The House of Favourite Newspapers

Jinsi Ya Kuanzisha Biashara Bila Mtaji Wa Pesa!

MAFANIKIO yamemaanishwa kwa kila mwenye juhudi kubwa. Jukumu lililo mbele yako ni kupambana kadiri uwezavyo ili uondokane na umaskini kisha kuukaribisha utajiri kwa kuchakarika. Elekeza nguvu na maarifa yako yote kwenye kutafuta mafanikio. Lazima siku moja uondoke huku dunia ikilitaja jina lako kwa heshima, maisha ni namna ulivyochagua kuishi. Hapa ninakuletea dondoo bora kabisa za kukuwezesha kuanzisha biashara bila kuwa na mtaji wa pesa na kupiga hatua kubwa katika biashara.

 

Ngoja nikuambie jambo muhimu, katika maisha kila kitu kiko kwenye utashi wa uamuzi wa mhusika. Maana yangu ni kwamba ukiamua kufanya jambo lolote na ukadhamiria kwa dhati na kuwekeza nguvu, akili na maarifa yote uliyonayo, kuna msemo wa kwamba mafanikio ni uamuzi wa mtu, lakini wengi hushindwa kuyafikia kwa sababu wanaamua, lakini wanakosa morali na mwendelezo wa uamuzi wao.

 

MAHITAJI MUHIMU ILI MTU AFANIKIWE

Yapo mahitaji muhimu matatu ili mtu afanikiwe. Mambo hayo ni wazo, pesa na watu. Bahati mbaya vyote vitatu ni nadra kuja kwa pamoja. Kwa ufafanuzi ni kwamba, mtu anaweza kuwa na wazo la biashara, lakini akawa hana pesa na watu. Au akawa na pesa, lakini akawa hana wazo la kuzifanyia pesa hizo na kuna mtu anaweza kuwa na watu wengi wa kuweza kumsaidia, lakini akakosa pesa na wazo. Maisha ni mtihani sana, ndiyo maana mara nyingi huwa ninasema inahitaji watu waliodhamiria na kujitoa kwa dhati tu kufanikiwa, vinginevyo utaishia kuwaza maisha mazuri, lakini kwenye uhalisia unaishi maisha ya maigizo.

 

 

SASA TUINGIE KWENYE MZIZI WA MADA

Kinachohitajika kwenye maisha ya biashara ni kuwa na wazo kwanza. Pesa na watu watafuata, lakini tayari umeshakuwa na wazo. Ngoja nifafanue. Unatakiwa uwaze ni kitu gani unaweza kukifanya kwa jamii. Kaa chini na uwaze kitu ambacho ukikifanya kitawavuta watu wengi kutaka huduma yako. Ukishakuwa na wazo hilo, mtafute mtu au watu wenye pesa, lakini hawana mawazo na uwashirikishe ili wakuwezeshe. Hakikisha ni watu ambao unawaamini au kabla hujawafuata, basi nenda kasajili wazo lako kwenye mamlaka husika na baada ya hapo zunguka na wazo lako kwa watu na taasisi mbalimbali zikiwemo benki ili upate pesa za kutekeleza wazo na mipango yako.

 

ANGALIZO KWENYE HILI

Nimesema uwe na wazo ambalo utaamini kwamba ukilifanya litakuingizia pesa na kukufanya kuwa mfanyabiashara mkubwa. Lakini
kitu cha kuzingatia hapa ni kwamba kwenye kutafuta wazo, hakikisha ni jambo ambalo litatoa mahitaji muhimu ya watu kwenye katika jamii inayokuzunguka. Watu wanapenda kupata suluhu ya haraka kwenye matatizo yao ndiyo maana mtu akibuni suluhu ya jambo fulani, huishia kuwa tajiri mkubwa kwa sababu watu watalazimika kutoa pesa ili wapate suluhu ya matatizo yao. Ndugu zangu, wazo ndiyo kila kitu kwenye ulimwengu wa biashara. Haihitaji kuwa na pesa mfukoni ndipo ufikirie kuanzisha biashara. Kwa kufanya hivyo utasubiri sana hadi ile picha ya Mnara wa Askari pale Posta Mpya, Dar igeukie upande wa Magharibi!

 

MFANO MWINGINE HAI

Kuna yule Babu wa Loliondo, Mchungaji Ambilikile Mwasapile, aliumiza kichwa
kwamba watu wengi wanasumbuliwa na magonjwa sugu ambayo tiba zake zimekuwa za kusuasua katika hospitali nyingi za kisasa. Akaja na wazo, ingawa alitoa ufafanuzi kuwa ‘alioteshwa’ na Mungu na kutangaza dawa ya kunywa kwenye kikombe na bei yake ikawa ni shilingi 500/= tu, sikilizia watu walivyomiminika Loliondo! Leo yule babu ambaye alikuwa akishia maisha ya kawaida, anafurahia wazo lake kwenye ukwasi ambao haupimiki! Maisha yameendelea kuwa matamu kwa sababu ya kuumiza kwake kichwa.

