The House of Favourite Newspapers

Kaze Ampa Tuisila Mapumziko Maalum Yanga

0

WAKATI nyota nane wakijiunga na timu za taifa kwa ajili ya mechi za kuwania kufuzu fainali za Afcon 2021, Kocha Mkuu wa Yanga Mrundi Cedric Kaze amewapa wachezaji mapumziko ya siku nne yatakayomalizika kesho Alhamisi.

 

Kati ya mastaa ambao watafaidika na mapumziko hayo ni Tuisila Kisinda ambaye hakuitwa kwenye timu yake ya taifa ya Congo pamoja na Michael Sarpong raia wa Ghana.

 

Hiyo ni baada ya kumaliza Dar es Salaam, Dabi dhidi ya Simba iliyopigwa wikiendi hii kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.

 

Katika mchezo huo, Yanga ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Mghana Michael Sarpong kabla ya beki wa Simba Joash Onyango kusawazisha.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Kaze alisema kuwa amewapa mapumziko ya siku nne wachezaji wake waliobakia kabla ya kuanza maandalizi ya kuelekea mchezo wao dhidi Namungo FC.

 

Kaze alisema kuwa ametoa mapumziko hayo kwa ajili ya kupumzisha miili ya wachezaji wake sambamba na kwenda kusalimia familia zao kabla ya kurejea kambini kuanza maandalizi ya mchezo huo Namungo.

 

Aliongeza kuwa ametoa muda huo wa mapumziko kutokana na mbeleni kukabiliwa na michezo miwili migumu dhidi ya Namungo na Azam FC ambayo yote wanahitaji pointi tatu.

 

“Ligi imesimama hivi sasa kutokana na baadhi ya wachezaji kuwepo kwenye majukumu ya timu zao za taifa, hivyo nimeona nitoe muda wa mapumziko kwa muda wa siku nne.

 

“Mapumziko hayo yalianza Jumapili baada ya kumaliza mchezo wa dabi dhidi ya Simba, hivyo timu itaanza mazoezi kesho Alhamisi sambamba na wachezaji kuingia kambini.

 

“Tunafahamu umuhimu mkubwa wa michezo yote iliyokuwa mbele yetu na kikubwa tunahitaji ushindi pekee tutakapocheza dhidi ya Namungo na Azam,”alisema Kaze.

Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Leave A Reply