The House of Favourite Newspapers

Kaseja Atibua Mipango ya Simba Kagera Sugar

STORI: Musa Mateja | CHAMPIONI| Dar es Salaam

KIPA mkongwe, Juma Kaseja, amewatahadharisha Simba kwa kuwaambia kwamba wajipange kisaikolojia kabla ya kuingia uwanjani kucheza na Kagera Sugar mechi ya Ligi Kuu Bara, kesho Jumapili.

Kaseja ambaye aliwahi kuwika na Simba na Yanga kwa nyakati tofauti, anatarajiwa kukiongoza kikosi cha Kagera Sugar anachokitumikia kwa sasa kupambana na vinara hao wa ligi kuu kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera.

Kipa huyo ameliambia Championi Jumamosi kuwa, Simba wanatambua kwamba watakuwa ugenini, hivyo ni lazima wajiandae kwa hali yoyote ile kwani nao hawataki kufungwa nyumbani.

“Simba waje tu kwani tumejiandaa vizuri kupambana nao na itakuwa jambo la fedheha sana kwa mashabiki kutuona tukirudia kosa lile la Yanga, tunataka kushinda na kutibua mipango ya Simba,” alisema Kaseja.

“Wajiandae kisaikolojia kwa sababu wapo ugenini na kama ujuavyo mechi za ugenini timu nyingi zikipoteza huanza kutoa visingizio.”

Mara zote Simba imekuwa ikijitamba kuifunga Kagera Sugar ikiwa ni mmoja kati ya mipango yao ya kuelekea kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu baada ya kufanya hivyo mara ya mwisho mwaka 2012.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime alisema; “Tupo vizuri kucheza na Simba, hatuwezi kutishwa na Simba na rekodi yetu ni nzuri kwa mechi za hivi karibuni.”

Kwa upande wake, Kocha wa Simba, Joseph Omog alisema: “Ninachotaka ni ushindi ili tuwe katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa msimu huu.”

Simba ipo kileleni mwa ligi kuu ikiwa na pointi 55, Kagera ni ya nne ikiwa na pointi 42. Zote zimecheza mechi 24.

 

Subscribe kwenye YouTube Chanel yetu ya Global TV Online ili zote kali zinazotufikia iwe nisiasa, michezo, comedy, burudani, stori za mastaa, muziki na nyingine kali zikufikie kwa wakati.

Comments are closed.