The House of Favourite Newspapers

Juuko Aomba Asicheze Simba SC

Said Ally, | CHAMPIONI|  Dar es Salaam

BEKI Mganda, Juuko Murshid, licha ya kurejea kwenye kikosi cha timu hiyo, ameomba asichezeshwe kwa sasa, bali apewe muda zaidi wa kufanya mazoezi kwa ajili ya kurejesha makali yake kutokana na kukaa muda mrefu nje bila kufanya mazoezi yoyote.

Juuko alitoweka kwenye kikosi hicho cha Simba kinachonolewa na Mcameroon, Joseph Omog, tangu alipokwenda kushiriki michuano ya Afrika (Afcon) mwaka huu alipokuwa na kikosi cha Uganda ‘The Cranes’ kabla ya kurejea hivi karibuni.

Juuko alikuwa sehemu ya mipango ya kocha Omog kwenye mchezo dhidi ya Mbeya City kutokana na Simba kutokuwa na mabeki wengi kwa sasa lakini aligoma kucheza kutokana na kutokuwa fiti, hivyo wakalazimika kumtumia Mghana, James Kotei katika nafasi ya ulinzi.

Kocha Msaidizi wa Simba, Mganda, Jackson Mayanja, amethibitisha kuwa beki huyo ameomba muda zaidi wa kukaa nje akifanya mazoezi. “Juuko hatukumtumia kwenye mechi na Mbeya City kwa sababu aliomba asicheze licha ya kwamba alikuwemo kwenye mipango na alitakiwa kuanza ila yeye mwenyewe akaomba asicheze kwa sababu hayupo fiti kwani tangu atoke Afcon hakuwahi kufanya mazoezi hata kidogo.

“Kuona hivyo tukaamua kumpumzisha na tukamtumia Kotei ambaye alicheza eneo hilo mechi na Yanga na akafanya vizuri, sasa tunamtengenezea Juuko mazoezi binafsi kwa ajili ya kumfanya arejeshe kiwango kama zamani,” alisema Mayanja. Mabeki wengine wa Simba ambao waliukosa mchezo huo ni Method Mwanjale ambaye bado ni mgonjwa, Novaty Lufunga ambaye hakuwepo kabisa na Janvier Bokungu ambaye ana adhabu ya kadi nyekundu.

Comments are closed.