The House of Favourite Newspapers

Kessy aigomea Simba, ataka mil 60

0

Hassan-‘-Kessy’-Ramadhani2Beki wa Simba, Hassan Ramadhan Kessy.

Khadija Mngwai, Dar es Salaam
BEKI wa Simba, Hassan Ramadhan Kessy, amegomea mkataba wa timu hiyo baada ya ule wa awali kufikia tamati mwishoni mwa msimu huu huku akiutaka uongozi wa timu hiyo kumpa milioni 60 ndiyo akubali kuanguka saini.
Kessy ambaye alisajiliwa Simba kwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu akitokea Mtibwa Sugar ambapo kumekuwa na vuta nikuvute baina yake na klabu yake hiyo tangu atue katika timu hiyo, awali aligoma kucheza kutokana na kutopewa nyumba na kutomaliziwa fedha za usajili.
Hata hivyo, mchezaji huyo ameonekana kuendelea kuwatesa viongozi wa Simba kutokana na kumhitaji mchezaji huyo huku akionyesha kuwa ni wa gharama kubwa.
Kikizungumza na Championi Jumatatu, chanzo cha kuaminika kutoka Simba kimeeleza kuwa, Kessy amewataka viongozi wa timu hiyo kumpa kiasi cha shilingi milioni 60 ili aweze kuanguka saini ya kuendelea kuitumikia timu hiyo, jambo ambalo limewashinda viongozi.
Aidha, inadaiwa kuwa dau hilo kubwa analolitaka mchezaji huyo linachangiwa na tetesi kuwa klabu kubwa za Yanga na Azam FC kumnyemelea hivyo kuwapa ugumu.
“Awali viongozi wa Simba walimuita Kessy ili aweze kuanguka saini, akakataa, hivyo kuleta mvutano na kutaka alipwe milioni 60, kiasi ambacho uongozi hauna uwezo nacho kulingana na hali halisi ya klabu kwa sasa.
“Uongozi unaendelea na mazungumzo na meneja wa Kessy, Athuman Tippo kuona watafikia wapi kwani kiasi cha fedha kilichopo ni kidogo na iwapo itashindikana basi tutaachana naye na kutafuta mbadala wake,” kilisema chanzo hicho.
Simu ya Kessy haikupatikana hewani kwa muda wote tangu juzi na jana hakuwepo hata benchi katika kikosi kilichocheza Kombe la FA dhidi ya Singida United.

Leave A Reply