The House of Favourite Newspapers

Kajala: Tunazeeka, hakuna tulichofanya

0

Kajala-Masanja-5331 Kajala Masanja

NA IMELDA MTEMA, RISASI Mchanganyiko

MMOJA kati waigizaji waliofanikiwa kutengeneza jina katika Bongo Muvi ni Kajala Masanja ambaye kwa mujibu wake mwenyewe, aliingia kwenye tasnia hiyo baada ya kuvutiwa na mkongwe Issa Mussa ‘Cloud 112’ miaka kadhaa iliyopita.

Staa huyo, ambaye wiki iliyopita alizindua filamu yake mpya iitwayo Sikitu, katika mahojiano maalum na gazeti hili, alikiri kuwa umri wake umekwenda na bahati mbaya, hakuna chochote cha maana alichokifanya katika fani hiyo inayosuasua.

kajalaAlisema kuna uzembe ulifanyika mwanzo, kipindi wanaingia kwenye filamu kiasi ambacho kwa hivi sasa tamthiliya zimeanza kupoteza mvuto kwa watu na hata wasambazaji.

Risasi: Kwa nini unasema kuwa uzee umekaribia na hakuna kilichofanyika kwenye filamu?

Kajala: Mimi naona hivyo kabisa, kwa sababu siku zinavyozidi kwenda hata mvuto wa kucheza kama mwanamke mrembo unapotea.

Risasi: Kwa nini unasema hivyo?

Kajala: Sababu huko nyuma kulikuwa na wapenzi wengi wa filamu zetu, tulikuwa tunapendwa sana.

Risasi: Unafikiri kwa nini zamani mlipendwa na hivi sasa hampendwi?

Kajala: Najua tatizo lililokuwepo, maana zamani alikuwepo Kanumba (Steven) na alikuwa akicheza filamu nzuri sana, kila mtu alikuwa akizipenda sasa wasanii wengi walikuwa wakijitahidi ili kuwa kama yeye, hivyo kulikuwa na filamu nyingi nzuri.

Risasi: Kwa hiyo ndiyo tunarudi kwenye ule usemi kuwa Kanumba kaondoka na Bongo Muvi yake?

Kajala: Ni kweli kabisa na ndivyo ilivyo maana hata mimi nilianza kuwika kipindi hicho nilichocheza naye filamu kama tatu hivi.

Risasi: Kwa hiyo unataka kuniambia kuwa hakuna mafanikio ya moja kwa moja uliyoyapata kutoka kwenye filamu?

Kajala: Maendeleo ni yaleyale ya kujulikana zaidi kwa sababu kuna tatizo kubwa kwenye filamu, hasa uhaba wa wasambazaji, msanii analazimika kusubiri malipo yake zaidi ya mwaka mmoja kwa filamu moja tu, maendeleo yanatoka wapi sasa!

Risasi: Mara nyingi watu wanapokuona unatoka na mtoto wako sehemu mbalimbali za starehe,

 wanakuchukulia tofauti labda unamfundisha mtoto vibaya, unazungumziaje hilo?

Kajala: Paula ni mtoto wangu, kuna wakati nampa uhuru kidogo wa kufurahi na mimi, lakini najua maadili ya kumfundisha mtoto na yeye anaelewa sana na ananiogopa pia, si wa kufanya ujinga mbele yangu.

Risasi: Vipi huna mpango wa kuongeza mtoto?

Kajala: Natamani sana ila nafikiri Mungu bado hajanipangia, ila naamini nitaongeza mmoja.

Risasi: Mwanao sasa amekua mkubwa, vipi unawezaje kujizua ili asiweze kuujua undani wako hasa katika uhusiano?

Kajala: Mimi nakuwa na mipaka yangu na mtoto na pia, siwezi kumleta mtu wangu nyumbani yeye akiwepo, kama aliwahi kumjua mmoja basi ndiyo huyohuyo.

Risasi: Vipi kuhusu suala la kuolewa tena maana bado umri unaruhusu?

Kajala: Unajua mimi nilifunga ndoa ya kanisani na mume wangu Faraji Augustino, nitasubiri.

Risasi: Mbona kuna tetesi kuwa siku hizi hata huendi gerezani kumsalimia.

Kajala: Ndiyo maana nakuambia kuwa ukisikiliza maneno ya watu wanapotosha, kwa nini nisiende kumuangalia na siyo mimi tu, mpaka familia yangu pia.

Risasi: Kuna ishu pia hii ya kutoka kimapenzi na Diamond, unazungumziaje?

Kajala: Unajua watu wanaweza kuzungumza kila jambo kuhusu wewe, lakini kikubwa kila mmoja ukweli anaujua kwenye moyo wake tu na si vinginevyo.

Leave A Reply