The House of Favourite Newspapers

Kahaba Kutoka China-11

0

Maisha yalikuwa magumu kwa upande wake hasa mara baada ya fedha ambazo alipewa na Joshua kumuishia. Hapo ndipo picha halisi ya maisha ya shida yalipoanza kujitokeza katika maisha yake. Rose akawa mtu wa kushinda ndani tu, maisha yake yalkuwa na upweke mkubwa, kitendo cha kukosa fedha kilimuweka katika wakati mgumu sana.
Hakutaka kukata tamaa japokuwa hakuju ni kwa namna gani angeweza kupata fedha za kuweza kutatulia matatizo mbalimbali ambayo alikuwa nayo katika kipindi hicho.Majirani zake hasa Bi Fatuma ndiye ambaye alikuwa karibu nae zaidi katika kipindi hicho. Kila wakati mwanamke huyu alikuwa akiongea nae mambo mbalimbali hali iliyomfanya Rose kumwambia mambo mengi isipokuwa usagaji ambao alikuwa amefanyiwa na Irene.
Ukaribu wao haukuishia hapo, kila siku walikuwa pamoja huku Bi Fatuma akijitahidi sana kufanya vitu mbalimbali kwa ajili ya Rose. Yeye ndiye ambaye mara kwa mara alikuwa akimnunulia dawa ambazo kama mama mjauzito alitakiwa kunywa, yeye ndiye ambaye akaamua kuishi nae kama mmoja wa familia yake. Alikuwa akimpa chakula pamoja na mahitaji mengine madogo madogo.
“Unajua kupika?” Bi Fatuma alimuuliza Rose.
“Ndio najua” Rose alijibu.
“Unaweza kupika mama ntilie?” Bi fatuma alimuuliza.
“Kupika mama ntilie? Mmmh!”
“Unaguna nini tena? Au bado unayafurahia maisha haya?” Bi Fatuma alimwambia na kumuuliza.
“Hapana”
“Basi kila kitu weka chini na twende tukafanye kazi hiyo iweze kutuingizia fedha” Bi Fatuma alimwambia Rose ambaye alionekana kujishtukia kufanya kazi hiyo.
“Hakuna tatizo” Rose alijibu.
Japokuwa mdomoni alikubaliana nae lakini moyoni mwake alionekana kulikataa hilo. Kwanza alijaribu kuuangalia uzuri ambao alikuwa nao na kisha kuifananisha na biashara ambayo alitakiwa kuifanya. Alizaliwa katika familia iliyokuwa na fedha na hivyo hakuwahi kufikiria hata siku moja kama angekuja kuwa mama ntilie. Ila kwa sababu alikuwa na uhitaji wa fedha, hakuwa na jinsi, akaamua kukubaliana nae.
“Kwa hiyo tutauzia wapi?” Lilikuwa swali ambalo lilitoka mdomoni mwa Rose.
“Kuna ghorofa linajengwa kule Posta. Huko ndipo tutakwenda kufanya biashara hiyo” Bi Fatuma alimwambia Rose.
Hakuwa na jinsi, kwa sababu maisha kwa wakati huo yalikuwa magumu sana basi akaaamua kwa moyo mmoja kuanza biashara ya kuuza mama ntilie katika jengo ambalo lilikuwa kwenye ujenzi maeneo ya Posta. Kwake, kipindi cha kwanza kazi ile ilionekana kuwa kubwa sana lakini mwisho wa siku akajikuta akiizoea na kuwa kama kawaida.
Ndio, alikuwa msichana mzuri sana lakini hakukuwa na mvulana yeyote ambaye alimuonyeshea macho ya matamanio kutokana na ujauzito ambao alikuwa nao katika kipindi hicho. Ujauzito ule uliwafahamisha watu kwamba tayari Rose alikuwa na mtu kwa hiyo hakutakiwa kusogelewa na mwanaume yeyote yule katika kipindi hicho.
