The House of Favourite Newspapers

OFM Yanasa Siri Bifu la Wema, Batuli

0

UNAJUA bifu la msanii Wema Sepetu na Yobnesh Yusuph Hassan ‘Batuli’, lililoteka mitandao ya kijamii mwishoni mwa wiki iliyopita, limetokana na nini; tulia upewe siri.

 

Kikosi kazi cha Oparesheni Fichua Maovu cha Global ‘OFM’ kimechimba chanzo cha ugomvi wa mastaa hao, wanaoshiriki kampeni za Chama Cha Mapinduzi ‘CCM’ na kuelezwa kuwa, Batuli ni mchokozi.

 

“Wasanii hasa wa Bongo Muvi, wameshirikishwa kwenye kampeni za CCM kwa kugawanywa kwenye makundi mawili.

 

“Kundi la kwanza linaitwa Mama Ongea na Mwanao, ambalo yupo Wema na wasanii wengine na lingine linaitwa Mafanikio, hili yumo Batuli na chokochoko zote zimeanzia hapa,” chanzo chetu kilisema.

 

UTAMU UKO HAPA

Fukuafukua ya OFM kwenye bifu hilo, inaonesha kuwa Batuli amekuwa na mtazamo hasi na wasanii wanaounda kundi la Mama Ongea na Mwanao, huku akivikwa ubaya kuwa ametumbukia nyongo kwa yeye kutokuwepo kwenye kundi hilo.

 

Inaelezwa kuwa, kabla ya kumtupia Wema kijembe kupitia sanamu ya mifupa ya binadamu iliyotafsiriwa na wengi kuwa alikuwa anamsema Wema kwa jinsi alivyokonda, alimkera kwanza kiongozi wa kundi la Mama Ongea na Mwanao, Steve Nyerere kwa kumpa maneno ya shombo.

 

“Alianza kugombana na Steve, alipotoka kwake kahamia kwa Wema, huyu dada ana matatizo sana.

“Kama hilo halitoshi, mara nyingi amekuwa anasema kundi letu limejaa wadangaji, sisi tumebaki kumtazama tu,” alisema mmoja wa wasanii kutoka kundi la Mama Ongea na Mwanao ambaye hakupenda kutajwa jina lake.

 

Aidha, OFM katika kuchunguza kwake, imebainika kuwa wasanii wanaounda kundi la Mama Ongea na Mwanao, ni ‘watu na nusu’ tofauti na wale wa Mafanikio, ambalo kiongozi wake ni Halima Yahya ‘Davina.’

 

Inasemwasemwa kwamba, uwepo wa Batuli kwenye kundi hilo, huwenda unamfanya ajione kama kashushwa hadhi na kwamba angependa awe sambamba na mastaa wenye majina makubwa Bongo, ambao inasemekana wanatunzwa vizuri.

 

SA’ ITAKUWAJE? Kifuatacho kwenye ugomvi huo hakijulikani, lakini tayari Wema amemfananisha Batuli na “mchawi” huku akimtolea povu kuwa anatafuta kiki za kijinga kupitia jina lake.

 

“Yaani ananikera sana, hana lolote anatafuta umaarufu kupitia mimi,” alisema Wema alipozungumza na mwandishi wetu kwa njia ya simu. Batuli alipotafutwa ili naye azungumze alianzaje kuposti picha ya mifupa ya binadamu na kuzua zogo mitandaoni, hakuweza kupokea simu kila alipopigiwa. Hata hivyo, baadhi ya watu wamewataka wasanii hao kuacha bifu na kujikita katika kukisaidia chama ambacho kimewapa nafasi ya kukifanyia kampeni.

 

“Hata kama wanalipwa kidogo, lakini kuaminiwa na CCM ni heshima, wanatakiwa kujitambua, waache utoto na mambo ya kijinga,” aliandika komenti mchangiaji mmoja kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram.

STORI MEMORISE RICHARD, Risasi

Leave A Reply