 

CHUKUA NA HII

Joseph Alex Kusaga, alibaini kuna upungufu fulani kwenye redio zilizokuwepo kwa wakati ule. Kwamba vijana walikuwa wanaachwa nyuma kwenye eneo la burudani ndipo akasugua kichwa na kuja na wazo la kuanzisha redio ambayo itajikita kwenye masuala ya burudani mwanzo
mwisho. Akaanza na redio ambayo aliita Mawingu FM kabla ya kuwa Clouds FM, leo hii Kusaga ni miongoni mwa vijana wenye mafanikio makubwa, kwa sababu aliwaza na kuibuka na suluhu la vijana kukosa burudani!

 

TUENDELEE NA MIFANO

Kuna simulizi inatajwa kuwa siku moja mzee wetu mwenye maarifa, hekima na busara tele, Dk Reginald Mengi alikuwa akisafiri na kushikwa na kiu kali kabla hajafika alikokuwa akienda. Alipata shida mno kwani hakukuwa na maji yaliyokuwa yakiuzwa mitaani. Ni hapo ndipo alikuja na wazo la kutengeneza maji yenye ubora mkubwa na kuyaweka kwenye chupa nzuri kisha kuyauza kwa bei ya kawaida. Ni hapo ndipo maji ya Kilimanjaro yakaanzishwa, huku chanzo chake kikiwa ni
kwenye yale maporomoko ya Mlima Kilimanjaro, eneo moja maarufu kwa jina la Shirimatunda. Leo hii kuna asiyejua ubora, thamani na heshima ya maji ya Kilimanjaro? Ukisimama na kutaja orodha ya watu waliofanikiwa katika biashara nchini Tanzania na ukaacha kumtaja Dk Mengi, itatulazimu tukupeleke kwa daktari bingwa wa magonjwa ya akili.

 

SASA TUELEWANE

Mtaji mkubwa wa biashara unayoitaka uko hapo nyuma yako. Ndiyo, unashtuka nini? Ni hapo kwenye kisogo. Akili yako ndiyo majibu yote ya maisha yako. Muhimu hapo ni kuitumia vyema akili yako kuwaza sana ili upate wazo ambalo litaleta mapinduzi kwenye jamii na hatimaye kubadili kabisa maisha yako. Unaweza ukabaini tatizo la kukithiri kwa uchafu mtaani kwako,
ukaanzisha mradi wa kuzoa na kuchoma takataka. Yaani ukawa unapita kwenye majumba ya watu na kukusanya takataka, lakini kwa weledi wa hali ya juu kabisa na ukiondoka wabaki wanasemezana, kweli huyu jamaa amefanya usafi wa maana na kesho yake watakuita tena na hapo utaanza kujikusanyia pesa za kukuza na kuimarisha zaidi kazi yako ya uzoaji wa takataka, pesa zitaanza kumiminika. Utaanza kuitwa kwenye majumba, lakini kadiri siku zinavyokwenda, utaanza kuitwa kwenye maofisi makubwa na hatimaye kupata tenda kwenye mashirika ya umma na binafsi kwa ajili ya usafi, kwa hapo hujawa tajiri kutokana na pesa utakazokuwa unajikusanyia?

 

TUKUBALIANE KWA HILI

SASA Kwa hiyo zama za kulalamika kwamba huna mtaji wa pesa zimepitwa na wakati na badala yake mtaji wa maskini siyo nguvu tu, bali ni nguvu na akili yake. Unajua akili zetu zina uwezo mkubwa mno wa kutupa kila tunachokitaka, tena kwa wakati. Tatizo ni kwamba hatuzitumii kwa kiwango kinachohitajika. Ni asilimia chache sana za uwezo wa akili ambazo hutumika katika kufanya na kuwezesha mambo. Hebu kuanzia leo chukua hatua ya kubadili maisha yako. Hapo ulipo, hebu haraka sana kama uko nyumbani ingia ndani na ukajitazame kwenye kioo. Hata kama uko mtaani tafuta sehemu yoyote yenye saluni na ukajitazame kisha ujisemee moyoni maneno haya; “Mungu aliponiumba alinipa zawadi moja ambayo ni kubwa na muhimu mno, zawadi hiyo ni akili yangu. Kuanzia leo natumia uwezo wangu wote wa akili kupambana na maisha. Nilizaliwa kuwa mshindi na mimi ni kichwa na siyo mkia. “Niko hapa nilipo kutokana na uamuzi ambao niliuchukua bila kujua, kuanzia leo nabadilisha aina ya matendo yangu, naondoa marafiki wote ambao hawana umuhimu kwangu, najua moyo utaumia, lakini akili imeshaamua hivyo, kifupi ni kwamba sasa napiga hatua kuitafuta hatma ya maisha yangu ambayo Mungu alinimaanishia na nimechoka kuishi maisha ya kuigiza na kubaki msindikizaji wa wenzangu, Mungu nisaidie na ukanyooshe mapito yangu, Amina.” Maneno haya ni nguvu mpya unayoipandikiza ndani yako. Sikiliza ndani yako, kuna uwezo mkubwa na wa ajabu mno ambao unasubiri amri yako tu utende mambo. Dunia hii ina pesa nyingi mno. Ndugu zangu, maisha ni kupambana na hatima ya maisha yako iko mikononi mwako. Wiki ijayo nitamalizia sehemu ya pili na ya mwisho ya mada hii. Kwa maoni, tafadhali tuwasiliane kupitia namba hizi; 0673 42 38 45.

Comments are closed.