The House of Favourite Newspapers

Kama Haoni Umuhimu Wako, Muombee Aishi Miaka Mingi!

0

JUMAMOSI nyingine Mungu ametukutanisha. Kama ilivyo kawaida, hapa huwa tunajadili mambo mbalimbali yahusuyo masuala ya mahusiano. Ili uweze kuishi vizuri, binadamu unahitaji mahusiano mazuri na binadamu wenzako.  Iwe ni rafiki wa kawaida na hata mchumba wako, mnapokuwa kwenye mahusiano mazuri ndipo utakapoona raha ya dunia. Tofauti na hapo, dunia utaiona chungu. Kuishi kwenye mahusiano mabaya siku zote ni matokeo.

Hakuna ambaye anapenda kuwa kwenye mahusiano mabaya, bali hutokea tu. Yawezekana mtu akawa ni mwema, mwenye tabia njema, lakini mwisho wa siku anajikuta kwenye mikono isiyo salama. Kila unalofanya kwako haliwi jema.

Hapo ndipo unapoyachukia mapenzi. Unajiuliza wenzako wanaishije? Wanawezaje kuyafurahia maisha ya mahusiano? Kwa nini wewe kila siku ni matatizo? Ndugu yangu usikate tamaa, maisha ya mahusiano ndivyo yalivyo.

Yawezekana ukakosea leo, kesho utakutana na mahusiano salama. Utasahau kabisa hayo mateso ambayo umewahi kuyapitia kabla. Utasahau kabisa, mambo mabaya yote yaliyopita kwenye maisha yako, yatabaki kuwa historia.

Hapa ndipo kwenye msingi wa mada yangu ya leo. Watu sasa hivi wanateswa sana na masuala ya mahusiano. Kinachowasumbua zaidi watu ni kushindwa kuendana kitabia pamoja na suala zima la tamaa.

Watu wanatamani maisha fulani kwenye mahusiano, wasipoyapata basi wanahangaika kuyapata mahali pengine. Unakuta mtu ana mahusiano huku na huku. Ana mtu huyu na anaye mwingine. Hii ni kutokana na kwamba, hawaridhiki.

Anaishi kwa kupima upepo. Anajaribu kuangalia wapi ni pazuri zaidi. Anajikuta yupo njia panda katika mahusiano yake na kujikuta akishindwa kuishi kwenye msimamo mzuri wa mahusiano. Watu wa aina hii hujikuta wameambulia maumivu kwa kukosa bara na pwani.

Marafiki, hakuna kitu kizuri kwenye mahusiano kama kuridhika. Wapo watu wanakutana na watu sahihi kabisa maishani mwao lakini kutokana na tamaa zao, wanajikuta wamewapoteza na matokeo yake wanajikuta kwenye majuto makali.

Wanajilaumu kwamba pengine wasingefanya makosa ya kuendekeza tamaa, walikuwa kwenye njia sahihi. Ulikuwa na mtu sahihi, amejaribu kufanya kila linalowezekana kukufanya uwe kwake lakini wewe wapi unaondoka.

Mtu anayeondoka kwa staili hii ndiye ambaye nasema, huna sababu ya kugombana naye. Wewe muache aende na zaidi ya yote muombee aishi maisha marefu. Ili wewe utakapokutana na mtu sahihi ambaye ataitambua thamani yako, awe shuhuda wa hilo.

Sina maana kwamba umlaani, hapana lakini kitendo cha kushuhudia wewe unaishi vizuri katika mahusiano yako mapya kitampa somo la maisha. Atajifunza na kuelewa kwamba maisha hayapaswi kuyachukulia poa. Unaposhikwa shikana.

Furaha ya mahusiano ni kukutana na mtu ambaye anakujali, anakupenda, anakuthamini na anayejua umuhimu wako. Mengine yote ni furaha za muda mfupi. Starehe za muda mfupi zisikutoe ufahamu na kujikuta kwenye majuto makali huko baadaye.

Uliyenaye ni bora kuliko yule unayetaka kwenda kuwa naye. Uliyenaye ni rahisi zaidi kumrekebisha sababu mnajuana kuliko yule usiyemjua, atakusumbua zaidi. Mheshimu mtu anayekuheshimu, mpende anayekupenda na umthamini mtu anayekuthamini. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine. Unaweza kunifuata kwenye kurasa zangu kwenye mitandao ya kijamii; Instagram & Facebook: Erick Evarist, Twitter: ENangale.

Leave A Reply