The House of Favourite Newspapers

Joto la Mapenzi – 51

0

ILIPOISHIA:
“Ambe nilikufungia moyoni mwangu na ufunguo niliutupia baharini katu hutatoka moyoni mwangu mpaka nakufa.”
“Ndiyo maana nimejitoa kwa ajili yako.”

“Mbona usiku mpenzi na umeingiaje?”
“Nimekuja usiku kwa vile mchana natafutwa.”
“Si ungenipigia simu nikukute sehemu?”
“Sina simu.”SASA ENDELEA…

“Shemu yupo wapi?”
“Nina wiki sijaonana naye.”
“Sasa mnaishije?”
“Ni historia ndefu.”

“Niambie basi mpenzi wangu.”
“Nitakwambia muda si mrefu.”
“Mmh! Sawa.”
“Naomba nikuage,” Ambe alimwambia Koleta.
“Ha! Mpenzi mbona haraka,” Koleta alishtuka.

“Ni kweli lakini muda wa mimi na wewe kukaa pamoja bado.”
“Twambe utaniua kwa mawazo.”
“Siwezi, vumilia tu kila kitu kitakwenda vizuri.”
“Kitakwenda vizuri mpaka lini, kumbuka nami nahitaji faraja yako.”

“Hilo nalijua au unataka nionekane kisha nifie gerezani au ninyongwe kabisa?”
“Sasa tutafanyaje? Basi nipeleke ulipo ili tuwe pamoja.”
“Toka tuanze mapenzi tumefurahia mapenzi yetu kwa muda gani?”
“Muda mchache sana.”

“Na mateso ya mioyo yetu?”
“Yamekuwa ya muda mrefu, kama moyo ungekuwa unavuja jasho kutokana na joto la mateso tunayoyapata ungekuwa umekauka.”
“Basi kama unajua hivyo nilikuja kukueleza jiandae kwa maisha mapya.”
“Tutaishi wapi?”
“Hiyo kazi niachie mimi.”

“Sawa mpenzi wangu, mama nimwambie?”
“Usimwambie kuna siku nitakuja rasmi tena mchana kweupeee na kupanga kila kitu.”
“Matatizo yako yatakuwa yamekwisha?”
“Kifo cha baba yake kimemaliza kila kitu.”
“Ina maana polisi hawakutafuti tena?”

“Wanitafute kwa kosa gani?”
“Kwa makosa ya nyuma.”
“Nani atawaambia?”
“Hakuna.”

“Basi jiandae kunipokea mchana na siku hiyo tutasafiri hadi nje ya nchi kufunga ndoa. Niandalie milioni kumi na passport zenu wote, nitamtuma mtu atazifuata dukani kwake kesho sawa mpenzi?”

“Hakuna tatizo, sasa utakuja lini?”
“Nitakujulisha.”
“Sawa mpenzi basi naomba ulale mpaka asubuhi.”
“Hapana sitakiwi kukutwa na mchana.”
“Jamani wewe mtu gani usiyetakiwa kuguswa na mchana ikiwa mbaya wako baba amekwishafariki?”

“Naomba uwe muelewa mpenzi wangu, ukiwa mbishi utanipoteza kabisa.”
“Sawa nakuombea kwa Mungu akulinde siku zote za maisha yako ili ndoto yangu ya siku moja kuwa mke na mume itimie.”

“Kwa heri mpenzi wangu, msalimie sana mwanangu Ambe Junior.”
“Salamu zimefika au nikamuamshe akuone?”

“Hapana siku itafika ataniona mpaka atachoka, kwaheri,” Ambe alimbusu Koleta na kutoka nje, Koleta alipotaka kumsindikiza alimkataza.
“Hapana we lala tu mpenzi,” Koleta alimuona Ambe akitoka nje, baada ya dakika kumi alinyanyuka kitandani na kutoka nje kwa kunyata.

Alitoka hadi sebuleni ambako palikuwa giza na kwenda hadi mlango wa kutokea nje, ulikuwa umefungwa. Alijiuliza ni kweli amezungumza na Ambe au alikuwa akiota. Alirudi ndani na kujilaza kitandani akiwa haamini, hakutaka lipite kimya, alimfuata Ester chumbani kwake ambaye alishtuka kuamshwa usiku wa manane.
“Vipi dada mbona saizi?”

“Kuna kitu kimenichanganya sana.”
“Kitu gani?”
“Kuna kitu kimenitokea kinanichanganya sijui ni ndoto au kweli.”
“Kitu gani tena hicho?” alimuelezea alivyotokewa na Ambe usiku ule na yote waliyozungumza.