Mwili wake tayari ulikuwa umeongezeka, japokuwa alikuwa ni msichana mwenye mawazo kila wakati lakini mawazo yale hayakumfanya kupungua. Uzito ukaongezeka na hata mwili wenyewe kuongezeka. Uzuri haukupungua hata mara moja jambo ambalo liliwafanya wavulana kumwangalia sana kama ishara ya kuiridhisha mioyo yao.
“Oyaaa Hemedi unaweza kuniangushia jiwe la kichwa” Jamaa mmoja alimwambia mwenzake katika kipindi ambacho walikuwa wakipandisha matofali ghorofani kwa kutumia ngazi.
“Daah! Unajua Rose mzuri sana. Yaani mzuri sana” Hemedi alimwambia mwenzake.
“Najua ila sio unamwangalia hivyo mpaka unidondoshee jiwe la kichwa. Twende kwanza,       Rose yupo utamwangalia hata baadae” Jamaa yule alimwambia Hemedi.
Bado uzuri wa Rose uliendelea kuwa gumzo mahali hapo. Hakukuwa na mwanaume ambaye alithubutu kumwangalia kwa mara moja na kuyapeleka macho yake pembeni, uzuri wake ulikuwa ukiendelea kuwavutia wanaume wengi mahali hapo. Uzuri wake pia ukaonekana kuwa mvuto kwa wanaume wengi kuja kwake na kisha kununua chakula, wanaume hawakutaka kupitwa na kitu chochote kile jambo ambalo lilikuwa likimfanya kupata wateja wengi na kumaliza chakula kwa haraka sana.
“Shida yangu si chakula kingi Rose” Hussein alimwambia Rose.
“Sasa shida yako nini tena?” Rose aliuliza huku akitabasamu.
“Kuna watu wamezaliwa na bahati zao bwana. Yaani toka wapo tumboni mwa mama zao, tayari walikuwa wameandikiwa bahati” Hussein alimwambia Rose.
“Sijakuelewa”
“Hahaha! Hivi mtu kukupa tumbo msichana mzuri kama wewe…sio bahati hiyo?” Hussein alimuuliza Rose.
“Kwa nini unasema hivyo?”
“U mzuri sana. Huyo jamaa kweli alijua kuchagua aisee” Hussein alimwambia Rose maneno ambayo yaliwafanya vijana wengi waliokuwa mahali hapo kuanza kucheka.
Yeah! Kila mtu alikuwa akikubaliana na uzuri ambao alikuwa nao Rose. Vijana ambao walikuwa wajenzi mahali hapo walikuwa wengi sana kiasi ambacho kilimfanya Rose kumaliza chakula mapema sana. Kazi hiyo ambayo kwake ilionekana kuwa ngumu kufanyika katika kipindi cha nyuma kwa sasa alikuwa akiifanya kama kawaida.
Wachina hawakuwa wakila chakula mahali hapo lakini mara baada ya Rose kujifunza kupitia vitabu vya mapishi jinsi ya kutumia viungo vya kichina katika vyakula mbalimbali, akaanza kutumia. Alipoona kwamba amepika chakula ambacho hakikuwa kingi huku akiwa ametumia viungo vingi vya kichina ambavyo alivinunua katika supermarket, Rose akamwambia Lucy ambaye akafika mahali hapo na kisha kukionja chakula hicho.
Chakula kilionekana kuwa kitamu, viungo ambavyo vilikuwa vimewekwa katika chakula kile vilionekana kupendezesha chakula kile na kuleta ladha ile ambayo Wachina walikuwa wakiitaka midomoni mwao. Hapo ndipo hata wale makarani wa kichina wakaanza kula chakula kile alichokuwa akikipika Rose. Nao Watanzania hawakutaka kupitwa, nao pia wakaanza kununua chakula hicho ambacho kilionekana kuwa na ladha tofauti midomoni mwao.
Rose hakubagua wateja, chakula chenye ladha ya viungo vya kichina kikaongezwa na hatimae kuzidi kupata wateja zaidi. Lucy ndiye ambaye alikuwa akikifurahia sana chakula hicho kiasi ambacho kila siku alikuwa mtu wa kwanza kufika mahali hapo na kisha kununua chakula ambacho kilikuwa na ladha ya viungo vya kichina.
