The House of Favourite Newspapers

Joto la Mapenzi – 50

0

“Da’ Koleta unakumbuka siku chache baada ya kusema utamuua baba, kilitokea kifo cha baba kibaya zaidi wewe ndiye uliyekuwepo hospitali. Baada ya kujua kuwa wewe ndiye uliyempokea mama na siku hiyohiyo kifo cha baba moja kwa moja nilijua umetimiza dhamira yako.

“Kwa kweli pamoja na kulia sana niliamini moyoni unachekelea kumuua baba yako kwa ajili ya mwanaume ambaye anaweza kukugeuka wakati wowote.”SASA ENDELEA…

“Ester kwa jina la Mungu, kifo cha baba mi sihusiki kwa njia yoyote japo waswahili wanasema ulimi uliponza kichwa.”

“Dada utajitetea tu lakini ukweli unabakia moyoni mwako kuwa ulimuua baba yako kwa ajili ya mwanaume.”
“Ester mbona hukunieleza jambo hili muda mrefu?”
“Hata ningekueleza usingenielewa.”

“Sasa leo nakuelewa?”
“Nina imani hata machungu yamekwisha tunazunguza kirafiki wala hakuna mtu mwenye hasira.”

“Ina maana kama baba angekuwa ni baba yako mzazi ungeweza kunifanyia kitu kibaya siyo kwa kuamini mimi ndiye niliyemuua?”

“Mmh! Sijui ila ningeumia sana kwani naamini mzazi hakosei ningekuwa tayari kumsamehe kwa lolote alilonitendea kwa kuamini mpaka kufika hapo ni juhudi zake.
“Unamtendea ubaya kwa kosa dogo tu la mapenzi na kusahau una deni kubwa la kulipa malezi yake kwako? Alikujali na kukupenda na kukupa kila ulichotaka. Lakini mwisho wa siku malipo yake ni kumuua baba yako kwa ajili ya mwanaume?” Ester alizungumza kwa sauti ya uchungu.

“Ina maana habari hizi ulimwambia mama?” Koleta alimuuliza.
“Ili iweje? Kwa vile tulizungumza wawili basi nilichokifikiria kiliishia moyoni mwangu.”
“Ester ninachokueleza ndiyo ukweli wenyewe.”
“Ukweli gani?”

“Ni kweli siku namrudisha mama nyumbani nikiwa na lengo la kwenda kumuua baba. Lakini baada ya kubakia chumbani peke yangu na baba, nilipomuangalia huruma ilinijia na kuyakumbuka maneno yako na kusitisha uamuzi wa kumuua baba yangu na kuuapia moyo wangu kuwa sitawaza tena wazo baya la kumuua baba yangu na kutafuta njia yoyote ya kumaliza tatizo la Ambe na familia yangu.

“Basi mdogo wangu baada ya kuwaza yale nilijilaza pembeni ya baba ili kumwangalia mgonjwa. Usiku niliamshwa na muuguzi na kunieleza kuwa baba amekufa kwa kweli nilishtuka sana.”

“Dada unajitetea tu lakini ukweli unabakia moyoni mwako.”
“Kama nimemuua kwa nini nikatae, ni mimi mwenyewe nilisema mbele yako kuwa nitamuua baba. Lakini leo nakueleza sikumuua unanikatalia una ajenda gani au umetumwa unipeleleze?” Koleta alikuwa mkali baada ya kuona Ester kashindwa kuuelewa utetezi wake.

“Hapana dada wala sikupelelezi ila nilikuwa nadhani tu kutokana na kauli yako mwenyewe ya kutaka kumuua baba.”

“Nimekueleza tangu mwanzo kuwa ulimi uliponza kichwa, hata mimi maneno yangu kwako leo yananihukumu lakini nimekueleza ukweli kuwa sihusiki na kifo cha baba husikii nikuambie nini unielewe?” Koleta alimjia juu Ester.

“Nisamehe dada kwa kukukwaza.”
“Si kunikwaza bali kuwa muelewa sijawahi kukudanganya, nikudanganye ili iwe nini? Ester nimeisha kueleza siri ambazo hakuna mtu yeyote anayezijua. Hata suala la kutaka kumuua baba nilikueleza wewe, kama ningekuwa nimemuua kwa nini nikufiche?”
“Sawa dada nisamehe kwa kuwaza vibaya.”

“Nimekusamehe lakini kuwa makini.”
“Nimekuelewa dada yangu, sasa nani kamuua baba?”
“Hata mimi sijui.”

