The House of Favourite Newspapers

Kajala umepaa angalia usianguke

0

KWAKO mwigizaji Kajala Masanja. Mambo vipi dada yangu, kitambo kidogo hatujaonana. Vipi mishemishe zinakwenda kama kawaida?Binafsi namshukuru Mungu naendelea vizuri. Kazi zinakwenda kama kawaida, tunapambana kuhakikisha tunatimiza wajibu wetu kama waandishi katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

imekukumbuka leo kwa barua maana wakati mwingine najua kutokana na majukumu, ni nadra sana kuonana. Lakini naamini kupitia barua hii, ujumbe wangu utakufikia.Dhumuni la barua hii, mbali na kukusalimu, ninataka kukumbusha juu ya kutambua umuhimu wa kujifunza kupitia mapitio yako. Kujua kwamba kuna leo na kesho. Kutambua ili uweze kufanikiwa, unapaswa kuwekeza katika miradi.

Uwe na vyanzo vingi vya fedha. Huwezi kuwa mtu wa matanuzi kila siku pasipo kuwa na vyanzo endelevu vya mapato.Mwishoni mwa wiki iliyopita, niliona jeuri yako kupitia moja ya magazeti Pendwa. Uliripotiwa kuhamia maeneo ya Mwenge jijini Dar. Katika mjengo wako mpya, kuna vitu vingi vya thamani. Hongera sana maana mtoto wa kike unalindwa na walinzi maalum, una wafanyakazi wa ndani watatu, si mchezo!

Mazagazaga ya ndani hayaelezeki. Mavazi, viatu na samani za ndani ni za gharama kubwa. Na hapo ndipo kwenye msingi wa kukuandikia barua hii. Dada yangu sikia, haijalishi umepata hizo fedha kwa njia gani lakini nikushauri sasa, usibweteke. Huu ni wakati wa wewe kushtuka na kutumia fursa hiyo vizuri.

Huu si muda wa kuonesha jeuri kwa mashosti zako kwa kuzungusha ‘raundi’ za vinyaji. Huu siyo wakati wa kumwaga fedha katika majumba ya starehe eti unawatuza wanamuziki. Usiwe mtu wa kupoteza mamilioni saluni wakati pato lako haliendani.

Wekeza kwenye miradi kwani tumeona mifano mingi ya wasanii wenzako ambao walionesha mbwembwe za aina hiyo halafu wakashindwa kudumu katika maisha hayo. Wanarudi katika maisha ya kawaida, wanafedheheka.

Miaka kadhaa iliyopita ulikuwa unaishi nyumbani pale Oysterbay jijini Dar. Ulikuwa kwa baba na mama. Angalau sasa umepiga hatua, unaishi kwako. Usikubali kurudi nyuma. Tatizo kubwa la wasanii wengi Bongo wanajisahau sana katika eneo la matumizi. Wanapenda kuvaa vitu ambavyo wakati mwingine haviendani na kipato chao. Wanalazimisha kuendesha magari ya kifahari wakati kiuhalisia hawana uwezo nayo. Hapo ndipo wengi wenu mnapopita njia zisizo sahihi ilimradi muende sawa na fasheni.

Usiwe miongoni mwa wasanii hao. Hadi kufikia hatua hiyo ina maana si haba, fedha ipo. Itengenezee mianya mingi ya kuzalisha ili kesho tusije kukushuhudia ukirudi kule kwenye kuungaunga tunakoishi sisi.
Ni matumaini yangu utakuwa umenisoma, nikutakie maisha mema na mafanikio zaidi.
Mimi ni ndugu yako,

………
Erick Evarist

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

Leave A Reply