuhakikisha huyo Dickson anapatikana.
Alikuwa na silaha zake, bunduki ndogo aina ya 45 Automatic upande wa kushoto kiunoni lakini katika soksi zake alikuwa na bunduki nyingine ndogo aina ya Revolver tena zote hizo zikiwa zimejaa risasi.
Alijitahidi kwenda mbele, alitembea mchana na usiku, alipita sehemu zilizokuwa na miti mingi, mabonde lakini aliendelea kusonga mbele. Chakula chake kikubwa huko njiani kilikuwa ni matunda mbalimbali ya miti.
Usiku wa siku hiyo alipolala na kuamka asubuhi, akaendelea na safari yake mpaka alipofika sehemu iliyokuwa na uwazi mkubwa, kulikuwa na shamba kubwa la mpunga, shamba lilelile alilopita Dickson kipindi cha nyuma.
Kabla ya kuingia ndani ya shamba hilo, akasimama na kuliangalia kwa makini. Kwa mtu kama yeye, mpelelezi aliyepitia mafunzo, hakutakiwa kufanya mambo kiholela, kila kitu alichotakiwa kufanya ilikuwa ni lazima kusubiri kwa muda.
Ardhini kuulionekana kuwa na alama za miguu ya watu, hiyo ikampa uhakika kwamba kulikuwa na watu mahali hapo kwani hata zile alama za miguu hazikuonesha kama watu hao walipita muda mrefu uliopita.

Akaanza kutembea pembeni ya shamba lile huku akionekana kuwa na wasiwasi, hisia zake zilimwambia kabisa kwamba kulikuwa na watu waliokuwa wakimwangalia. Alikuwa na bastola hakutaka kuzitoa kwani aliamini kama kulikuwa na watu, wasingekuwa na bastola, silaha zao zingekuwa za jadi kitu ambacho kingemfanya kupambana nao vilivyo.
Wakati akiwa ametembea kama hatua hamsini, akahisi nyuma yake kulikuwa na mtu akimsogelea, alichokifanya ni kupiga hatua ndefu mbili mbele kisha akageuka na teke moja la ghafla, alichokisikia nyuma yake ni uyowe mkubwa.
“Unaniuaaaaaa….” alisema mwanaume mmoja, alikuwa chini, teke lile lililopigwa, lilimpiga vilivyo kichwani.
Ghafla, wanaume watatu wakatokea mahali hapo, walikuwa na mikuki, wakamnyooshea Fredrick ambaye hakuonesha wasiwasi wowote, alibaki akiwaangalia.
“Mikono juu!” alisema mwanaume mmoja.
“Na miguu je?” alijibu Fredrick kijeuri, tena huku akiwaangalia watu hao, hakuonekana kuwa na hofu hata kidogo.
“Tumesema nyosha mikono juu!”
“Hebu acheni upuuzi, nipo safarini, mnanichelewesha, mmemuona mwanaume mmoja mwenye sura mbaya akipita huku?” aliuliza Fredrick huku akiwaangalia wanaume hao.
“Mikono inauma, siwezi kufanya hivyo!”
“Nimesema nyosha mikono juu!”
*   *   *
“Kwa nini umekuja kijijini kwetu?” Kijana yule alirudia swali lake.
Dickson akabaki akimwangalia, kilichomtia hofu ni ile picha aliyokuwa ameishika kijana yule. Japokuwa ilikuwa ni kijijini alijua kwamba kijana huyo ndiye aliyepeleka picha na mwisho wa siku wanakijiji kuanza kumkimbia kwa kuwa walimuogopa.
“Unahitaji nini kutoka kwangu?” aliuliza Dickson huku akimwangalia kijana yule.
“Sihitaji chochote kile, ninataka uondoke kabla polisi hawajafika,” alisema kijana yule.
Dickson hakutaka kuzungumza kitu, alichokifanya ni kuendelea na safari yake. Alikuwa amechoka na alitegemea angepumzika kijijini hapo lakini hilo likashindikana, hivyo akaondoka zake.

Mguu ulikuwa ukimuuma lakini hakusimama, kidonda kilizidi kuongezeka, kilichimbika na kitu pekee alichokihitaji kilikuwa ni dawa tu, ila kijijini hapo, hakukuwa na msaada wowote ule, hivyo akaondoka.
Wanakijiji ambao walikuwa wamejificha walibaki wakimwangalia, hata kutoka huko walipokuwa hawakuthubutu kwani habari ambazo kijana yule alizileta kijijini pale, aliziongezea chumvi kwa kusema kwamba Dickson alikuwa na uwezo wa kulipua sehemu yoyote ile kwani kila alipotembea, alitembea na mabomu.
Njia nzima alikuwa na mawazo tele, hakutaka kurudi nyuma, japokuwa mbele yake kulikuwa na safari ndefu ya kuelekea Mwanza lakini ilikuwa ni lazima afike huko kwa kupita pori mpaka pori.
Baada ya mwendo kama wa kilometa mbili, akaanza kusikia sauti za watu kutoka porini. Kwanza kitu alichokijua ni wanakijiji tu ambao kazi yao ilikuwa ni kushinda mashambani mwao.
Hakutaka kuogopa, alijiamini sana, alichokifanya ni kusimama wima ili kuwaona hao watu ambao walikuwa porini kuja mahali pale aliposimama.

Ghafla, wanaume watatu walioshiba, waliokuwa na bunduki nzito mikononi mwao wakatokea mahali hapo, Dickson akashtuka, alipomwangalia mmoja wapo, huyu alikuwa Savimbi, mmoja wa wanaume walioshiba ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kuteka mabasi yaendayo mikoani.
Alipomuona, akashtuka, wote wakaangaliana, walifahamiana, vijana wengi wa Savimbi ambao walikuwa wakielekea benki jijini Dar es Salaam kuiba fedha waliuawa na mwanaume huyo alipokuwa polisi.
Alimfahamu, aliujua uwezo wake, wakabaki wakiangalia, umbali uliokuwepo kati yao, kama miguu ishirini hivi.
Alichokifanya Savimbi ni kuikoki bunduki yake na wale vijana wake, mtu aliyesimama mbele yake, alikuwa akimchukia mno, ilikuwa bora kumpenda shetani lakini si huyo Dickson, leo aliingia kwenye kumi na nane zake, ilikuwa ni lazima amuue.
Dickson akabaki akitetemeka.

Je, nini kitaendelea? Usikose wiki ijayo kwenye gazeti hilihili.

Leave A Reply