The House of Favourite Newspapers

Unending Love – 60

1

Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kutoa figo yake moja na kumpa Anna ambaye alikuwa na matatizo ya figo zake kushindwa kufanya kazi. Anaamua pia kukataa kusomea upadri akiamini kwamba akimaliza shule, ataoana na Anna ili waishi kama mume na mke.

Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa Anna, wazazi wa msichana huyo wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi Jafet na wazazi wake. Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani.

Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William. Mapenzi yao yanaendelea na baadaye Anna ananasa ujauzito lakini William anamruka futi mia moja.

Anna anaamua kutoroka kurejea nyumbani kwao, Mwanza bila William kujua chochote na mipango ya wazazi wake kumtoa ujauzito kihalali kutokana na matatizo ya kiafya yaliyokuwa yanamsumbua inafanikiwa lakini matatizo mengine ya figo yanazuka upya na kusababisha akalazwe.

Upande wa pili, Suleikha anazidi kumganda Jafet kama ruba na hatimaye wawili hao wanaingia rasmi kwenye uhusiano wa kimapenzi.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

“Mungu wangu, inaonekana kuna tatizo kwenye figo aliyopandikizwa, imeharibika kutokana na kushindwa kufuata dozi ya dawa alizoandikiwa na pia kwa sababu ya matumizi ya pombe, inabidi alazwe haraka sana,” alisema daktari aliyempokea Anna katika Hospitali ya Bugando jijini Mwanza.

Wazazi wake hawakuwa na cha kufanya, mipango ikafanyika haraka ambapo Anna alilazwa kwenye wodi maalum na kutundikiwa dripu huku madaktari wakiitana kwa dharura kujadiliana juu ya namna ya kumsaidia msichana huyo.

“Unajua wakati mwingine huu unakuwa ni uzembe wa wazazi, kwa nini mgonjwa anakaa muda mrefu bila kunywa dawa na hakuna anayeshtuka? Kwa nini mtu anakunywa pombe wakati inafahamika kwamba anaumwa?”

“Dokta huu siyo muda wa kulaumiana, wazazi wana makosa, mgonjwa mwenyewe ana makosa lakini kwa sasa jambo muhimu ni kuhakikisha tunamsaidia huyu binti,” madaktari walikuwa wakijadiliana ndani ya ofisi yao. Hali ya Anna ilionesha kuwachanganya mno.

“It seems she has a Non Adherence Syndrome which has been caused by not taking her anti-rejection medication. As the results the body has reacted to transplanted kidney and destroyed it.”

(Inaonekana amepatwa na tatizo ambalo kitaalamu linaitwa Non Adherence lililosababishwa na mgonjwa kushindwa kufuata dozi ya dawa za kuzuia mwili kuikataa figo yake. Matokeo yake mwili ukaanza kuikataa figo iliyopandikizwa na kuiharibu kabisa).

Dokta Marthers Lucille, mtaalamu wa magonjwa ya figo kutoka nchini Marekani aliyekuwa amekuja Hospitali ya Bugando kwa ajili ya ziara ya kikazi ya kuwasaidia wagonjwa wenye matatizo hayo, aliwaambia madaktari wenzake wakati wakiendelea kujadiliana kuhusu hali ya Anna.

“What can we do now?” (Tutafanya nini sasa?)
“She must be administered to Dialysis as soon as possible.” (Ni lazima aingizwe kwenye tiba ya Dialysis haraka iwezekanavyo).

“But our hospital here is not well equipped to offer such a service to critical patients like her. Maybe it will be better if we refer her to Muhimbili National Hospital in Dar es Salaam.”

(Lakini hospitali yetu haina vifaa vya kutosha kutoa huduma hiyo kwa wagonjwa ambao wapo kwenye hali tete kama huyu. Nafikiri itakuwa bora kama tutampa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam) daktari mkuu wa hospitali hiyo aliwaambia wenzake, wazo ambalo kila mmoja alilikubali.