“Where did you learn to cook Chinese food? (Umejifunza wapi kupika chakula cha kichina?)” Lucy aliuliza huku akionyesha uso uliokuwa na tabasamu.
“From differerent books (Kutoka katika vitabu mbalimbali)”
“It is very delicious (Ni kitamu sana)” lucy alimwambia Rose.
“Thank you (Asante)” Lucy aliitikia.
Siku ziliendelea kukatika mpaka katika kipindi ambacho Lucy akapotea kabisa mahali hapo. Watu walikuwa wakijiuliza juu ya mahali ambapo alipokuwepo lakini kutokana na hali ambayo alikuwa nayo kabla, wengi wakagundua kwamba katika kipindi hicho alikuwa amejifungua mtoto kutokana na mimba ambayo alikuwa nayo kuwa kubwa sana katika kipindi kile cha nyuma.
Vijana wakaonekana kumkumbuka, vijana wakaukumbuka uzuri wake lakini zaidi ya yote, walikikumbuka chakula chake ambacho kilikuwa kinaonekana kuwa tofauti sana. Hapo ndipo vijana walipojipanga kwa ajili ya kwenda kumtembelea Rose ambaye bado alikuwa nyumbani. Baada ya Lucy kupata taarifa juu ya safari ambayo walikuwa nayo wajenzi, nae akaungana nao na kisha kuanza kuelekea huko.
Rose alikuwa akipendwa na kila mtu, katika kipindi hicho kila mtu alikuwa akitaka kumuona msichana huyo ambaye zilikuwa zimepita siku arobaini tangu aache kuja katika biashara yake. Kutoka Posta mpaka Kinondoni wala hakukuwa mbali sana, wakatumia dakika chache wakafika na kisha kumsalimia Rose ambaye alikuwa na mtoto wake aliyeonekana kuwa na afya njema.
“Kabla ya yote hebu tuambie, mwanajeshi au nesi?” Hemedi, kijana aliyeonekana kuwa mchangamfu sana aliuliza.
“Nesi” Rose alijibu huku akitabasamu.
“Afadhali sasa. Nadhani mtoto wangu kapata mrembo wa kuoa” Hemedi alimwambia Rose.
Siku hiyo ikaonekana kuwa furaha kwa kila mtu, kila mmoja alikuwa akitaka kumuona mtoto wa Rose ambaye alipewa jina la Lydia. Alionekana kuwa mtoto mzuri ambaye alichukua sura nzuri ya mama yake. Lucy hakuweza kuvumilia, akamchukua Lydia na kisha kumpakata, kwake alionekana kuwa mtoto mzuri zaidi.
Rose hakutaka kwenda tena katika biashara zake, kila siku alikuwa akiishi nyumbani pale akimlea mtoto wake ambaye alizidi kukua zaidi na zaidi. Bi Fatuma alikuwa mtu pekee ambaye alikuwa akimsaidia kwa kila kitu mahali hapo. Msichana Irene ambaye alikuwa akimtegemea nae alikuwa amekwishakata mguu kufika mahali pale jambo lililoonyesha kwamba alikuwa amekasirika kutokana na Rose kupata ujauzito na hivyo kumkatalia kumfanyia usagaji.
Rose hakujali, katika kipindi hicho tayari alikuwa amekwishafungua biashara yake ya kuuza chakula hapo hapo Kinodnoni, hakutaka kwenda mbali na nyumbani hapo kutokana na kuwa na mtoto ambaye mara kwa mara alikuwa akihitaji uangalizi mkubwa. Alisaidiana na Bi fatuma katika kila kitu, kwake, alimchukulia kama mama yake aliyemzaa.
“Kwa hiyo baba yake anakuja lini kumwangalia mtoto wake?” Bi Fatuma alimuuliza Rose.
“Wala sitaki aje kwa sasa”
“Kwa nini?”
