The House of Favourite Newspapers

Mnyarwanda wa Singida United Awateka Mashabiki

0

 

Straika wa Singida United, Mnyarwanda, Danny.

STRAIKA wa Singida United, Mnyarwanda, Danny Usengimana, ameonekana kuwateka mashabiki wa soka mkoani hapa kutokana na uwezo mkubwa wa kufunga mabao aliokuwa nao.

Usengimana ambaye amesajiliwa na Singida United kwa mkataba wa miaka miwili akitokea timu ya Polisi ya nyumbani kwao, Jumatatu ya wiki hii alifunga mabao mawili kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Pamba FC katika ushindi wa mabao 5-0 uliopigwa kwenye Uwanja wa Nyamagana.

Kabla ya kutua Singida United, Usengimana aliibuka Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Rwanda misimu miwili mfululizo, ambapo msimu uliopita alifanikiwa kutupia kambani jumla ya mabao 19 akiwa na timu yake ya Polisi.

Katika mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika jana Alhamisi asubuhi kwenye Uwanja wa Nyamagana ambapo Championi lilikuwepo, Usengimana alikuwa akizungumzwa na mashabiki wa soka waliokuwa wakishuhudia mazoezi hayo huku wengine wakisema akionekana na Simba na Yanga, lazima wamchukue.

“Jamaa anajua sana kufunga, hapa Singida wamepata mchezaji, naamini atafanya vizuri katika ligi na kupambana na hao washambuliaji wa Simba na Yanga ambao kila msimu wanaonekana kuwa juu katika orodha ya wafungaji, wasipoangalia huyu mchezaji anaweza kuondoka muda si mrefu endapo Simba na Yanga zitamuona,” alisema mmoja wa mashabiki hao.

Hata hivyo, gazeti hili likataka kujua mipango yake mwenyewe Usengimana katika msimu ujao, ambapo alisema kwa kifupi kuwa: “Mimi siyo msemaji, ngoja ligi ianze watu wataniona uwanjani.”

(Stori: Omary Mdose | Championi Ijumaa)

Leave A Reply