The House of Favourite Newspapers

Jini mweusi 75

0

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.
Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.
Aliyekuwa akiwaua wanawake hao ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Dickson. Aliwaua kwa siri lakini baada ya kipindi fulani kupita, akagundulika na hivyo kuanza kutafutwa.
Aliamua kukimbia kupitia Mlandizi, huko, akapitia misukosuko mingi na mwisho wa siku akajikuta kwenye kijiji kimoja ambapo baada ya wanakijiji kumuona, wakaanza kujificha. Huku akijiuliza nini kinaendelea, akatokea kijana aliyekuwa na picha yake mkononi, Dickson akashtuka.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Walibaki wakiangaliana, walifahamiana, Savimbi alikuwa mtu hatari, jambazi ambaye kila siku alikuwa akikiongoza kikosi cha porini kuteka mabasi na kuwafanyisha abiria vitendo vya kinyama.
Hata na yeye alipomwangalia Dickson, alimfahamu vilivyo, alikuwa miongoni mwa askari hatari sana, wenye mafunzo makubwa, aliwasumbua vijana wake kwa kipindi kirefu, leo hii alikutana naye porini.
Watu hao walikuwa na silaha mikono mwao na Dickson hakuwa na kitu chochote kile. Kila alipowaangalia, aliona kabisa kwamba kifo kipo mbele yake, hakutaka kujiuliza nini cha kufanya, hapohapo akaanza kukimbia.
Savimbi na vijana wake wakaanza kumkimbiza huku wakimrushia risasi. Mbali na kupambana, Dickson alikuwa mtu hatari katika kukwepa, hakukimbia moja kwa moja, alikimbia kwa staili ya zigzag tena katika miti iliyokuwemo mle porini.
Risasi zote alizokuwa akirushiwa alizikwepa vyema na kupiga kwenye miti. Mahali hapo kulikuwa na pori kubwa, alijitahidi kukimbia kwa tahadhali, japokuwa mguu wake mmoja ulikuwa na kidonda kikubwa lakini hakujali, hakutaka kusimama, aliendelea mbele huku akiruka kila kizuizi alichokutana nacho njiani.
Savimbi na vijana wake hawakutaka kukata tamaa, waliendelea kumkimbiza Dickson lakini mwanaume huyo alikuwa na kasi kubwa hivyo kuona wakiachwa taratibu na baada ya dakika chache, Dickson akawapotea.
“Yupo wapi?” aliuliza Savimbi huku akihema kama mbwa.

Walimtafuta sehemu hiyo lakini hawakumpata, hawakujua kama Dickson aliendelea kukimbia au alijificha sehemu fulani. Walichokifanya kama kumtisha ni kuanza kupiga risasi mfululizo kila upande ili kama amejificha atoke alipokuwa lakini bado kulikuwa na ukimya.
“Atakuwa ametuacha, ana bahati sana, ningemuua na kumla nyama, katusumbua sana huyu mtu, katukosesha sana madili,” alisema Savimbi kwa hasira.

Wakati wakiyazungumza hayo, Dickson alikuwa mbali kabisa, aliendelea kukimbia, mguu ulikuwa ukimuuma sana lakini hakutaka kusimama, bado aliendelea mbele huku akichechemea.
Hakukuwa na sauti za vitu vingine zilizokuwa zikisikika zaidi ya ndege tu. Aliendelea kwenda mbele huku akichechemea mpaka alipofika sehemu ambayo aliamini kwamba angeweza kupumzika kwani kadiri muda ulivyokuwa ukienda mbele na ndivyo alivyozidi kuchoka na mguu kuuma zaidi.

Akatulia sehemu iliyokuwa na miti mingi iliyotengeneza kama chumba fulani na kukaa hapo. Mguu ulikuwa kwenye maumivu makali, hakuwa na dawa wala kitu chochote kile, alichokifanya ni kuchukua majani kisha kuanza kufuta damu zilizoendelea kutoka katika kidonda.
Muda ulikuwa umekwenda sana, ilikuwa ni saa kumi jioni, mwili ulichoka na macho yake yalikuwa mazito mno. Hakutaka kubaki macho, ilikuwa ni lazima apumzike hata kabla ya kuendelea na safari yake. Akajikuta akipitiwa na usingizi mzito.