“Mmh! Itakuwa ndoto tu hiyo.”
“Lakini nimezungumza naye na kunieleza vitu anavyovitaka nimpatie kwa ajili ya harusi yetu.”
“Vitu gani?”
“Fedha na picha za watu wote kwa ajili ya safari ya kwenda kufunga ndoa nje ya nchi.”
“Mmh! Hiyo safari ya wapi?”
“Kwa kweli hakunieleza.”

“Mmh! Fanya hivi hiyo keshokutwa chukua vitu vyote alivyovitaka kwako pamoja na hiyo fedha utajua kama ni ndoto au kweli.”
“Mmh! Sawa, mwaka huu nisipokuwa mwendawazimu siwi tena.”
“Punguza mawazo, kama ni ndoto inakuonesha Ambe yupo hai.”
“Kama ni kweli?”

“Ni kitu cha kushukuru, sishangai Ambe kuingia ndani kama aliweza kuokolewa kwenye mikono ya polisi wenye silaha, bila ulinzi anashindwa vipi.”
“Mmh! Haya na Mungu amlinde.”

Koleta aliagana na Ester na kurudi chumbani kwake kulala. Akiwa amejilaza kitandani bado alikuwa na maswali yasiyo na majibu, alijiuliza ile ilikuwa ndoto au kweli Ambe mpenzi wake aliingia ndani na kuzungumza naye. Alikubaliana na mawazo ya Ester kuwa siku aliyoelezwa afanye kama alivyoelekezwa ili aone ilikuwa ndoto au kweli.

Bila kutegemea alipitiwa usingizi mpaka siku ya pili.
* * *
Siku aliyoahidiwa alichukua vitu vyote alivyoelezwa na Ambe awe navyo na kumpa mtu atakayemtuma. Akiwa dukani mawazo yake yote yalikuwa kwa mpenzi wake. Mpaka inaingia mchana hakukuwa na dalili zozote za mtu kuja kuchukua mzigo, kitu kilichomtia wasiwasi Koleta na kumuuliza Ester.

“Ester nina wasiwasi ile ilikuwa ndoto.”
“Kwa nini?”
“Mpaka muda huu sijamuona mtu.”
“Dada mbona muda bado.”

“Kama angekuwa mtu wa kuja angekuwa ameshakuja, nina wasiwasi huenda ilikuwa ndoto lakini Ambe ameshakufa.”
“Dada mbona unapenda kumuua shemeji, tusubiri mpaka jioni ili tuwe na uhakika kama ni ndoto.”

“Ester unanipa moyo lakini unaelewa kabisa siku ile tulizungumza mengi juu ya Ambe na siku zote ukimuwaza sana mtu lazima umuote. Wewe mwenyewe uliona milango yote ilikuwa imefungwa lakini niliota kaingia ndani na kutoka.”

“Si vibaya kuleta vitu na mtu asitokee, ingekuwa mbaya ukakaidi kuleta ukiamini ni ndoto na kisha atokee huoni kama ungezidi kumkwaza shemeji.”
“Mmh! Mbona mwaka huu Ambe atanitesa, heri ningejua moja basi.”
“Kujua lipi?’

“Kama mzima au amekufa.”
“Ili iweje?”
“Kama amekufa nisimfikirie kwani siku moja tutakuja kuonana na kama mzima basi ajitokeze ili nami basi nipumzike kama wengine wenye wapenzi wao.”
“Dada jambo hili linahitaji subira.”
“Miezi sita midogo?”

“Mingi lakini hatujui Ambe baada ya kutoka katika mikono ya polisi amekwenda kujificha wapi?”
“Hujui kiasi gani mapenzi kwa upande wangu yamekuwa mateso, toka niyajue mapenzi sijawahi kufurahi kama wenzangu,” Koleta alisema kwa uchungu.

“Najua dada, lakini bado nakuomba tuvute subira kwa leo ili tuone ni ndoto au kweli.”
“Yaani nakumbuka wakati nimelala nilipapaswa na kufumbua macho na kumuona Ambe na kuzungumza naye, toka hapo sikulala mpaka nilipokuja kwako. Sasa jamani kuna ndoto ya mtu kuota akiwa macho?”

“Kwa kweli bado umenipa wakati mgumu wa kujua ilikuwa ndoto au kweli.
Itaendelea wiki ijayo.

Leave A Reply