Ikabidi wazazi wa Anna waitwe haraka na kupewa maelekezo hayo ambapo nao waliafikiana mara moja. Kwa kuwa fedha hazikuwa tatizo kwa baba yake Anna, harakaharaka mipango ya kumsafirisha Anna kuelekea jijini Dar es Salaam ikaanza. Kutokana na hali yake jinsi ilivyokuwa ilikuwa ni lazima asafirishwe kwa ndege.

Baada ya kila kitu kukamilika, Anna alitolewa Hospitali ya Bugando kwa gari maalum la kusafirishia wagonjwa (ambulance) na kukimbizwa mpaka Uwanja wa Ndege wa Mwanza. Kwa kuwa tayari mawasiliano yalikuwa yameshafanyika, muda mfupi baadaye Anna aliingizwa kwenye ndege iliyokuwa ikikaribia kuondoka na kwenda kulazwa kwenye chumba maalum kilichotengwa kwa ajili ya wagonjwa kama yeye.

Dakika kadhaa baadaye, ndege ilianza kujongea taratibu kuelekea kwenye njia za kurukia (run ways), ikazidi kuongeza kasi huku muungurumo wa injini ukizidi kuongezeka na muda mfupi baadaye, ilipaa na kuiacha ardhi ya Mwanza, safari ya kuelekea jijini Dar es Salaam ikaanza.

“Usijali utapona mwanangu, sisi wazazi wako tutafanya kila kinachowezekana kuhakikisha unarudi kwenye hali yako ya kawaida,” alisema baba yake Anna na kumbusu mwanaye huyo kwenye paji la uso, kauli ambayo pia iliungwa mkono na mama yake. Wakawa wanaendelea kumbembeleza binti yao huyo na kumtaka aamini kwamba atapatiwa matibabu ya uhakika na kurudi kwenye hali yake ya kawaida.

Baada ya kusafiri angani kwa takribani saa moja, ndege iliyokuwa imewapakiza Anna, wazazi wake pamoja na abiria wengine, iliwasili jijini Dar es Salaam, ikatua salama kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ambapo mipango ilifanyika harakaharaka, Anna akashushwa kwenye ndege na kupelekwa kwenye gari maalum la kubebea wagonjwa.

Harakaharaka akaondolewa uwanjani hapo na kukimbizwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
* * *
“Ahsante kwa kunipenda Suleikha, na mimi naahidi nitakuwa na wewe na nitakupenda kadiri ya uwezo wangu wote,” alisema Jafet na kumkumbatia Suleikha kimahaba. Muda mfupi baadaye, wawili hao waligusanisha ndimi zao na kuanza kuwaiga njiwa wanavyoyalisha makinda yao.

Kwa mara nyingine, Jafet na Suleikha walijikuta wakielea kwenye ulimwengu wa kimapenzi huku kila mmoja akionesha kuzama kwenye dimbwi la mahaba lenye kina kirefu.

Siku hiyo ilipita, mapenzi kati ya Suleikha na Jafet yakazidi kuongezeka na kuwafanya wawili hao kuwa gumzo kila walipokuwa wanakwenda, ndani na nje ya chuo hicho. Furaha ya Jafet ilizidi kuongezeka kila kukicha, afya yake nayo ikazidi kuimarika huku kila kitu kikibaki kuwa historia kwenye maisha yake.

“Jafet! Jafet!”
“Vipi mbona mbiombio Lazaro?”
“Nimetumwa na Dean (mlezi wa wanachuo) kuja kukuita, amesema kuna dharura inabidi uwahi haraka iwezekanavyo,” Lazaro, mwanachuo aliyekuwa akisoma na Jafet, alimkurupusha kijana huyo aliyekuwa amepumzika kwenye chumba chake akiwa na Suleikha.

“Kuna nini tena?” Suleikha aliingilia kati mazungumzo lakini hakuna aliyekuwa na majibu, harakaharaka Jafet akajiandaa na kutoka. Huku nyuma Suleikha naye alijiandaa na kuwafuata, akiwa na shauku kubwa ya kutaka kujua kilichotokea.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

1 Comment
  1. ahady kidehele says

    haya kamtibu anna nadhanii amekuja mikoni mwako

Leave A Reply