The House of Favourite Newspapers

Kesi ya Zitto Kabwe Mahakama Kusikiliza CD

0

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu kesho inatarajia kutoa uamuzi wa ama kupokea kielelezo cha CD iliyohifadhiwa video iliyorekodiwa wakati wa mkutano wa Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe au la.

 

Wakili wa utetezi, Jebra Kambole amedai leo Desemba 3 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa nyaraka inayotakiwa kutolewa na Sajent James ni ya kielektroniki hivyo inatakiwa kufuata maelekezo ya sheria inayohusu utoaji wa kielelezo cha kielektroniki.

 

Amedai CD ambayo inatakiwa kupokelewa mahakamani haijarekodiwa na shahidi huyo hivyo ameshindwa kukithi matakwa ya kifungu 18 (2) (a) cha sheria hiyo ya kielektroniki.

 

Pia, amedai shahidi huyo ameshindwa kuonesha machine iliyotumika kurekodi na kama ilikuwa inafanya kazi vizuri na kuomba mahakamani isipokee kielelezo hicho.

 

Akipinga hoja hizo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga alikiri kuwa kielelezo ambacho shahidi wao anataka kipokelewe kesho na kitumike kama ushahidi mahakamani ni cha kielektroniki. Alidai kitu ambacho shahidi alikuja kukielezea mahakamani hapo ni kuhusu uchunguzi walioufanya katika video kama ni halisi au la.

 

Alidai hakuna kifungu ambacho upande wa utetezi wamekielezea kwamba aliyerekodi video ndio anayepaswa kutoa kielelezo hicho. Kutokana na mabishano hayo, Hakimu Shaidi amesema atatoa uamuzi kesho kama kielelezo hicho kipokelewe au la.

 

Awali, shahidi wa 14 ambaye ni Mtaalamu wa Uchunguzi wa Kisayansi kutoka Makao Makuu ya Polisi, Sajent James (52) alidai alipata barua iliyoambatanishwa na CD kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni ikielekeza kufanya uchunguzi wa picha iliyomo kwenye kielelezo hicho.

 

Alidai barua hiyo ilipewa namba OB/IR/8291/2018 ya Oktoba 10,2018 ililetwa na Koplo Faraji na baada ya kuipokea, mkuu wake wa kazi, SP Tumaini alimpa jukumu la kufanya uchunguzi. Alidai baada ya uchunguzi aligundua kuwa video iliyohifadhiwa kwenye CD ni halisi hivyo aliandaa hati kwa mujibu wa kifungu cha 202 (1) cha Sheria ya Mwendendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

 

Alidai ripoti ya uchunguzi wa kielelezo hicho aliandika Desemba 6, 2018 na kuiomba mahakamani ipokee kielelezo hicho na kioneshwe kilichomo ndani ya CD.

 

Katika kesi hiyo, Zitto anadaiwa Oktoba 28, 2018 akiwa katika mkutano na waandishi wa habari, uliyofanyika katika Makao Mkuu ya ofisi ya Chama cha ACT Wazalendo alitoa maneno ya uchochezi yenye kuleta hisia ya hofu na chuki.

 

Inadaiwa alisema; ” Watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika kituo cha afya Nguruka, Polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kituo cha afya Nguruka kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua”.

Leave A Reply