The House of Favourite Newspapers

Kesi za Talaka Zaongoza

0

 

MASHAURI ya kudai talaka miongoni mwa wanandoa yanaongoza katika idadi ya kesi zinazofunguliwa na kusikilizwa katika mahakama maalum inayotembea, Mahakama hiyo kwa mkoa huu inatoa huduma katika wilaya za Ilemela na Nyamagana.

 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza wakati wa hafla ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu mahakama hiyo ilipoanza kutoa huduma, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama ya mwanzo ya Mkuyuni jijini Mwanza, Jenifer Nkwabi alisema kesi 502 zimefunguliwa mahakamani hapo tangu Julai, 2019, kati ya hizo, zaidi ya kesi 200 ni za kudai talaka.

 

“Kesi nyingine zinazoshika nafasi za juu katika mashauri yaliyofunguliwa mbele ya mahakama inayotembea ni za mashauri ya ndoa, watu kudaiana fedha na mirathi,” alisema Nkwabi.

 

Mratibu wa mahakama hiyo ambayo pia inafanya shughuli zake mkoani Dar es Salaam, Moses Ndelwa alisema hadi kufikia Mei, 2021, jumla ya kesi 1, 208 zilifunguliwa katika mikoa hiyo miwili, huku kesi 520 zilizofunguliwa Mwanza zikiwa zimesikilizwa na kumalizika.

 

“Watu 13,668 wamehudumiwa na mahakama inayotembea kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita,” alisema Ndelwa.

 

Akizungumzia huduma ya mahakama inayotembea, Getruda Stephano, mkazi wa mtaa wa Buhongwa jijini Mwanza alipongeza kuanzishwa kwa huduma ya mahakama inayotembea, akisema inawawezesha wananchi wanaoishi maeneo yasiyo na majengo ya mahakama kupata haki kupitia mkondo wa sheria.

 

Leave A Reply