The House of Favourite Newspapers

Kamwe Usifosi Penzi, Lazima Utaumia Tu!

0

KATIKA pitapita zangu, nilikutana na dada ambaye alinisimulia mengi kuhusu penzi lake.Alinieleza jinsi anavyotatizika na maisha ya mapenzi na kwamba anaishi na mwanaume kwa sababu hana kazi.

Pia ni kwa sababu mwanaume huyo, ndiye anayemtimizia mahitaji yake yote.

Alinidokeza zaidi kwamba kama atapata kazi na kuweza kujikimu kimaisha, basi nia yake ni kuondoka na kuanza maisha yake binafsi.

 

Nilipomuuliza ameishi kwenye hali hiyo kwa muda gani, akanieleza kuwa ni zaidi ya miaka mitano ambayo amekuwa na mwanaume huyo.Akanieleza zaidi kwamba mwanaume huyo ana tabia zilizopinda na amekuwa anamnyanyasa na kumtesa, lakini imebidi aishi naye kwa sababu ya uwezo wake kimaisha.

 

Jambo kubwa zaidi ya yote, huyu dada akanieleza kwamba hampendi mwanaume huyo na wala hana tena mvuto naye hata chembe.Katika maelezo yote aliyonipa, tathmini yangu ya awali ni kwamba, dada huyu anaishi katika utumwa wa mapenzi.

Kwamba anaishi na mwanaume, hana mapenzi naye, lakini anafosi tu aendelee kuishi naye kwa sababu ya maslahi binafsi.

Unakuta mwanamke anaamua kuwa na mwanaume fulani ingawa anajua wazi kwamba hampendi, lakini kwa sababu jamaa ameonesha mapenzi kwake na anajua wazi anampenda, basi anakubali kwa sababu ya kupata kitu.Wapo wanaokuwa na uhusiano na wapenzi ambao hawana kabisa mapenzi nao.

 

Wanalazimika kuwa nao kwa sababu mbalimbali, mojawapo ikiwa ni kupenda kupita kiasi huku wakitumia ushawishi wa kila aina ili nao wapendwe.Wanafanya hivyo kwa sababu wanafahamu wazi kwamba hawapendwi.

 

Wakati mwingine ni kutokana na shinikizo la ndugu, jamaa au marafiki, kumshawishi aendelee kung’ang’ania mahali kwa sababu ya maslahi au labda sababu ya kukidhi matakwa ya jamii.

 

Kama upo kwenye tafrani hii, utambue kwamba ni kazi ngumu mno kumbadilisha binadamu mwenzako, kama hakupendi mpishe na umpatie nafasi, usilazimishe mambo.Huna sababu ya kuunyima moyo wako haki ya kuwa na yule unayempenda zaidi, mapenzi hayalazimishwi.

 

Pesa, mali na anasa zote hutafutwa na hata siku moja haziwezi kununua penzi la dhati. Anza kubadilika, ondoa fikra zako mgando na uingize ufahamu mpya utakaokuweka kwenye ramani ya maisha ya kibinadamu na siyo ya kinyama kama uliyo nayo sasa.

 

Ujumbe wa leo pia ni kwa wazazi ambao wanachochea mabinti zao waishi na wanaume wasiowapenda na kuwatumia kama chanzo cha kipato. Kwani shinikizo hili husababisha watoto kujikuta wakiishi katika ndoa ambazo zinafanana na gereza la mapenzi.Siku zote, maji yakishamwagika hayazoleki.

 

Kwa wale ambao tayari wameshafunga ndoa, inakuwa ni vigumu kuvunja muunganiko huo hivyo wanajikuta wakiendelea kuteseka badala ya kufurahia maisha ya ndoa au uhusiano wa mapenzi.Na hali hii ikiendelea kwa muda mrefu, ndipo mmoja anaweza kuamua kutafuta pumziko nje ya ndoa yake na matokeo yake yakawa ni mshikemshike.

 

Kama ni mzazi, mpatie nafasi mwanao ya kumchagua yule anayemtaka, akiwa ni mwenye pesa ni sawa na akiwa ni kuli mbeba mizigo bandarini, pia ni sawa. Nafasi yako kama mzazi ni kumshauri mwanao kama utaona anakuwa katika uhusiano ambao una shaka nao.

 

Kumng’ang’aniza mwanao kuwa katika uhusiano ambao yeye haupendi, ni kumharibia maisha yake, maana badala ya kufikiria maisha yake, atajikuta akifikiria jinsi alivyo katika gereza la watumwa wa mapenzi. Mpatie nafasi mwanao aishi maisha yale aliyojichagulia na siyo uliyomchagulia. Wazazi na ninyi badilikeni!Kwa leo naishia hapa, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine murua

 

Leave A Reply