The House of Favourite Newspapers

Kilichonitokea Baada ya Kubakwa na Kaka Yangu-40

0

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale mama Bite alipoingia katika chumba walichokuwa wakilala mabinti zake na kumwuliza Dorcas kuhusu nguo alizopewa na Tabu na kumwambia alijua mpango wa kuondoka msichana huyo wa kazi akaanza kumshambulia kwa matusi na kumpiga kibao kilichomfanya aangukie kitandani. Je, kilifuatia nini? Songa mbele…

Alipoona nimeangukia kitandani, aliniinua huku akinitukana na kunipiga kibao kingine nikaanza kulia.
“Wewe kinyago leo utanitambua, unajifanya unashangaa Tabu kutoroka wakati unajua kila kitu, kwa nini hukuniambia mapema?” Dorcas anasema mama huyo alimjia juu.

Nikiwa naendelea kujitetea kwamba sikuelewa chochote alimtuma Bite aende akamchukulie fimbo, mwanaye alikwenda uani na kurudi na fimbo ya mti wa muarobaini.

Mama alinitoa mle chumbani na kunipeleka sebuleni akaanza kunitandika hadi alipokuja mama wa jirani aliyesikia wakati nikilia na kuuliza sababu za kunichapa.
Mama alimfahamisha,  yule mama alimsihi asiendelee kunichapa ndipo alisema ilikuwa bahati yangu nilipata mtetezi lakini siku ile ningemtambua.

Nakumbuka siku hiyo sikula chakula cha usiku, nikiwa chumbani kwangu nilikumbuka mengi nikalia sana na kumkumbuka marehemu mama yangu pamoja na mama mkubwa wa Mbeya.

Hata hivyo, sikuwa na la kufanya kwani kilichonifanya niwe nyumbani kwa mama Bite ni kusoma kama alivyoniahidi, nikaamua kuvumilia kwa sababu hapakuwa na mtu wa kunisaidia kupata elimu.
Usiku baba aliporejea alisimuliwa kila kitu kuhusu kutoweka kwa Tabu, baba alishauri kukicha mama akatoe taarifa polisi ili kama atapata tatizo wasije kuhusishwa.
Kulipokucha, kabla ya baba kwenda kazini aliniita sebuleni na kuniuliza rafiki yangu Tabu aliniaga anakwenda wapi, nikamwambia sikuelewa chochote.

Licha ya kuniuliza mara kadhaa nami kusisitiza sikufahamu chochote aliridhika niliongea ukweli, akamwambia mama  ambaye hakukubaliana naye.
Baada ya baba kuelekea kazini, nikaanza kufanya usafi wa nyumba nzima, nilipomaliza niliosha vyombo na kuinjika uji. Wakati huo akina Bite na kaka yao Barton walikuwa wanauchapa usingizi.
Kwa upande wa mama, mumewe alipoondoka alirudi chumbani kwake, sikuelewa kama alikuwa amelala au alikuwa akifanya kitu gani.

Kwa kuwa tangu nilipoamka sikuwa nimefungua kinywa, nilichukua mkate ambao baba alikujanao pamoja na blue band nikamimina chai kwenye kikombe nikaanza kunywa.
Nilifanya hivyo kwa sababu sikuwa mpenzi sana wa uji, nikiwa nimeketi sebuleni sehemu ya kulia chakula nakunywa chai, mama alitoka chumbani kwake.

Aliponiona alisimama na kujishika kiuno kisha kunikata jicho, kitendo cha  kufanya hivyo kilisababisha moyo wangu kupiga paa kwani nilielewa hakupenda ninywe chai!
“Hivi wewe kinyago nani kakuambia unywe chai tena kwa mkate wenye siagi, unajua huo mkate kaletewa nani?” Dorcas anasema mama Bite alimwuliza.

Aliponiuliza hivyo nilipata hofu nikashindwa kumjibu kwa sababu sikuona kama nilifanya kosa na sikuwa na nia ya kula mkate wote, alipoona nimekaa kimya aliniuliza;
“Wewe si ninakuuliza mbona umekaa kimya au ndiyo kiburi cha kwenu?”
Nikiwa bado nimepigwa na butwaa na kushindwa kumjibu, alinifuata akanishika mkono na kunivuta, niliteleza na kuanguka chini.

Licha ya kuanguka mama hakunionea huruma aliniinua na kunizaba kibao, kabla sijakaa sawa akaniongezea kingine nikaona nyota zikitembea usoni.
Kwa maumivu niliyopata nilianza kulia na kumuomba msamaha mama kama nilikosea anisamehe hakuridhika akaendelea kunipiga na kunishambulia kwa matusi.

Wakati akinipiga huku akinivuta, sketi yangu ilinivuka nikabaki na nguo ya ndani pekee, nikiwa katika hali hiyo Barton aliyesikia nikilia aliamka na kuja sebuleni na kushuhudia nguo yangu ya ndani ikionekana.Sikuelewa sababu ya Barton kuendelea kuniangalia badala ya kuondoka, nilijiuliza kama aliyekuwa akipigwa au kuwa katika hali ile angekuwa dada yake Bite au Monica angevumilia kuwaangalia.
Jambo la kushangaza, mama hakujali aliendelea kunishambulia mpaka Bite na Monica walipoamka na kuhoji sababu za kuadhibiwa namna ile.
“Huyu msichana ni jeuri sana, mimi namwuliza badala ya kunijibu ananikunjia sura, hivi hanijui eh?” mama aliwaambia mabinti zake.
Je, kitaendelea nini? Usikose mkasa huu wa kusisimua toleo lijalo.

Leave A Reply