The House of Favourite Newspapers

Kama kweli unahitaji mafanikio, kuwa wa kipekee!

0

Na AMRAN KAIMA| GAZETI LA IJUMAA| MAISHA, SAIKOLOJIA NA WEWE

MAFANIKIO ni kitu muhimu kwani kila binadamu anahitaji kuyapata kwa udi na uvumba lakini kwangu mafanikio naweza kusema ni matokeo chanya ambayo mtu anayapata kutokana na kutimiza ndoto au malengo aliyojiwekea. Wapo watu wengi sana ambao wanatamani kuingia katika ulimwengu wa mafanikio na pengine kuwa matajiri wakubwa.

Lakini ndoto zao hizo huishia kuwa ndoto za alinacha kwani hutawaliwa zaidi na maneno kuliko matendo ya namna ya kuzitimiza. Ukweli uko hivi; unapohitaji kuingia katika ulimwengu wa watu waliofanikiwa ni lazima ujue namna ya kujitofautisha na wengine.

Sina maana ujitofautishe na wengine kwa kuwadharau ama kutoshirikiana nao katika mambo mbalimbali, simaanishi hivyo. Ninachozungumzia hapa ni ile namna ya kufanya mambo kwa utofauti na uweledi wa hali ya juu. Mnaweza watu kumi mkawa mnafanya biashara moja inayofanana katika mtaa wenu lakini ukashangaa mmoja wenu anapata wateja wengi.

Kwa imani mbovu zilizojengeka kwa baadhi ya watu, wapo watakaosema mtu huyo anatumia ndumba katika biashara yake. Matokeo yake na wewe unaanza kutumia pesa zako kwenda kwa waganga ili biashara yako ichanganye.

Lakini kumbe inawezekana yule anayefanya vizuri kwenye biashara yake kushinda nyie wala hajaenda kwa mganga, alichokifanya ni kujitofautisha na nyie. Yawezekana ana nidhamu zaidi kuliko wengine, muaminifu na mbunifu na uchangamfu katika biashara yake.

Kwani nani asiyejua kuwa nidhamu ni msingi wa kuelekea katika ujenzi wa nyumba ya mafanikio? Wapo watu wanaharibikiwa mambo yao kila kukicha kutokana na kutokuwa na nidhamu. Pengine ni wanafunzi, wafanyakazi au wafanyabiashara na wanashindwa kuwa makini na kitu kinachoitwa utiifu na kujishusha.

Eti wao kwao kujishusha ni ishara ya unyonge!! Sasa wewe hupaswi kuwa miongoni mwao. Ninachokushauri ni kuwa mtiifu, jishushe, omba msamaha inapobidi na uwe makini hata katika matamshi yako. Vilevile ni lazima ujitofautishe na wengine katika uaminifu wako.

Kwanza unapaswa kujijengea uaminifu wewe mwenyewe kabla ya wengine kukuamini. Yakupasa kujiamini wewe kama wewe ya kuwa unaweza na hakuna yeyote anayeweza kukuzuia katika imani yako hiyo. Pia ni lazima ujijengee uaminifu miongoni mwa watu wanaokuzunguka, kwani kwa kufanya hivyo utakuwa unajijengea mtaji mkubwa. Kumbuka uaminifu ni mtaji hivyo ni lazima uwe mwaminifu, iwe ni katika biashara, kwenye jamii ama ofisini kwako. Kama wewe ni mfanyabiashara epuka kuambiwa;

“Mmmh! Yule jamaa mafuta yake anapunja sana’ au ‘Aaah! Yule maziwa yake siyo mazuri, huwa anachanganya na maji.’ Ni lazima kujijengea uaminifu miongoni mwa watu au katika jamii inayokuzunguka ili kuwa tofauti na wengine.

Lakini jitofautishe na wengine hata katika ubunifu. Kama nilivyosema kuwa kuna watu wanaofanya biashara moja inayofanana katika mtaa mmoja hata watu kumi lakini lazima atakuwepo ambaye ana wateja wengi. Mfano, katika mtaa ninaoishi mimi wapo akina mama kama sita wanaofanya biashara ya kuuza chakula (Mama n’tilie), lakini kuna mama mmoja ambaye huwa anapata wateja wengi sana na kuwahi kumaliza biashara yake kila siku kabla ya wengine.

Nilijiuliza maswali mengi juu ya mama huyo, ila nilichoamua ni kwenda kula kwa wote kwa siku tofauti ili niweze kujua siri iliyojifi cha hasa kwa yule mama mwenye wateja wengi. Kweli baada ya utafi ti wangu huo mfupi, niligundua kuwa kumbe yule mama mwenye wateja wengi huwa anaweka maji ya kunywa ya bure tena yaliyochemshwa tofauti na wengine ambao wao huuza maji ya kunywa tena yasiyochemshwa!!

Kumbe tunapaswa kutambua kuwa ubunifu ni kitu muhimu sana katika kila jambo tunalofanya. Iwe ofi sini au hata katika biashara zetu.
Shinda Nyumba; Washindi wa Pikipiki, Televisheni, Simu Walivyokabidhiwa

Leave A Reply