The House of Favourite Newspapers

Kazi Imeanza… Milioni 350 Zashusha Kiungo Simba

0

SIMBA SC inatakiwa kutumia dola 150,000 (sawa na Sh 352,185,000) kumshusha kiungo mkabaji wa St George, Yiech Gatoch Panom raia wa Ethiopia.

Tayari Simba mapema tu imeanza mikakati ya usajili, huku baadhi ya wachezaji wakitajwa kujiunga na timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao.

Kati ya nafasi ambazo Simba wamepanga kuziboresha kwa kusajili wachezaji ni safu ya kiungo mkabaji inayochezwa na Sadio Kanoute, Mzamiru Yassin, Jonas Mkude na Ismael Sawadogo.

Mmoja wa mabosi wa Simba, ameliambia Spoti Xtra kuwa, tayari uongozi wa timu hiyo, wamepeleka ofa ya kumuhitaji kiungo huyo mwenye umbile kubwa kwa ajili ya kuimarisha safu hiyo ya kiungo.

Bosi huyo alisema tayari wameanza mazungumzo ya kumsajili kiungo huyo ambaye uongozi unaamini wakimpata, basi tatizo sugu la kiungo watalimaliza.

Aliongeza kuwa, uongozi wa St George tayari wameitangazia Simba ofa ya kumuachia kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28.

“Yapo maeneo mengi yenye upungufu katika timu yetu, ambayo ni lazima tuyafanyie maboresho, kati ya hayo ipo safu ya kiungo ya ukabaji na Panom ni kati ya wachezaji tuliokuwepo katika mazungumzo naye.

“Hivyo muda wowote tutakamilisha dili hilo la la usajili, uzuri kwamba uongozi wa Simba upo tayari kutoa kiasi hicho cha pesa kuipata saini yake,” alisema bosi huyo.

Akizungumzia hilo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema: “Uongozi upo msituni ukijipanga kwa ajili ya usajili, kweli kabisa yapo baadhi ya majina ya wachezaji tupo nao katika mazungumzo ambayo kama  yakienda vizuri tutamalizana nao.”

Panom amewahi kuzitumikia klabu za Wolaitta Dicha, Al-Anwar, Haras El Hodoud, Makelle City, Ethiopian Coffe, El Gouna na Anzhi Makhachkala ya Urusi.

STORI NA WILBERT MOLANDI

Leave A Reply