“Basi tu. Kama akipajua mahali hapa, anaweza akapigwa mkwara na baba apataje nilipo, akipataja na baba kuja hapa, itakuwa sio vizuri” Rose alijibu.
Alichokuwa amekiamua Rose ndicho ambacho alikuwa amekiamua, hakutaka Joshua apafahamu mahali hapo, alitaka kubaki hivyo hivyo mahali hapo kwa ajili ya usalama wake. Lydia hakuwa mtoto wa kulia sana, mara nyingi alikuwa kimya ila alikuwa akipenda sana kunyonya.
Kidogo maisha yalikuwa yakienda sawa, hata pale ambapo Irene alipoamua kuonyesha ubaya wake kwa kuja kuchukua kila kilichokuwa chake, Rose hakubaki mikono mitupu, alikuwa amekwishaanza kununua baadhi ya vyombo mbalimbali ndani kwake. Kuhusu kulala, wala hakujali sana, godoro ambalo alipewa na Bi fatuma ndilo ambalo alikuwa akilitumia kulalia kila siku usiku.
“Mungu yupo. Kuna siku atakuona tu” Bi Fatuma alimwambia Rose maneno ambayo yalionekana kumfariji kupita kawaida.
Miezi iliendelea kukatika, mpaka mwezi wa sita unakwisha, Rose akapokea simu moja, simu ambayo ikaonekana kumshtua kupita kawaida. Kwanza hakuamini, hakuamini kama ile simu alikuwa amepigiwa yeye. Muda wote uso wake ulikuwa ukitabasamu kwa furaha, alikuwa akiongea huku machozi ya furaha yakiwa yakimtoka. Kwake simu ile ikaonekana kuwa kama sapraizi, akajikuta akizidi kutokwa na machozi zaidi.
Simu ilipokatika, Rose akaruka juu kwa furaha, simu ile ambayo aliipokea ikaonekana kumfurahisha kupita kawaida. Kelele za furaha yake ndizo ambazo zikamfanya Bi fatuma kufika ndani ya chumba kile ambapo akamkuta Rose akiendelea kuruka kwa furaha.
“Umasikini basiiiiiiiii….!” Rose alimwambia Bi Fatuma ambaye alionekana kumshangaa.

****

Yeah! Ilikuwa ni simu, simu moja ambayo ilimfanya Rose kuwa na furaha kupita kawaida, ilikuwa ni simu ambayo ilimfanya kujiona kama alikuwa anakwenda kuwa milionea katika kipindi kichache kijacho. Katika kipindi chote hicho, Rose alionekana kuwa na furaha zaidi, alikuwa akijipa uhakika kwamba katika kipindi kichache kijacho maisha yake yangekwenda kubadilika kabisa.
Hakuamini, alikuwa akijiona kama yupo ndotoni ambapo baada ya kipindi kichache kuamka  na kujikuta yupo katika godoro lililochoka ambalo alikuwa amepewa na Bi Fatuma ambaye alionekana kumjali kupita kawaida huku pembeni akiwepo mtoto wake, Lydia. Rose hakutaka kuongea kitu kingine kwanza, alikuwa akihitaji muda wa kushangilia hata kabla hajaongezea maneno mengine yenye furaha.
Bi Fatuma alikuwa na hamu ya kutaka kujua kuhusiana na simu ile ambayo ilimfanya Rose kuwa na furaha kupita kawaida. Kila alipomtaka Rose aongee zaidi na zaidi lakini Rose akaonekana kushindwa, bado furaha ilikuwa imemkaba kooni na hivyo alihitaji kufurahia zaidi.    Bi Fatuma hakuonekana kujali sana, alichokifanya ni kumpa nafasi zaidi ya kufurahia kwa kuamini kwamba baadae angeweza kumwambia ni kitu gani ambacho kilikuwa kimeendelea mpaka kuwa katika hali ile ya furaha. Baada ya kufurahia sana na kushangilia, Rose akakaa chini.
“Haya sasa niambie, kuna nini?” Bi Fatuma alimuuliza Rose.
