The House of Favourite Newspapers

Katiba ya Tanzania Inasemaje Rais Akifariki Dunia?

0

Baada ya Rais wa Tanzania John Magufuli kufariki dunia, hakuna uchaguzi mwingine unaofanyika badala yake, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ataapishwa kuwa Rais kwa kipindi kilichosalia katika muhula wa miaka mitano.

 

Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kwa Rais kufariki akiwa madarakani, hivyo hakuna uzoefu wa nini kinafanyika katika hali kama hii.

 

 

 

 

Kwa mujibu wa kifungu cha 37 (5) cha Katiba ya nchi hiyo iliyotungwa mwaka 1977, nafasi ya urais inapokuwa wazi kwa sababu yoyote ikiwemo kifo, viongozi watatu wameorodheshwa na ni Makamu wa Rais, na endapo hatakuwepo atachukua Spika wa Bunge na kama hayupo atachukua Jaji Mkuu.

 

 

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 37 (5), baada ya Samia kuapishwa atashauriana na chama anachotoka (CCM) kisha atamteua mtu atakayekuwa makamu wa Rais. Hivyo kwa mujibu wa katiba, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan ni rais mteule wa Tanzania.

 

 

“Endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki dunia, kujiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi au kutomudu kazi zake kutokana na maradhi ya mwili au kushindwa kutekeleza kazi na shughuli za Rais, basi Makamu wa Rais ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda uliobaki katika kipindi cha miaka mitano…” inaeleza katiba ya Tanzania katika kifungu cha 37 (5).

 

 

Mama Samia atakuwa Rais wa sita wa Tanzania na wa pili kutokea upande wa Zanzibar. Rais mwengine aliyetokea Zanzibar alikuwa Rais wa awamu ya pili wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi aliyetawala kwa miaka 10 kutoka mwaka 1985 mpaka 1995.

 

 

Kwa mujibu wa kifungu hicho cha 37 (5), baada ya kula kiapo cha urais, atashauriana na chama chake cha siasa, ambacho kwa sasa ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais atapendekeza jina la mtu atakae kuwa Makamu wa Rais na uteuzi huo utathibitishwa na Bunge kwa kura zisizopungua asilimia hamsini ya wabunge wote.

 

 

Kwa mujibu wa katiba, kwa kuwa anatokea Zanzibar, Makamu wake anatakiwa kutokea upande wa Tanzania Bara. Ukomo wa madaraka pia umeelekezwa kwa mujibu wa katiba hiyo katika mazingira kama haya yanayoendelea Tanzania:

 

 

“Endapo Makamu wa Rais anashika kiti cha Rais kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 37(5) kwa kipindi kinachopungua miaka mitatu ataruhusiwa kugombea nafasi ya Rais mara mbili, lakini kama akishika kiti cha Rais kwa muda wa miaka mitatu au zaidi ataruhusiwa kugombea nafasi ya Rais mara moja tu.”

 

 

Hivyo, kwa kuwa Mama Samia ataingia madarakani ikiwa ni miezi mitano tu toka awamu ya pili ya Magufuli kuanza, ataongoza nchi kwa takribani miaka minne unusu, hivyo ataruhusiwa kugombea urais mara moja tu.

 

Katiba

37 (5) Endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki dunia, kujiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi au kutomudu kazi zake kutokana na maradhi ya mwili au kushindwa kutekeleza kazi na shughuli za Rais, basi Makamu wa Rais ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda uliobaki katika kipindi cha miaka mitano na kwa masharti yaliyoelezwa katika ibara ya 40, kisha baada ya kushauriana na chama cha siasa anachotoka Rais atapendekeza jina la mtu atakayekuwa Makamu wa Rais na uteuzi huo utathibitishwa na Bunge kwa kura zisizopungua asilimia hamsini ya Wabunge wote.

 

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli amefariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa akipatiwa matibabu.

 

 

Taarifa za kifo cha Rais Magufuli, zilitangazwa jana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ametangaza kifo akisema Magufuli alifariki dunia saa 12 jioni kwa maradhi ya moyo baada ya kulazwa katika hospitali hiyo tangu Machi 6.

 

Leave A Reply