The House of Favourite Newspapers

Kamanda OFM avamiwa na vibaka

1

shekideleKamanda wa Oparesheni Fichua Maovu (OFM) ya Global Publishers, Mkoa wa Morogoro, Dustan Shekidele.

Mwandishi wetu, Moro
Hii si sawa! Kamanda wa Oparesheni Fichua Maovu (OFM) ya Global Publishers, Mkoa wa Morogoro, Dustan Shekidele amevamiwa na vibaka kisha kuporwa kamera na simu alipokuwa akiwatetea wananchi waliovamiwa na vibaka hao katika Mkesha wa Mwaka Mpya.

Awali kamanda huyo alikuwa kwenye Mkesha wa Mwaka Mpya katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mji Mpya, alipotoka majira ya saa 6:00 usiku ndipo akapigiwa simu na akina mama waliokuwa wakilalamika kuporwa simu na mabegi yao na kundi la vibaka eneo Mwembesongo, Mti-Mkubwa.

Kamanda huyo alifika eneo hilo na kushuhudia matairi kadhaa yakiteketea kwa moto barabarani huku akina mama walioporwa vitu vyao wakiangua vilio.

Alipofika eneo hilo, bila kuchelewa, alianza kutekeleza majukumu yake ambapo alitoa kamera na kuanza kuwapiga picha akina mama hao kabla ya kufanya nao mahojiano.
Katika hali ya kushangaza, mara tu baada ya kuonekana kwa mwanga wa kamera, ghafla walitokea vibaka wawili upande wa nyuma wa kamanda wetu kisha kumpora kamera na simu na kutoweka.

Akihojiwa na gazeti hili, kamanda huyo wa OFM alisimulia: “Nilipofika eneo la tukio nilikuta watu wachache wakiwafariji akina mama hao ambao walikuwa wakimpeleka mgonjwa hospitalini usiku huo.

“Wakati nawapiga picha akina mama hao, vibaka wawili walitokea nyuma yangu na kunipora kamera na simu, nilishindwa kuwamudu kwa sababu walinizidi nguvu kwani kulikuwa na wenzao wengine hivyo wangechukua pikipiki yangu.”

Baada ya matukio hayo, majira ya saa 8:00 usiku, polisi walifika eneo la tukio na gari la maji ya washawasha na kuwatawanya watu waliokuwa eneo hilo.

Siku iliyofuata (Ijumaa), kamanda huyo alitinga eneo hilo la tukio ambapo kijana mmoja aliyekuwepo eneo la tukio alisema:

”Nilishuhudia akina mama walivyoporwa vitu vyao na wewe ulivyoporwa kamera yako, nimeamua kutoa ushirikiano kwako na niko tayari hata kutoa ushahidi polisi na mahakamani kwa kuwa wewe ulifika kutekeleza majukumu yako.

“Waliokupora ni wale vijana wa kundi la Kizazi Jeuri wanakaa Mji Mpya, jirani na stendi ya daladala.”

Baada ya kupewa maelezo hayo, kamanda huyo alifika katika eneo hilo na kuwakuta vibaka wanne ambapo walipomuona tu walianza kumwambia:
“Pole sana, jana tumeshuhudia ukiporwa kamera lakini usiogope waliochukua tunawajua kama vipi njoo kesho (juzi) tutakupa jibu.”

Kesho yake, Jumamosi, mwandishi wetu alifika eneo hilo na katika hali ya kushangaza bosi wa vijana hao aliyetajwa kwa jina la Kibua Adam alikuja juu akipinga vijana wake kupora kamera.

Baada ya kukumbana na kashikashi hiyo, kamanda huyo alikwenda kuripoti kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul ambapo vibaka hao wanasakwa.

1 Comment
  1. Msomi says

    Duh! Hata kiongozi wa ‘vibaka’ anajulikana kabisa na yuko tayari kutetea ‘vibaka’ wake?

Leave A Reply