“Nimepigiwa simu”
“Kutoka wapi?” Bi Fatuma alimuuliza.
“Kutoka kwa Bi Lucy”
“Yule mchina?” Bi fatuma aliuliza huku akionekana kushtuka.
“Ndio”
“Amesemaje?”
“Daah! Sijui niseme nini aiseee…yaani siamini” Rose alisema huku uso wake ukionekana kuwa na furaha tele.
“Kuna nini tena Rose? Mbona unanihadithia nusu nusu?” Bi Fatuma alimuuliza.
“Amenitaka niende nikaishi kwake” Rose alijibu huku meno yote yakionekana.
“Ukaishi kwake?” Bi Fatuma aliuliza huku akionekana kushtuka.
“Ndio. Daah! Najiona kubadilisha maisha yangu” Rose alimwambia Bi Fatuma.
“Ila bado sijajua kabisa kuhusiana na hilo. Ukaishi kwake ili iweje?” Bi Fatuma alimuuliza   Rose.
“Nikaishi kwake na kumsaidia kazi zake za pale nyumbani kwake. Hii ni taarifa nzuri sana kwangu, naamini shida zote zimefikia ukingni” Rose alimwambia Bi fatuma.
“Na vipi kuhusu mtoto?”
“Amesema niende nae pia”
“Sawa. Hiyo ni bahati lakini kamwe usisahau ulipotoka. Mshukuru Allah kwa kila kitu” Bi Fatuma alimwambia Rose.
“Siwezi kusahau na siwezi kumsahau Mungu. Kila siku nitatakiwa kumshukuru kwa kila kitu” Rose alijibu.
Siku hiyo ikaonekana kuwa siku nyingine, siku mpya ambayo Rose alikuwa ameiingia katika maisha yake, siku ambayo ilimpa furaha ambayo wala hakuwa akitegemea hata kidogo. Kitendo cha yeye kuitwa na Bi Lucy kwenda kuishi kule ndicho kitu ambacho kilionekana kumpa furaha kupita kawaida. Kwake, alikuwa na uhakika kwamba alikuwa anakwenda kubadilisha maisha yake katika kipindi hicho.
Mbele yake aliyaona mafanikio yakija kwa kasi sana, aliona kila kitu katika kipindi hicho kingekwenda vizuri kama ambavyo alikuwa amepanga, maisha ya shida na dhiki ambayo aliyaona kwamba angeyaishi mtoto wake, Lydia yakaonekana kuanza kufutika akilini mwake, katika kipindi hicho alijiona akikaribia kuishi katika maisha ya mafanikio kupita kawaida.
Kwake, kwa kitendo cha kwenda kuishi na Bi Lucy kikaonekana kuwa kitendo kimoja ambacho kilitakiwa kufanyika kwa haraka sana bila kujifikiria. Katika kipindi cha siku mbili za mbele, alitakiwa kuanza kazi kwa Bi Lucy, chakula ambacho alikuwa akikipika huku akiweka viungo vingi vya kichina ndivyo ambavyo vilionekana kumvutia Bi Lucy mpaka kufikia hatua ya kumtaka Rose aende akafanye kazi ndani ya nyumba yake.
Rose hakutaka kumfikiria Irene, alikuwa amepuuzia kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea katika maisha yake ya nyuma. Ni kweli kwamba alikuwa msagaji katika kipindi cha nyuma lakini ile haikumaanisha kwamba katika kipindi hicho alikuwa msagaji kama kipindi cha nyuma, kwa moyo mmoja alikuwa ameamua kuyabadilisha maisha yake, hakutamani tena kuwa msagaji.
Ukiachana na Irene, pia hakutaka kumfikiria sana baba yake, kwake, mwanaume huyo alionekana kutokuwa na utu, alikuwa akitumia nguvu zake kumlea mtoto katika malezi ambayo wala hakuwa akiyapenda, malezi ambayo hayakumpa uhuru wowote kwa kumfanyia jambo hili na lile. Katika kipindi cha nyuma alikuwa akimchukia sana baba yake lakini katika kipindi hicho hakuwa na jinsi, alitakiwa kumpenda baba yake, Bwana Shedrack kwani hakutaka kuanza safari ya mafanikio huku akiwa na mzigo wa chuki moyoni mwake.
