The House of Favourite Newspapers

Katumbi Agoma Kumuuza Samatta Ubelgiji, Huenda Akabaki TP Mazembe

0

samattaMbwana Samatta

IKIWA tayari Ubalozi wa Ubelgiji nchini Tanzania umekwishatoa viza kwa mshambuliaji Mbwana Samatta kwenda kusaini klabu ya KRC Genk, lakini taarifa zinasemekana kuwa huenda anaweza akabaki TP Mazembe ya DRC kumalizia Mkataba wake hadi Aprili.

Hiyo inatokana na Rais wa Mazembe, Moise Katumbi kugoma kumuuza Mwanasoka huyo Bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani katika klabu hiyo Ligi Kuu ya Ubelgiji.

katumbiRais wa Klabu ya TP Mazembe, Katumbi Moise.

Inasemekana pia kuwa, Katumbi anataka Samatta anende kucheza Nantes FC ya Ligi Kuu ya Ufaransa, ambayo amekwishafikia makubaliano nayo, na kwamba wiki iliyopita Nantes FC ilituma mwakilishi wake jijini Dar es Salaam, ambaye alifanya mazungumzo na Meneja wa Samatta, Jamal Kisongo mbele ya Ofisa mmoja wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Katika mazungumzo, Kisongo alifikia makubaliano ya maslahi binafsi na Samatta ikiwemo dau la kusaini, mshahara, masharti na marupurupu mengine. Kisongo alitaka kiwepo kipengele cha mchezaji kutorejeshwa Afrika iwapo hatapata nafasi ya kucheza Nantes, bali auzwe klabu nyingine ya Ulaya na ikakubaliwa.

samattasSamatta hivi karibuni akikabidhi jezi yake kwa rais Mstaafu, Dk Jakaya Kikwete wakati Waziri wa Habari, Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mh. Nape Nnauye akishuhudia tukio hilo. 

Nantes ilionesha nia ya dhati kabisa ya kumchukua Samatta na Kisongo aliinuka kwenye meza ya mazungumzo akiwa amekubali na kusema anakwenda kuzungumza na mchezaji. Hata hivyo, inaonekana Samatta mwenyewe ndiye anayetaka kwenda Ubelgiji na si Ufaransa, kwani kitendo cha Kisongo kutorejesha majibu kwa Nantes kinaashiria ameshindwa kumshawishi mchezaji wake akubali ofa hiyo.

Wakati huo huo, Rais wa Mazembe hayuko tayari kumuuza Samatta Ubelgiji na yuko tayari kuona Samatta anabaki Mazembe kumalizia Mkataba wake ili aondoke kama mchezaji huru Aprili, hali ambayo itamlazimu kusubiri hadi Agosti kusaini Genk.

Kwa sasa, kambi ya Samatta inajaribu kuomba msaada kwa viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakazungumze na Katumbi ili akubali kumuacha mchezaji aende klabu aliyochagua.

Rais Mstaafu, Dk Jakaya Mrisho Kikwete ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa chama tawala, CCM, Waziri wa Michezo, Nape Nnauye kwa pamoja wameahidi kumsaidia Samatta katika suala la kumlainisha Katumbi akubali kupokea ofa ya Genk.

Wakati huo huo, Nantes wamekuwa wakimpigia simu Kisongo wakisema wanamsubiri mchezaji aende kusaini, lakini Meneja huyo anakosa majibu ya uhakika.

Inaonekana tayari Katumbi anaujua mchezo wote unaoendelea naye ameamua kukaa kimya akiamini Samatta hawezi kufanya chochote kwa sasa bila baraka zake. Wazo la kusema Samatta asubiri hadi mwezi Aprili atakapomaliza Mkataba wake ili kusaini kama mchezaji huru mwezi Agosti, halifurahiwi hata na Kisongo mwenyewe.

Samatta aliyejiunga na TPM mwaka 2011 akitokea Simba SC aliyoichezea kwa nusu msimu, akitokea African Lyon, hadi sasa ameichezea klabu hiyo mechi 103 na kuifungia mabao 60. Ndani ya mechi hizo, kijana huyo wa umri wa miaka 24, ameshinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na Mazembe, huku naye akiibuka mfungaji bora wa michuano hiyo na kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora Anayecheza Afrika.

Leave A Reply