The House of Favourite Newspapers

Kesi ya Balali: Wakuu wa Polisi Wafika Mahakamani Kutoa Maelezo

WAKUU wa vituo vya polisi Kijitonyama na Oysterbay leo Ijumaa Oktoba 25, 2019 wameitikia wito wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu walikotakiwa kufika kutoa maelezo ya kukaa na mtuhumiwa kwa siku 14 badala ya kumpeleka gereza la Segerea.

 

Walipofika mahakamani hapo saa 5:34 asubuhi waliingia katika ofisi ya Hakimu mfawidhi, Kelvin Mhina wakiambatana  na wakili wa serikali mwandamizi Wankyo Simon na kuzungumza hadi saa hadi saa 5:50 asubuhi.

 

Baada ya kumaliza mazungumzo hayo waliondoka na mshtakiwa waliyekuwa wakimshikilia katika vituo hivyo, Elizabeth Balali alipandishwa kizimbani.

 

Elizabeth alifikishwa mahakamani hapo Oktoba 10, 2019 akikabiliwa na mashtaka ya kujipatia Sh 25 milioni kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji fedha.

 

Elizabeth anayedaiwa kuwa msimamizi wa mali za mke wa  gavana wa zamani wa Benki Kuu Tanzania (BoT), marehemu Daudi Balali, siku hiyo alisomewa mashtaka  na wakili Wankyo Simon mbele ya hakimu mfawidhi, Kelvin Mhina.

 

Jana Alhamisi Oktoba 24, 2019 mshtakiwa huyo alifikishwa katika mahakama hiyo akitokea kituo cha polisi Kijitonyama, na Hakimu Mhina ambaye alisikiliza kesi hiyo mara ya kwanza kuagiza arejeshwe kituoni na kutaka wakuu wa vituo hivyo kufika mahakamani leo kujieleza.

Leo mbele ya  Hakimu Mhina ambapo wakili Wankyo alieleza mahakama kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi  bado haujakamilika, aliomba ipangiwe tarehe nyingine.

Hakimu Mhina baada ya kusikiliza hoja hizo ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 7, 2019 na kutamka mshtakiwa kupelekwa rumande, “nasisitiza tena mshtakiwa apelekwe rumande.”

 

Akimsomea mashtaka Oktoba 20, 2019 wakili wa Serikali Wankyo Simon alidai  kati ya Oktoba 19 na Desemba 21, 2017 jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alijipatia Sh25 milioni kwa ulaghai kutoka kwa Dk Roderick Kisenge kwa kumuuzia eneo la mita 900 ambalo halijapimwa lililopo Boko Dovya wilayani Kinondoni wakati akijua si lake.

 

Katika shtaka la utakatishaji fedha, Wankyo alidai katika kipindi hicho  mshtakiwa alipokea Sh25 milioni kutoka kwa Dk Kisenge kupitia akaunti yake iliyopo  Benki ya CRDB wakati akijua fedha hizo ni zao la kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

 

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Elizabeth hakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza makosa ya uhujumu uchumi.

 

Hakimu Mhina katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 109/2019 alimueleza mshtakiwa huyo kuwa licha ya mahakama kutokuwa na uwezo wa kuisikiliza, pia shtaka la utakatishaji wa fedha halina dhamana.

 

Siku hiyo ilielezwa mahakamani hapo kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuahirishwa hadi jana ambapo ilibainika kuwa alikuwa katika vituo hivyo badala ya Segerea na leo wakuu hao wa vituo kutakiwa kuripoti kituoni hapo, hakimu kueleza kuwa kesi hiyo itatajwa tena leo..

 

View this post on Instagram

 

A post shared by Global Publishers (@globalpublishers) on

Comments are closed.