“Huenda ni shemeji katimiza aliyoyasema juu ya kugeukwa.”
“Ester jiepushe kuwaza vitu vya kufikirika, una uhakika gani ikiwa mtu hatujui kama yupo salama.”

“Dada shemeji Ambe yupo hai, ipo siku utamuona tu nakuapia.”
“Mmh! Na maneno yako yawe ya kweli ili nimuone mpenzi wangu.”
“Samahani dada kama nitakuudhi kwa swali langu.”
“Umeanza tena, swali gani tena?”
“Kuhusu shemeji Ambe.”

“Kafanya nini?”
“Kwa mfano shemeji akisema yeye ndiye kamuua baba atafanyaje?”
“Nifanye nini kivipi?”
“Utapokeaje taarifa hiyo?”

“Sitafanya lolote kwa kuamini kila mmoja atakuwa ametimiza alichokikusudia.”
“Kukusudia kivipi?”
“Aliahidi kabla ya kufa yeye atakufa baba, nami nilimhakikishia hakuna tatizo yakageuka. Alichokifanya baba kama ni kweli aliyemuua ni baba Junior naamini malipo yale yalimstahili.”

“Kama yalimsitahili kwa nini ulilia sana?”
“Kwa vile ni baba yangu.”
“Angekuwa mtu mwingine?”
“Siwezi kujibu kitu ambacho sikijui.”

Kwa vile muda ulikuwa umekwenda sana kila mmoja alikwenda chumbani kwake. Koleta pamoja na kuamini Ambe amekufa, alijikuta akikubaliana na Ester huenda alikuwa hai. Swali likabakia kama yupo hai alikuwa wapi. Usiku akiwa amejilaza alishtuliwa na mkono uliokuwa ukimpapasa. Alipofumbua macho alishtuka na kutaka kupiga kelele asiamini alichokiona mbele yake lakini alikatazwa ndipo akatetemeke mpaka haja ndogo kumtoka.

“Shiii,” sauti ilimkataza kupiga kelele.
“Ha…ha…pana,” Koleta alibabaika kuona kitu ambacho hakutegemea kukiona usiku ule.
“Hapana nini?” sauti ilimuuliza kwa sauti ya chini.
“Ni wewe?”

“Ndiyo mimi.”“Kwa nini lakini?”
“Kwa nini nini?”
“Kwa nini unanitesa?” Koleta alimwaga machozi.
“Nani anateseka kati yako na mimi?”

“Najua unateseka mpenzi wangu, lakini hata mimi nimekuwa nikiteseka zaidi, ulikuwa wapi?”
“Hata mimi sijui, ni Mungu tu ndiye anayenilinda.”
“Unajua baba amefariki?”
“Ndiyo najua, hata kwenye mazishi nilikuwepo.”
“Mbona sikukuona?”

“Sikutakiwa kuonekana kwa vile bado natafutwa na pengine vifo vyote vya polisi na baba yako ningepewa mimi unafikiri ningeshikwa ningepona?”
“Kweli usingepona, ulikwenda wapi mpenzi wangu?”
“Hata mimi sijui.”

“Unanipenda kweli?” Koleta aliuliza kwa sauti ya kilio.
“Ningekuwa sikupendi nisingeuza uhai wangu, nimekuwa kama gaidi kila kona natafutwa, yote kwa ajili ya mapenzi yangu kwako nikupende vipi? Hivi kweli dunia ya leo iliyojaa wanawake wazuri wanaozaliwa kila siku kuna mwanaume anaweza kupoteza muda wake kwa ajili ya mwanamke mmoja tena mwenye kumletea matatizo?”

“Ni kweli mpenzi wangu, hata mimi nimekuwa tayari kukaa bila mwanaume kwa kipindi kirefu. Nimekuwa nateseka moyoni mwangu baada ya kuona kama nakukosea pia si mwanamke mkweli kwako kwa kukuingiza kwenye matatizo kila siku. Nateseka kwa kuhofia kukupoteza mpenzi wangu naamini bila wewe sina maisha.”
“Sasa kwa nini huniamini, nifanye kitu gani uamini?”
“Wasiwasi wangu kukupoteza wewe!”

“Niliapa kutengana na wewe labda nife au wewe kunikataa mimi.”
“Ambe nilikufungia moyoni mwangu na ufunguo niliutupia bahari katu hutatoka moyoni mwangu mpaka nakufa.”
“Ndiyo maana nimejitoa kwa ajili yako.”

“Mbona usiku mpenzi na umeingiaje?”
“Nimekuja usiku kwa vile mchana natafutwa.”
“Si ungenipigia simu nikukute sehemu?”
“Sina simu.”

Itaendelea wiki ijayo.

Leave A Reply