The House of Favourite Newspapers

Kapombe Amvuta Simba Beki KMC

0

BEKI wa kulia wa KMC, Israel Patrick Mwenda, amefichua kwamba, amekuwa akivutiwa kwa kiasi kikubwa na uchezaji wa Shomari Kapombe wa Simba.

 

Mwenda ambaye hivi sasa anahusishwa kutakiwa na timu za Simba na Yanga, amesema tangu akiwa mdogo anachipukia kisoka, Kapombe ndiye mchezaji anayemfuatilia kwa ukaribu sana.

 

Beki huyo Jumapili iliyopita akiwa na jezi ya Taifa Stars, alifunga bao la faulo ya moja kwa moja katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Malawi ambao Taifa Stars ilishinda 2-0.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Mwenda alisema hivi sasa amekuwa akisikia taarifa za kutakiwa na timu hizo kongwe hapa nchini, lakini bado hajapokea ofa rasmi.

 

Aliongeza kwamba, hivi sasa mkataba wake na KMC unaelekea ukingoni ukitarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu, hivyo yeyote kati ya Simba au Yanga akimfuata, atajiunga nayo wakifikia makubaliano mazuri.

 

“Kapombe ndiye mchezaji ambaye namfuatilia sana, tangu mdogo nimekuwa nikimuangalia na kujifunza mengi kutoka kwake. “Kwa sasa mkataba wangu unaelekea ukingoni, unamalizika mwisho wa msimu huu, hivyo naweza kwenda popote iwe Simba au Yanga

. “Mimi si shabiki wa hizo timu, hivyo siwezi kuchagua pa kwenda kucheza, kikubwa ni makubaliano tu,” alisema Mwenda.

CAREEN OSCAR,Dar es Salaam

Leave A Reply