The House of Favourite Newspapers

Kada CCM Auawa Kisa Sh 200

0

KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM); Kata ya Tungi, Manispaa ya Morogoro, Baraka Masuki amedaiwa kuuawa kwa kupigwa kichwa kwenye paji la uso na mteja wa baa yake aliyefahamika kwa jina moja la ldd huku chanzo kikidaiwa kuwa ni shilingi 200.

Masuki ambaye alikuwa Mjumbe wa Serikali ya Mtaa Tubuyu B, Kata ya Tungi kupitia CCM, alifikwa na umauti Januari 15 muda wa saa mbili usiku.

TUKIO LILIVYOKUWA

Aidha, wakizungumza na RISASI Mchanganyiko mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo; Maga Masoud, alisema baa hiyo ya Masuki ipo karibu na kituo cha daladala cha Tubuyu, hivyo madereva wanaposubiri foleni huelekea hapo kucheza Pool.

“Kulitokea mzozo kati ya wafanyakazi wa baa ya Mangi (Masuki) na jamaa mmoja aliyefahamika kwa jina moja la ldd ambapo alikuwa akidai tokeni ya Sh 200 na wafanyakazi hao waligoma kumpa tokeni hiyo, hivyo ldd kwa hasira naye akaamua kuchukua mipira miwili ya kuchezea pool na kuondoka nayo.

“Mmiliki wa baa yaani Masuki alipofika na kuelezwa, aliamua kwenda nyumbani kwa ldd kwa lengo la kufuata mipira ya Pool kama unavyojua mpira mmoja ukipungua hamuwezi kucheza.

“Inadaiwa alipofika nyumbani kwa ldd walipishana kauli, wakakunjana ndipo ldd akaona fedheha kukunjwa mbele ya familia yake na kuamua kujimwambafai kwa kumtwanga kichwa Mangi kwenye paji la uso ambapo alianguka na kupiga kisogo na kufariki.” Alisema Maga ambaye ni dereva wa daladala za Tubuyu Mjini.

MWENYEKITI AFUNGUKA

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Tubuyu B; lbrahimu Chombocho, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo kwenye mtaa huo na kubainisha kuwa ni pigo kubwa ndani ya chama cha CCM mkoa wa Morogoro.

“Marehemu alikuwa nguzo muhimu kwa chama chetu Kata ya Tubuyu, alishika nyadhifa mbalimbali kwenye chama na hadi mauti yanamfika alikuwa ni mjumbe wangu wa serikali ya Mtaa. “Kabla ya kifo, nusu saa nyuma nilikuwa naye na tulipoachana ndipo kaelekea kwenye baa yake” alisema mwenyekiti huyo.

Hata hivyo, Mwenyekiti huyo alisema mtuhumiwa huyo ambaye ni mkazi wa mtaa wake, ametoweka tangu alipotekeleza tukio hilo.

Aidha, RISASI lilimtafuta kwa njia ya simu bila mafanikio Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa ili kuthibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Marehemu ameacha mjane Helka Masuki, watoto sita na mjukuu mmoja.

Januari 19 mwaka huu ibada ya kumuombea marehemu iliyoongozwa na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) – Ushirika wa Mji Mwema Kata ya Tungi, Rhoda Chamshama nyumbani kwa marehemu, ilipokamilika muda wa saa 10 jioni, msafara wa kuelekea Moshi kwa mazishi ulianza.

STORI: DUSTAN SHEKIDELE, MOROGORO

Leave A Reply