Ukiachana na hao pia kulikuwa na mtu mwingine, huyu alikuwa Peter. Kwanza alichokifanya ni kusahau kila kitu ambacho alikuwa amekifanya pamoja na mwanaume huyo ambaye alikuwa na mapenzi ya dhati, mwanaume ambaye alikuwa akipambana kila siku kuhakikisha kwamba Rose anakuwa wake. Baada ya msaada mkubwa wa Bwana Shedrack, Peter akafanikiwa lakini hilo halikuwa jambo ambalo lilimpa furaha, alikuwa na Peter si kwa sababu alikuwa akipenda kuwa na mwanaume huyo, hapana, alikuwa nae kwa sababu alikuwa akitaka kumridhisha baba yake ambaye hakuonekana kuwa muelewa hata kidogo.
Ukiachana na hao wote, kulikuwa na mtu mwingine, mtu huyu alionekana kuwa maalumu kwa ajili yake, mtu ambaye alikuwa na mapenzi ya dhati, inawezekana kuwa zaidi ya watu wote, huyu aliitwa Joshua. Mwanaume huyu ndiye alikuwa mwanaume wa kwanza kupata nafasi ya kuuchezea mwili wake na kisha kufanya nae mapenzi kwa mara ya kwanza na kufanikiwa kumpa ujauzito.
Huyo ndiye alikuwa mwanaume pekee ambaye alikuwa ndani ya kichwa chake katika kipindi hicho, ni mara nyingi sana alikuwa akimkumbuka kwa mengi lakini katika kipindi hicho hakuwa na jinsi, alitakiwa kuishi maisha yake kwa wakati huo, maisha ya kujitegemea pamoja na mtoto wake huku akiamini kwamba kuna siku angeweza kuwa tena pamoja na mwanaume huyo ambaye alimpa nafasi kubwa ndani ya moyo wake.
Baada ya siku mbili kutimia, moja kwa moja Rose akafuatwa na gari mpaka nyumbani pale na kisha Bi Lucy kuteremka na kisha kumchukua na kuondoka nae kwa ajili ya kuanza maisha ndani ya nyumba yake. Bado kila kilichokuwa kikitokea kwa wakati huo kilizidi kuonekana kama ndoto fulani ambayo baada ya muda fulani angeamka na kujikuta pale pale pa kila siku, kwenye godoro lililochoka.
Kila kilichokuwa kikiendelea hakikuwa ndoto, kilikuwa ni kitu halisi ambacho kilikuwa kikiendelea kufanyika katika ulimwengu halisi. Ndani ya gari, Rose alitamani kulia, hakuamini kama leo hiyo alikuwa akienda kuishi na mchina, mchina ambaye alionyesha kwamba alikuwa na mapenzi ya dhati kwake.
Baada ya kufika nyumbani, hapo ndipo Rose alipoanza kufanya kazi zake. Kila kitu ambacho alikuwa akikifanya hakikuwa kikubwa sana na mara nyingi kazi zake wala hazikuwa kubwa kama alivyokuwa akifikiria kabla. Kama kufua, kulikuwa na mashine za kufulia, kama kupiga deki, kulikuwa na vifaa maalumu ambavyo vingemfanya kutokuinamana na kuuchosha mgongo wake.
Maisha yake nyumbani hapo yakaonekana kuwa mazuri, kila siku Bi Lucy alikuwa akipenda kukaa karibu na Rose huku akitamani sana kuisikia historia ya maisha yake ambayo ilimfanya kuwa mahali pale. Kwa Rose, wala hakutaka kumficha Bi Lucy, akajaribu kumwelezea kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea katika maisha yake, hakuficha kitu, hata suala la usagaji alikuwa amelizungumzia kwa ukaribu sana.
