The House of Favourite Newspapers

Kaze Tambo Tupu, Ataja Aina Ya Ubingwa Wa Yanga

0

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mrundi, Cedric Kaze, amesema atahakikisha wanapambana katika kila mchezo kwa kupata matokeo ya ushindi bila ya kupoteza mchezo wowote kwa lengo la kuipa heshima timu hiyo baada ya kumaliza mzunguko wa kwanza bila kufungwa msimu huu.

 

Yanga imemaliza mzunguko wa kwanza bila ya kufungwa katika mechi 17 huku ikiongoza ligi ikiwa na pointi 43 ambapo imempa matumaini makubwa kocha huyo kuendelea kufanya vizuri katika mzunguko wa pili.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Kaze alisema kitendo cha timu hiyo kumaliza mzunguko wa kwanza bila ya kupoteza ni heshima kubwa kwake na kinampa ari kubwa ya kuendelea kupambana kwa kuhakikisha hawapotezi mchezo wowote.“

Nadhani ni jambo kubwa kuwa timu imemaliza mzunguko wa kwanza bila ya kupoteza mchezo wowote, kwetu ni heshima lakini inaonyesha jinsi gani timu inavyocheza kwa kujituma kwa kuhakikisha tunafikia malengo.

 

“Kitu kikubwa ni kuona tunakuwa na malengo mengine ya tofauti katika mzunguko wa pili kwa sababu tunahitaji ubingwa lakini bado heshima inahitajika ila itatokana na nguvu ya timu ikiwa inapambana kama tulivyofanya kwenye mzunguko wa kwanza, najua ushindani utakuwa mkubwa lakini bado haiwezi kuturudisha nyuma,” alisema Kaze

Stoti na Ibrahim Mussa,Dar es Salaam

Leave A Reply