Mara baada ya saa mbili, Dickson akashtukia akiamshwa hapo alipolala, sauti iliyosikika ikimuamsha haikuwa ya amani hata kidogo, ilikuwa ni sauti iliyojaa amri, akayafumbua macho yake kuangalia ni nani aliyekuwa akimwamsha.
Kitu cha kwanza kabisa kukiona kilikuwa ni mdomo wa bunduki. Dickson akashtuka, akayaona maisha yake kuwa hatarini, hata kabla hajasema kitu chochote, mtu huyo akamkandamiza na mguu wake palepale chini.
“Tulia hivyohivyo, nimekutafuta sana mpumbavu wewe,” alisema mwanaume huyo huku akiwa na hasira, hapohapo akaanza kuikoki bunduki yake tayari kwa kumfyatulia risasi Dickson pale chini alipomkandamiza.
*     *     *
Kwa kumwangalia usoni tu, Fredrick hakuonekana kuwa mtu wa kawaida, alionekana kuwa mtu hatari aliyekuwa na mafunzo makubwa ya kupambana na watu wengi.
Japokuwa aliambiwa kwamba anyooshe mikono juu lakini hakutaka kufanya hivyo ndiyo kwanza alibaki akiwaangalia watu hao huku uso wake ukionesha kama mtu aliyekuwa akihitaji kitu fulani kutoka kwao.
“Nimewauliza swali, mnanikumbuka?” aliuliza Fredrick, alionekana kuwa mwanaume jeuri.

Wao ndiyo walikuwa na silaha mikononi mwao lakini hawakuonekana kujiamini, walihisi kwamba hata kama watamrushia mishale, mwanaume huyo angeikwepa na kuwafuata.
Wakajikuta wakizishusha silaha hizo chini na kumwangalia. Hapohapo Fredrick akaanza kupiga hatua kuwafuata watu hao, alipowafikia, akasimama karibu yao na kuanza kuzungumza nao.
“Ninamtafuta mtu mmoja hivi, inasemekana alipita hapa,” alisema Fredrick.

“Nani?”
“Mwanaume mmoja mwenye sura mbaya, mmemuona?” aliuliza.
Wanaume hao wakabaki kimya kwanza, walimuona mtu huyo, aliyekuwa akizungumziwa alikuwa Dickson, mwanaume mwenye sura mbaya ambaye naye aliwasulubu baada ya kutaka kumfunga kwenye mti.
Kama alivyokuwa huyo mwanaume aliyesimama mbele na ndivyo alivyokuwa Dickson, naye alionekana kuwa mtu wa mapambano ambaye hakutakiwa kufuatwa hovyo.
“Tulimuona ni mtu hatari sana,” alijibu mwanaume mmoja.
“Lini?”
“Siku mbili zilizopita. Tulikuwa watu kama wanne hivi, akatupiga wote, ila tulimjeruhi mguuni kwa mshale,” alisema mwanaume huyo.

“Alielekea wapi baada ya kuondoka?”
“Hatujui, alitupiga na kuzimia, hatukujua alielekea wapi,” alijibu mwanaume huyo.
Fredrick alikasirika, alitumia muda wake mwingi kutembea pori kwa pori mpaka kufika mahali hapo na mwisho wa siku kuambiwa kwamba mtu huyo alipita mahali hapo siku mbili zilizopita.
Walichokifanya wanakijiji hao ni kumchukua na kumpeleka nyumbani kwao na kumtaka kukaa huko japo kwa saa kadhaa kabla ya kuendelea na safari yake ya kumtafuta huyo mtu aliyekuwa akimtafuta.
Wanakijiji walikuwa na maswali mengi juu ya huyo mtu, alionekana kuwa mgeni mahali hapo lakini wakulima wale walizungumza naye kila wakati kama mtu ambaye walikuwa wakifahamiana naye kwa kipindi kirefu.
Ingawa wanakijiji hao walimuuliza sababu za kumtafuta huyo mtu zilikuwa zipi, Fredrick hakujibu, hakutaka mtu yeyote afahamu lolote lile kwa kuhisi kwamba inawezekana Dickson angepata taarifa kwamba nyuma kulikuwa na mtu aliyekuwa akimtafuta.

“Hatakuwa mbali kutoka hapa ni lazima niendelee kumtafuta,” alisema Fredrick, hakutaka kukaa kijijini hapo.
Siku hiyohiyo akaondoka kuendelea na safari yake, mbele yake kulikuwa na kazi kubwa sana ambayo ilikuwa lazima aikamilishe haraka iwezekanavyo.
Je, nini kitaendelea na je Fredrick atafanikiwa kumpata Dickson? Usikose wiki ijayo.

Leave A Reply