Ile ikaonekana kuwa stori mbaya ambayo ilimuumiza hata Bi Lucy mwenyewe, hakuamini kama kulikuwa na mwanamke ambaye alikuwa na umri wake ambaye alipitia katika matatizo kama yale. Japokuwa alikuwa amesahau mengi lakini Bi Lucy alikuwa akimfariji kila siku, faraja ambazo zilimfanya Rose kuwa imara zaidi na zaidi.
Mara kwa mara, Lee ndiye ambaye alikuwa akicheza sana na Lydia, Lee akaonekana kuvutiwa sana na Lydia huku akipenda kumbeba na kwenda nae huku na kule japokuwa alikuwa na miaka mitatu na nusu tu. Wote kwa pamoja wakaungana na kuwa kama familia moja, Rose hakuchukuliwa kama mfanyakazi ndani ya nyumba hiyo, alichukuliwa kama mmoja wa familia hiyo.
“Kuna vitu ambavyo vitatakiwa kufanyika. Unaonaje kama baadae tukaenda kufanya manunuzi ya nguo?” Bi Lucy alimuuliza Rose.
“Hakuna tatizo” Rose alijibu.
Hayo ndio yalikuwa maisha ambayo walikuwa wakiishi, Rose akaonekana kuridhika na kuvutia zaidi mpaka kuwa zaidi ya uzuri ambao alikuwa nao katika kipindi cha nyuma.      Muonekano wake ukawavutia vijana mbalimbali waliokuwa wakifika mahali hapo lakini kwa Rose wala hakuonekana kujali kabisa.

Mwaka wa kwanza ukapita, bado Rose alikuwa ndani ya nyumba hiyo, mwaka wa pili ukapita mpaka mwaka wa tano kuingia. Hakukuwa na kitu ambacho alikuwa akikikumbuka nyuma zaidi ya kumkumbuka Bi Fatuma ambaye alikuwa akiwasiliana nae sana pamoja na Joshua ambaye toka aondoke nyumbani hakuwa amewasiliana nae tena.
Katika miaka mitano, Lydia alikuwa amekua sana na hivyo kuwa mmoja wa wanafunzi katika shule ya St Marry ambayo alikuwa akisoma pamoja na Lee. Ukaribu wao ulikuwa mkubwa kila siku, walimu walikuwa wakiwashangaa huku mara kwa mara wakihoji maswali lakini hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akifahamu kile ambacho kilikuwa kikiendelea kwa watoto hawa.
Katika vichwa vyao, Lee alionekana kuwa tofauti sana, alikuwa na akili nyingi kupita kawaida. Katika umri wa miaka nane ambao alikuwa nao alipitishwa madarasa mawili lakini bado huko alikuwa kichwa zaidi ya wanafunzi wote. Ni kweli alikuwa mtundu lakini pamoja na utundu wake huo, alikuwa akipenda sana kukaa na kompyuta mapajani mwake japokuwa hakuwa akijua ni kitu gani ambacho alikuwa akitakiwa kukifanya.
Lyidia hakuwa na akili sana kama ilivyokuwa kwa Lee lakini mara nyingi Lydia alionekana kuwa mtoto mpole ambaye hakupenda kuongea na watoto wengi shuleni pale. Katika siku za kwanza walimu walifikiri kwamba Lydia alikuwa mgonjwa lakini mara baada ya kumsoea, wakagundua kwamba ile ndio ilikuwa asili yake.
Watoto wawili wenye tabia tofauti wakawa wakiishi pamoja, Lee alikuwa mtundu na muongeaji sana ila kwa Lydia alikuwa mpole na mkimya sana. Lee hakupenda kumuona Lydia akiwa katika hali hiyo, kila siku alikuwa akitaka kumuona Lydia kiwa muongeaji kama yeye lakini Lydia hakuonekana kubadilika kabisa, bado alikuwa akiendelea kuwa kimya na mpole sana.

 

JE, nini kitaendelea?
Tukutane kesho hapahapa.

Leave A Reply