The House of Favourite Newspapers

Julio, Sekilojo Chambua, Waingia Mitaani Kusaka Vipaji Vya Soka Na Kucheza Safari CUP, Mchezaji Bora Kusajiliwa (EPL)

0
Kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ akimpa mpira Meneja wa Bia ya Safari Lager, Pamela Kikuli. Kushoto ni aliyekuwa mshereheshaji wa tukio hilo, Mbwiga Wambwiguke na kulia ni kocha, Sekilojo Chambua.

Dar es Salaam 19 Septemba 2023: Makocha wazawa wa hapa nchini, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na Sekilojo Chambua wamepewa kazi maalum na Kampuni ya Bia ya TBL kupitia bia ya Safari Lager kutafuta vijana wa mitaani kwenye mikoa ya Mbeya, Arusha, Mwanza na Dar es Salaam  wenye vipaji vya soka kwaajili ya kushiriki michuano ya kuibua vipaji iitwayo Safari CUP.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo hiyo, Meneja wa Bia ya Safari, Pamela Kikuli amesema wamewachagua makocha hao kutokana na uzoefu na heshima yao katika soka na wanaimani kuwa zoezi hilo watalifanya kwa haki. Kikuli ameendelea kusema;

Mshereheshaji kwenye hafla hiyo Mbwiga Wambwiguke (kushoto) akiwa na makocha Julio na Sekilojo (kulia)

“Kampeni hii ya Safari Cup ina lengo la kutafuta mabingwa wapya katika tasnia ya mpira wa miguu ambayo itasindikizwa na kauli mbiu ya “Mabingwa wapya katika kandanda”.

“Tunaamini hapa nchini kuna vipaji vingi sana vya soka lakini mpaka sasa wachezaji hao hawajasajiliwa kwenye ligi yeyote, kwa hiyo lengo kuu la kampeni hii ni kwenda kusaka vipaji hivyo katika mikoa mbalimbali.

“Na katika kusaka vipaji hivyo mpango huo utafanywa na makocha wenye uzoefu Jamhuri Kihwelo maarufu kama Julio na Sekilojo Chambua na tutaenda mikoa mbalimbali kuchagua wachezaji hao ambao tutawapambanisha na kupata wachezaji 22 kwa mkoa kwa mikoa minne tutakayoanza nayo kutembelea.

“Wachezaji hao wa mikoa hiyo minne tunatarajia kuwachuja na kupata wachezaji 22 ambao tutawakuza na kuwapa mazoezi na kisha kuwashindanisha na moja ya timu kubwa hapa nchini ambayo tutaitangaza hapo baadae.

“Katika mechi hiyo mchezaji atakayeibuka mchezaji bora kutoka katika hao 22 atapata nafasi ya kusajiliwa na moja ya timu zinazoshiriki ligi kuu ya nchini Uingereza (EPL) na wachezaji hao watapata kifuta jasho cha shilingi milioni 44” Alisema Kikuli.

Kikuli aliitaja mikoa hiyo minne kuwa ni Mbeya ambapo zoezi hilo litafanyika Viwanja vya FFU Oktoba 7 mwaka huu, Arusha Oktoba 21 katika Viwanja vya Ngarenaro, Mwanza Novemba 4 katika Viwanja vya Nyamagana na kumalizia na Dar es Salaam Novemba 18 mwaka huu katika Uwanja wa Kinesi uliopo Ubungo.

Kikuli amewataka vijana wapenda soka na wenye vipaji kujitokeza kwa wingi kwenye maeneo hayo yaliyotajwa tarehe husika kwa ajili ya mchujo kwani kwa wenye vipaji vya kweli na hawakuwa na nafasi ndiyo nafasi pekee ya kuonesha uwezo.

Leave A Reply